Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, akitoa maelekezo kwa Mkuu wa Kivuko cha MV. Chato, Eng. Fredinand Mishamo (Wa kwanza kushoto), alipokagua kivuko hicho, wilayani Chato, mkoani Geita.
Fundi wa Kivuko cha Mv Chato kutoka Wakala wa Ufundi na Umeme Nchini (TEMESA), Bw. Mbondo Jackson, akimweleza Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, namna injini ya Kivuko cha MV. Chato inavyotumia mafuta, alipotembelea kivuko hicho, wilayani Chato, Geita.
Muonekano wa Kivuko cha MV Chato kilichopo Wilaya ya Chato mkoani Geita.
Mkuu wa Mkoa wa Geita, Meja Jenerali Mstaafu Ezekiel Kyunga, akimuonesha Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa (mwenye shati la blue), ramani inayoonesha mtandao wa barabara za mkoa wa Geita, alipomtembelea Ofisini kwake.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, akisisitiza jambo kwa wafanyakazi wanaofanya kazi kwenye Sekta ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (hawapo pichani), alipoongea nao Mkoani Geita.
Serikali kupitia Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS), imeanzisha Kitengo maalum cha Wahandisi Washauri (TECU), ili kuwajengea uwezo wahandisi wazawa kusimamia miradi ya ujenzi wa barabara nchini na hivyo kuokoa kiasi kikubwa cha fedha ambacho kingetumika kuwalipa wahandisi washauri kutoka nje ya nchi.
Akizungumza mkoani Geita mara baada ya kukagua mradi wa ujenzi wa barabara ya Uyovu-Bwanga-Biharamulo yenye urefu wa KM 112 ambayo pia inasimamiwa na Wahandisi Washauri Wazawa, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa amesema mpaka sasa wahandisi wazawa wanasimamia miradi mbalimbali ya barabara katika mikoa ya Kagera, Mwanza, Geita na Kilimanjaro ambapo kupitia miradi hiyo serikali imeokoa dola za kimerani milioni mbili ambazo zingetumika kulipa wahadisi kutoka nje ya nchi.
“Nitahakikisha ninakijengea uwezo kitengo hiki ili kuweza kuokoa fedha nyingi zaidi. Nimeridhishwa na usimamizi wa wahandisi hawa katika barabara hii ambayo ipo katika hatua nzuri”, amesema Prof Mbarawa.
Waziri Mbarawa ameongeza kuwa Serikali itahakikisha kuwa miaka mitano ijayo miradi yote mikubwa nchini itasimamiwa na Wakala huo ili kuokoa fedha za ndani na badala yake fedha hizo kuelekezwa kwenye miradi mingine ya ujenzi.
Kwa upande wake, Meneja wa TANROADS, mkoa wa Geita Eng. Harun Senkuku amesema kuwa mradi wa ujenzi wa barabara ya Uyovu-Bwanga umefikia asilimia 47 na Bwanga – Biharamulo umefikia asilimia 42 na ujenzi wake unagharimu zaidi ya shilingi Bilioni 90.
Aidha, Eng. Senkuku amemuahidi Waziri huyo kukamilisha ujenzi huo kwa wakati ili wananchi wa mikoa ya kagera na Geita kuweza kutumia barabara hiyo.
Naye, Mhandisi Msahauri kutoka TECU Eng. Gladson Yohana amesema kuwa kusimamia miradi mikubwa kama hiyo kumewasaidia kujifunza zaidi kwa vitendo na amemuhakikishia Waziri huyo kusimamia barabara hiyo kwa kuzingatia ubora na viwango vinavyotakiwa.
Katika hatua nyingine Waziri Prof. Mbarawa amekagua kivuko cha MV. Chato na kumuagiza Meneja wa Wakala wa Ufundi na Umeme nchini (TEMESA), mkoa wa Geita Eng. Fredinand Mishamo kuhakikisha kuwa kivuko hicho kinajiendesha chenyewe kutoka kwenye mapato yanayopatikana.
Prof Mbarawa amemtaka Meneja huyo kuhakikisha kuwa mapato yatokanayo na kivuko hicho yanaongezeka ili kuweza kusaidia changamoto ndogondogo katika kivuko hicho.
Eng.Mishamo amemuelezea Waziri huyo changamoto zinazokabili kivuko hicho kuwa ni kukosa maegesho katika baadhi ya maeneo.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni