.

.

.

.

.

.

.

.
KARIBUNI TUHABARIKE, TUELIMISHANE, TUPEANE HABARI ZA KUKUFANYA UTABASAMU KIDOGO NA MATUKIO YALIYOFANYIWA UCHUNGUZI WA KINA TOKA KILA PEMBE CONTACTS: +255 787 377 722 Email: drweyunga@gmail.com PIA UNAWEZA KUNI FOLLOW KUPITIA INSTAGRAM YANGU @drweyunga | TANGAZA NASI ILI UWAFIKIE WATU WENGI ZAIDI.

Alhamisi, 17 Novemba 2016

BALOZI SEIF ASISITIZA MIUNDOMBINU BORA KATIKA MAJENGO YA MAABARA

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akikata utepe kuashiria kuzindua pamoja na kukabidhi Jengo la Maabara la Skuli ya Sekondari ya Kitope aliloligharamia yeye pamoja na ufadhili wa Ubalozi China Nchini Tanzania na Kampuni ya simu za mkononi yaTigo.
Mwalimu wa Masomo ya Sayansi wa skuli ya Sekondari Kitope Mwalimu Ali Mohamed aliyeshika kifaa cha Maabara akimuelezea Balozi Seif urahisi wa kazi yao ya ufundishaji kwa sasa baada ya kupata Maabara yenye kukidhi kiwango kinachokubalika kwa skuli za Sekondari.Kushoto ya Mwalimu Ali ni msimamizi wa ujenzi wa jengo hilo Bwana Yaser De Costa.
Mwalimu Ali Mohamed akiendelea kutoa maelezo kwa Balozi Seif jinsi wanafunzi wa masomo ya sayansi katika skuli yao walivyofarajika kutokana na kujengewa maabara iliyokamilika kwa kazi zao za vitendo. Kulia ya Mwalimu Ali ni Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mheshimiwa Riziki Pemba Juma.
Mwalimu Wanu Ndende Juma akiwasilisha Risala ya walimu na wanafunzi wa skuli ya Sekondari ya Kistope kwenye hafla ya uzinduzi na kukabidhiwa rasmi jengo la Maabara ya skuli hiyo lililomalizika kujengwa pamoja na kuwekwa vifaa vyake.
Baadhi ya Wanafunzi wa skuli ya sekondari ya Kitope wakifuatilia matukio mbali mbali yaliyojiri kwenye uzinduzi wa maabara ya skuli yao.

Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini “B” Ndugu Issa Juma akitoa salamu katika hafla ya uzinduzi wa jengo jipya la maabara ya skuli ya sekondari ya kitope.
Kulia ya Ndugu Issa ni Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mh.Mmanga Mjengo Mjawiri, Mke wa Mwakilishi wa Jimbo la Mahonda Mama Asha Suleiman Iddi, na kushoto ya Nd. Issa ni Balozi Seif Ali Iddi, Waziri wa Elimu Mh. Riziki Pemba Juma na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Bibi Khadija Bakari.
Waziri wa Elimu Mh. Riziki Pemba Juma akimshukuru Mwakilishi wa Jimbo la Mahonda Balozi Seif kwa uzalendo wake wa kuunga mkono sekta ya Elimu wakati wa hafla ya uzinduzi wa Maabara ya skuli ya Kitope.

Kulia ya Mh. Riziki ni Mwakilishi wa Jimbo la Mahonda Balozi Seif Ali Iddi na kushoto ya Mh. Riziki ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu Bibi Khadija Bakari, Mwalimu Mkuu wa Skuli ya Sekondari ya Kitope Nd. Suleiman Juma na Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kaskazini “B” Nd. Hilika Fadhil Ibrahim.
 

                                                                                              Picha na – OMPR – ZNZ.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliitahadharisha Jamii kuelewa kwamba maendeleo kwa wana Taaluma wa Fani ya Sayansi iwe Maskulini au vyuoni yataendelea kuwa ndoto iwapo hakutakuwa na mipango imara ya kuimarisha miundombinu kwenye Majengo ya Maabara katika maeneo husika.

Alisema Wazazi kwa kushirikiana na Kamati za Maskuli na vyuo kupitia usimamizi wa Wizara inayosimamia masuala ya Elimu bado wana jukumu la kuhakikisha vilio vya Wanafunzi kutokana na kukabiliwa na ukosefu wa Maabara kwenye Taasisi zao vinamalizika.

Balozi Seif Ali Iddi ambae pia ni Mwakilishi wa Jimbo la Mahonda alitoa tahadhari hiyo wakati wa hafla fupi ya kukabidhi pamoja na kulizindua rasmi Jengo la Maabara ya Skuli ya Sekondari ya Kitope iliyomo ndani ya Wilaya ya Kaskazini “B”.

