Pamela Mollel,Arusha
Watanzania wametakiwa kudumisha amani ya nchi kwa kuepuka kufanya matukio ambayo yanaweza kuchochea vurugu na hatari ya kuliingiza taifa katika hali ya machafuko.
Wito huo umetolewa jana na mchungaji kiongozi wa kanisa la Ukombozi hapa nchini, Nabii B. G Malisa wakati alipokuwa akihubiri neno la Mungu katika viwanja vya reli jijini Arusha na kuhudhuriwa na maelfu ya watu
Nabii Malisa alisema kwamba watanzania wana jukumu kubwa la kuhakikisha wanaombea amani ya nchi iendelee kutawala kwa kuwa bila amani hakuna kitu kitakachoweza kuendelea katika nchi hii
Aidha alisema kuwa amekuwa akifanya ziara mbalimbali katika nchi mbalimbali duniani na kushuhudia hali ya usalama ikiwa tete ambapo askari wamekuwa wakitembea mitaani huku wameshika silaha za moto.
"Hivi karibuni nilikuwa Nigeria wakati nashuka uwanja wa ndege nilipokelewa na askari wenye silaha za moto nikajiuliza maswali mengi sana kuhusu amani tuliyonayo hapa Tanzania "alisema Malisa
Hatahivyo, alitoa wito kwa serikali kuunga mkono juhudi za viongozi mbalimbali wa dini hapa nchini katika kuwasaidia vijana na kusema viongozi wa dini wanafanya kazi kubwa katika kuwainua watu kiuchumi na kuwaepusha na vitendo viovu.
Awali akizungumza na waandishi wa habari mchungaji wa kanisa la Ukombozi tawi la Arusha Mchungaji Ushindi alisema kwamba mhubiri huyo atakwenda kufanya huduma ya maombezi mkoani Arusha kwa siku nane na kuwataka wakazi hao kujitokeza kwa wingi.
Mchungaji Ushindi alisema kuwa wakazi wa jiji la Arusha wamepata neema kubwa ya kupata neno la Mungu kupitia mkutano huo wa maombezi .
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni