WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema
Serikali imeunda timu ya wataalamu ambao watatoa ushauri juu ya suala
zima la kuhamishia makao makuu Dodoma.
Ametoa kauli hiyo leo mchana
(Jumamosi, Oktoba 1, 2016) wakati akizungumza na watumishi wa
Serikali wa mkoa wa Dodoma, wazee wa mkoa huo, wafanyabiashara pamoja
na viongozi mbalimbali kwenye ukumbi wa mikutano wa Dodoma (Dodoma
Convention Centre).
“Tumeunda timu ya watu 10 ambao ni
wataalamu waliobobea kwenye masuala ya ujenzi wa miji mikuu, hawa
wana uzoefu wa kuangalia makao Makuu ya nchi yanafananaje. Watakuja
Dodoma, wapitie master plan na kisha watapita kwenye maeneo kadhaa ya
mji ili waone hali halisi ikoje ndipo watupe maoni yao,” amesema.
“Tunataka tusirudie kosa la Jiji
la Dar es Salaam la kulazimika kubomoa makazi ya watu kila
inapolazimu kufanya uboreshaji wa miundombinu. Hawa watu watatuambia
wapi tunatakiwa tuweke njia nne au sita za magari, wapi tuweke
bustani au wapi tujenge nyumba za ghorofa moja, mbili, tatu au
zaidi,” ameongeza.
Akifafanua kuhusu miundombinu,
Waziri Mkuu amesema timu hiyo pia itatakiwa kutoa ushauri juu ya wapi
ijengwe njia ya malori tu au mahali gani zinahitajika kujengwa
barabara za juu (flyovers) ili kuepusha msongamano katikati ya mji wa
Dodoma.
Bila kutaja majina ya wajumbe wa
timu hiyo, Waziri Mkuu amesema timu hiyo itaongezewa wataalamu kutoka
China na Malaysia ambao nchi zao tayari zina uzoefu wa kuhamisha
makao makuu ya nchi zao zaidi ya mara moja.
Alitumia fursa hiyo kuwaeleza
watumishi juu ya uwepo wa Tume ya Kuboresha Maslahi ya Wafanyakazi
ambayo imekuwa ikifanya kazi tangu mwaka jana. “Kuna vikao vimekuwa
vinafanyika tangu mwaka jana baina ya Serikali na viongozi wa vyama
vya wafanyakazi kwa lengo la kujadili uboreshaji wa maslahi ya
wafanyakazi, na jambo hili linaendelea vizuri,” amesema.
Kuhusu madeni ya watumishi wa umma,
Waziri Mkuu amewasihi watumishi wawe na imani na Serikali yao kuhusu
madeni hayo na kwamba ikimaliza uhakiki unaofanyika hivi sasa, kila
mwenye stahili zake atalipwa.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu
ameutaka uongozi wa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA)
ihakikishe inakamilisha upimaji wa viwanja 100,000 kama
ilivyojipangia ili watumishi hao pamoja na wananchi waweze kupatiwa
viwanja haraka iwezekanavyo.
“Nimearifiwa kuwa mna mpango wa
kupima viwanja 100,000 kwa ajili ya kuwapatia wananchi na watumishi.
Kamilisheni utaratibu huo haraka ili watumishi wapewe viwanja na
waweze kujenga nyumba zao za kuishi,” amesema huku akishangiliwa.
Natambua kuwa mmekubaliana kuanzisha
utaratibu wa kuingiza viwanja kwenye mfumo wa kompyuta ili kuepuka
double allocation. Harakisheni zoezi hilo ili kama itawezekana, kabla
ya Novemba kazi hiyo iwe tayari na watu wapatiwe viwanja chini ya
mfumo huo mpya,” amesisitiza.
Kuhusu huduma za kijamii kama elimu,
umeme, maji na masoko, Waziri Mkuu amewahakikishia watumishi hao
kwamba Serikali imeangalia kila eneo na kuzingatia mapendekezo
yaliyotolewa ili kuboresha utoaji wa huduma hizo. Amewataka watumishi
hao wabadilike na wawe tayari kuwapokea watumishi wenzao
watakaowasili kwa awamu kuanzia mwezi huu.
(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980,
DODOMA
JUMAMOSI, OKTOBA MOSI, 2016.
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni