WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Tanzania ni miongoni mwa nchi saba Barani Afrika ambazo uchumi wake unakua kwa kasi zaidi hivyo amewakaribisha wawekezaji kuja kuwekeza kwenye sekta mbalimbali ikiwemo ya viwanda.
Tanzania ni nchi ya pili kwa kasi ya ukuaji wa uchumi Barani Afrika ambapo uchumi wake unakuwa kwa asilimia 7 ikiongozwa na Ivory Coast inayokua kwa asilimia 8.5, Senegal ya tatu (asilimia 6.6), D’jibout ya nne (asilimia 6.5), Rwanda ya tano (asilimia 6.3), Kenya ya sita (asilimia 6.0) na Msumbiji ya saba (asilimia 6.0).
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo jana jioni (Alhamis, Oktoba 13, 2016) wakati akifungua kongamano la Jumuiya ya Dawoodi Bohora lililohusu fursa za uwekezaji.
Amewakaribisha wanajumuia hiyo kuja kuwekeza nchini. Kongamano hilo lilifanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Mwalimu Nyerere.
“Tanzania ina sera nzuri za kiuchumi ambazo zimesababisha uchumi wake kuendelea kuwa imara kwa zaidi ya miongo miwili sasa. Naikaribisha jumuiya ya Bohora kuja kuwekeza na kufanya biashara Tanzania,” alisema.
Waziri Mkuu alisema makampuni yatakayowekeza nchini yatafaidika na uwepo wa malighafi za kutosha, sera nzuri uwekezaji pamoja na uhakika wa usalama wa mali zitakazowekezwa nchini kwa sababu ya hali ya amani na utulivu iliyoko nchini.
Alisema licha ya Tanzania kuwa maeneo mazuri kwa ajili ya uwekezaji pia ina soko la uhakika kwa sababu ya kuwa mwanachama wa jumuiya mbili ambazo ni Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) zenye watu takriban milioni 600.
“Tanzania ni kitovu cha biashara kwani inapakana na nchi nane ambazo kati yake nchi sita zinatumia bandari ya Dar es Salaam kusafirisha mizigo yake. Mizigo hiyo husafirishwa kwa njia ya reli na barabara,” alisema.
Nchi zinazopakana na Tanzania ni Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Malawi, Zambia, Msumbiji, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC). Zinazotumia bandari ya Dar es Salaam ni Uganda, DRC, Rwanda, Burundi, Malawi na Zambia.
Kwa upande wake Mratibu wa Kongamano hilo la kidini (Ashara Mubarak) lililowakutanisha Mabohora kutoka duniani kote Bw. Murtaza Adamjee ameahidi kushirikiana na Serikali katika kutangaza fursa za uwekezaji zilizoko nchini.
Bw. Adamjee alimuhakikishia Waziri Mkuu kwamba Mabora dunia nzima wanakuja Tanzania kuwekeza katika sekta mbalimbali hususan ya viwanda. “Tutafikisha ujumbe kwa Mabohora dunia kote kwamba Tanzania ni sehemu salama ya kuja kuwekeza,”
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
2 MTAA WA MAGOGONI,
S. L. P. 3021,
11410 - DAR ES SALAAM. IJUMAA, OKTOBA 14, 2016.
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni