.

.

.

.

.

.

.

.
KARIBUNI TUHABARIKE, TUELIMISHANE, TUPEANE HABARI ZA KUKUFANYA UTABASAMU KIDOGO NA MATUKIO YALIYOFANYIWA UCHUNGUZI WA KINA TOKA KILA PEMBE CONTACTS: +255 787 377 722 Email: drweyunga@gmail.com PIA UNAWEZA KUNI FOLLOW KUPITIA INSTAGRAM YANGU @drweyunga | TANGAZA NASI ILI UWAFIKIE WATU WENGI ZAIDI.

Jumamosi, 15 Oktoba 2016

WAZIRI MKUU APOKEA MSAADA WA SH. MILIONI 27.62

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amepokea fedha taslimu sh. milioni 25.62 pamoja na nguo zenye thamani ya sh. milioni mbili kutoka kwa wadau mbalimbali.

Makabidhiano ya michango hiyo yamefanyika leo (Ijumaa, Oktoba 14, 2016) kwenye ukumbi wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Magogoni jijini Dar es Salaam.

Akiwashukuru wadau hao Waziri Mkuu ameahidi kuwa Serikali itahakikisha michango hiyo inafikishwa Kagera kwa walengwa.

“Nawashukuru kwa kuamua kutumia siku ya leo ya kukumbuku ya kifo cha Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Nyerere kuwachangia wenzetu waliopatwa na maafa,” amesema.

Waziri Mkuu amesema michango hiyo ni muhimu na inaonyesha mshikamano wa dhati uliopo baina ya Watanzania.

Misaada hiyo imetolewa na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) sh. milioni 20, Mtandao wa Wasanii Tanzania sh. 620,000 na nguo mifuko miwili, Chama cha Makatibu Mahsusi (TAPSEA) sh. milioni tano.

Wengine ni Umoja wa Wafanyabiashara Ndogondogo soko la Kariakoo ambao wametoa marobota mawili ya nguo (suruali, kanzu na nguo za akinamama na moja la wanasesere kwa ajili ya watoto waliopatwa na maafa vyote vikiwa na thamani ya sh. milioni mbili.

Fedha na nguo hizo vimetolewa kwa ajili ya wananchi walioathirika na tetemeko la ardhi lililotokea mkoani Kagera Jumamosi, Septemba 10, mwaka huu na kusababisha vifo vya watu 17 na wengine 440 walijeruhiwa.

Pia tetemeko hilo limesababisha nyumba 2,063 kuanguka huku nyingine 14,081 zikiwa katika hali hatarishi na 9,471 zimepata uharibifu mdogo huku wananchi 126,315 wakihitaji misaada mbalimbali .

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
2 MTAA WA MAGOGONI,
S. L. P. 3021,
11410 DAR ES SALAAM

Hakuna maoni :

Chapisha Maoni