Jengo hilo aliloligharamia yeye pamoja na kupata msaada wa nguvu za ufadhili wa baadhi ya vifaa kutoka Ubalozi wa Jamuhuri ya Watu wa China na Kampuni ya mitandao ya simu za mkononi ya Tigo limegharimu jumla ya shilingi za Kitanzania Milioni 38,780,000/-.

Balozi Seif alisema wanafunzi wa Skuli ya Sekondari ya Kitope kwa sasa hawana sababu ya kufanya vibaya katika mitihani yao ya Kitaifa kutokana na kumalizika kwa Jengo hilo la Maabara ambalo lilikuwa kilio kwao na walimu wao kwa karibu miaka Kumi sasa.

Aliwaasa Wanafunzi hao kuhakikisha kwamba Vifaa walivyopatiwa kwenye Maabara ya Skuli yao wataendelea kuvitunza kwa tahadhari ili viweze kudumu kwa kipindi kirefu na kutumiwa pia na wanafunzi wenzao watakaofuatia baada ya wao.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif aliupongeza na kuushukuru Uongozi wa Ubalozi wa Jamuhuri ya Watu wa China hapa Nchini pamoja na ule wa Kampuni ya Mitandao ya Simu za mkononi wa Tigo kwa upendo wao wa kuunga mkono Sekta ya Elimu hapa Zanzibar.

Katika kusaidia kupunguza changamoto zinazowakabili walimu na wanafunzi wa skuli ya sekondari ya Kitope Balozi Seif aliahidi kuwapatia mashine Moja ya Fotokopi itakayosaidia kukidhi mahitaji yao hasa wakati wa kujiandaa na mitihani ya majaribio.

Balozi Seif aliuagiza Uongozi wa Skuli hiyo kufanya tathmini ya matengenezo ya vyoo, milango na madirisha kwa Darasa wanaloendelea kulijenga kwenye skuli hiyo na kumpatia gharama zinazohitajika kwa ajili ya kuangalia mbinu zitakazosaidia kukamilisha ujenzi huo.

Mwakilishi huyo wa Jimbo la Mahonda aliwahakikishia Wananchi wa Jimbo hilo kwamba kazi kubwa iliyopo mbele kwa Viongozi wa Jimbo hilo ni kupeleka nguvu zao katika uimarishaji miundombinu ya Maabara kwa Skuli iliyobakia ya Sekondari ndani ya Jimbo hilo iliyopo katika Kijiji cha Mahonda.

Akisoma risala kwa niaba ya walimu na wanafunzi wa Skuli ya Sekondari ya Kitope Mwalimu Wanu Ndende Juma amemuelezea Mwakilishi wa Jimbo liliomo Skuli hiyo Balozi Seif Ali Iddi kuwa anapenda Elimu kiasi kwamba amekuwa mdau muhimu na mshirika mkubwa katika maendeleo ya skuli ya Kitope.

Mwalimu Wanu alisema juhudi za Mwakilishi huyo zimewezesha kulipatia ufumbuzi wa kudumu tatizo zito la ukosefu wa Maabara lililokuwa likiwakabili wanafunzi pamoja na walimu wa Kitope kwa miaka mingi na kupelekea wanafunzi wengi waliowahi kusoma skuli hiyo kukosa mafunzo ya vitendo.

Wamemshukuru na kumpongeza Balozi Seif kwa uzalendo wake wa kujikubalisha kuwa Mkombozi katika kuchangia Sekta ya Elimu uliomuwezesha ndani ya kipindi cha Miezi Mitatu kufanya mambo mengi katika Sekta hiyo kwenye Jimbo analolitumikia la Mahonda.

Mapema Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mheshimiwa Riziki Pemba Juma aliwaomba Wanafunzi wa Skuli hiyo ya Sekondari Kitope kuongeza juhudi katika masomo yao hasa yale ya fani ya Sayansi ili kujitengenezea fursa pana ya kuendelea na masomo yao katika viwango vya Vyuo vya juu.

Mh. Riziki alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali imeanzisha utaratibu maalum wa kutenga nafasi kumi za kufadhili wanafunzi watakaopata Daraja la Kwanza kwenye Mitihani yao ya Kidato cha sita katika Fani ya Sayansi ili waendelee na masomo yao katika kiwango cha Digirii ya kwanza.

Waziri Riziki alisema ataona fahari itakapofikia wakati miongoni mwa wanafunzi watakaobahatika kupata fursa hiyo za kuendelea na elimu ya Digirii wanatoka katika skuli ya Sekondari ya Kitope kutokana na miundombinu waliyoekewa ya upatikanaji wa huduma za Maabara Skulini pao. 


Othman Khamis Ame 
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar 
17/11/2016.


Hakuna maoni :

Chapisha Maoni