Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amesema Kenya ni nchi inayoongoza
kwa uwekezaji nchini Tanzania ikilinganishwa na nchi nyingine za Bara
la Afrika.
Rais Magufuli amesema hayo leo
tarehe 31 Oktoba, 2016 katika mkutano na waandishi wa habari
uliofanyika katika Ikulu ya Nairobi nchini Kenya ambako ameanza ziara
ya Kiserikali ya siku mbili kwa mwaliko wa Rais wa Jamhuri ya Kenya
Mhe. Uhuru Kenyatta.
Rais Magufuli ambaye kabla ya
Mkutano huo na waandishi wa habari amepokelewa rasmi kwa kupigiwa
mizinga 21 na kukagua gwaride rasmi lililoandaliwa kwa heshima yake
na baadaye kufanya mazungumzo rasmi na mwenyeji wake Rais Uhuru
Kenyatta, amesema takwimu za kituo cha uwekezaji Tanzania (TIC)
zinaonesha kuwa Kenya ina jumla ya kampuni 529 zinazoendesha shughuli
zake nchini Tanzania ambapo zimewekeza Dola za Marekani Bilioni 1.7
na zimeajiri watu 56,260.
Pia, Rais Magufuli amebainisha kuwa
biashara kati ya Tanzania na Kenya imeongezeka kutoka Shilingi za
Kitanzania Bilioni 652.9 hadi Shilingi za Kitanzania Trilioni 2.044.
"Naomba niwahakikishie kuwa
uhusiano na ushirikiano wetu ni mzuri na utaendelea kuwa mzuri zaidi,
na kwetu sisi Tanzania, Kenya ndio nchi ya kwanza kwa uwekezaji
kuliko nchi zote za Afrika.
"Tunashirikiana vizuri katika
uchumi, watu wetu wanafanya kazi pamoja, yapo makabila yetu ambayo
yanaingiliana kwa shughuli zao za kila siku na hata wanyamapori wetu
wanazunguka katika nchi zote mbili bila kujali mipaka" amesema
Rais Magufuli.
Dkt. Magufuli amesisitiza kuwa
Serikali yake itaendeleza na kuimarisha zaidi uhusiano na Kenya
ulioasisiwa na Rais wa Kwanza wa Tanzania Hayati Mwalimu Julius
Kambarage Nyerere na Rais wa Kwanza wa Kenya Hayati Mzee Jomo
Kenyatta na amewakaribisha wafanyabiashara wengi zaidi wa Kenya
kuwekeza nchini Tanzania.
"Kabla ya kuja hapa nimekwenda
kutoa heshima katika kaburi la Mzee Jomo Kenyatta, kwa kweli
nimeguswa sana na kazi kubwa iliyofanywa na wazee wetu, naomba
niwahakikishie kuwa tunawathamini sana ndugu zetu Wakenya na
tutaendelea kufanya hivyo" amesisitiza Dkt. Magufuli.
Kwa upande wake Rais wa Jamhuri ya
Kenya Mhe. Uhuru Kenyatta amemshukuru Rais Magufuli kwa kukubali
mwaliko wake na amemhakikishia kuwa Kenya itaendeleza na kuimarisha
zaidi uhusiano na ushirikiano na Tanzania.
"Kwetu sisi Tanzania ni ndugu
zetu, ni kaka na dada zetu tunao ushirikiano wa siku nyingi na wa
kidugu na tutahakikisha tunauendeleza ushirikiano na uhusiano huu
mzuri ulioasisiwa na wazee wetu" amesema Mhe. Kenyatta.
Rais Kenyatta amesema Tanzania na
Kenya ni nchi zinazofanana kwa mambo mengi muhimu ikiwemo
kubadilishana uongozi wa Serikali kwa njia ya amani na ameongeza kuwa
katika mazungumzo yao wamekubaliana kuwa nchi hizi zitaendelea
kuzisaidia nchi nyingine za Afrika Mashariki zinazokabiliwa na
matatizo mbalimbali.
Aidha, Rais Kenyatta amesema Kenya
itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kutekeleza miradi ya
ushirikiano ikiwemo ujenzi wa miundombinu kama vile barabara ya
Bagamoyo (Tanzania) hadi Malindi (Kenya) pamoja na mambo mengine
ambayo Tume ya pamoja ya ushirikiano kati ya nchi hizi mbili (Joint
Commission Cooperation) itayaainisha.
Baadaye leo, Rais Magufuli
anatarajiwa kuhudhuria dhifa ya kitaifa katika Ikulu ya Nairobi
aliyoandaliwa na mwenyeji wake Rais Uhuru Kenyatta na Kesho
anatarajiwa kutembelea kiwanda cha maziwa cha Eldoville kilichopo
Karen Jijini Nairobi, na kuzindua barabara mchepuko ya Southern
By-pass iliyopo Jijini Nairobi.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais,
IKULU
Nairobi
31 Oktoba, 2016
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni