.

.

.

.

.

.

.

.
KARIBUNI TUHABARIKE, TUELIMISHANE, TUPEANE HABARI ZA KUKUFANYA UTABASAMU KIDOGO NA MATUKIO YALIYOFANYIWA UCHUNGUZI WA KINA TOKA KILA PEMBE CONTACTS: +255 787 377 722 Email: drweyunga@gmail.com PIA UNAWEZA KUNI FOLLOW KUPITIA INSTAGRAM YANGU @drweyunga | TANGAZA NASI ILI UWAFIKIE WATU WENGI ZAIDI.

Alhamisi, 24 Novemba 2016

HATUTAWAVUMILIA WAAJIRI WASIOTOA MIKATABA – MAJALIWA

* COTU –Kenya yasema wanatamani Rais Magufuli aende kwao kwa mwaka mmoja

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali haitawavumilia waajiri ambao hawatoi mikataba ya ajira kwa wafanyakazi wao na amewaonya waache tabia hiyo mara moja.

“Nitoe wito kwa waajiri wote ambao wamekuwa na tabia ya kutokutoa mikataba ya ajira kwa wafanyakazi wao, waache tabia hiyo mara moja, kwani Serikali haitamvumilia mwajiri wa namna hii,” alionya.

Ametoa agizo hilo leo (Jumatano, Novemba 23, 2016) wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Sita wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) katika ukumbi wa Mwalimu Julius K. Nyerere ulioko Chuo cha Mipango, nje kidogo ya mji wa Dodoma.

Akijibu hoja ya waajiri kutokutoa mikataba ya ajira kwa wafanyakazi ambayo iliibuliwa kwenye risala yao, Waziri Mkuu amesema kifungu cha 14 cha Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini Na. 6 ya mwaka 2004 kinaelekeza aina mbalimbali za mikataba inayotakiwa kutumika kuajiri wafanyakazi. “Kisheria mwajiri anao wajibu wa kuhakikisha kila mtumishi wake ana mkataba wa kazi kwa maandishi,” alisisitiza.

“Pia ninawaagiza maafisa wa kazi wanaohusika na kaguzi za kazi kote nchini, wahakikishe kila mwajiri anafikiwa wakati wa ukaguzi na hatua stahiki zinachukuliwa kwa wote wasiotekeleza matakwa ya Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini,” alisisitiza.

Alisema mkataba wa ajira ni haki ya mfanyakazi na ndiyo ufunguo wa mahusiano mema yanayoweza kuleta utulivu, amani, kuongeza tija na uzalishaji sehemu ya kazi.

Akijibu hoja kuhusu wafanyakazi kuwekwa ndani kiholela, kunyanyaswa, kushushwa vyeo na kusimamishwa kazi na wanasiasa, Waziri Mkuu alisema Serikali chini ya uongozi wa Dkt. John Pombe Magufuli itaendelea kuzingatia utawala wa sheria na kanuni za utawala bora ili kuhakikisha kuwa haki za wafanyakazi zinalindwa ipasavyo.

”Kimsingi watumishi wanasimamiwa na mamlaka za kinidhamu na sheria mbalimbali ambazo hazina budi kuangaliwa kwa pamoja kabla ya kuchukua hatua. Ninawaagiza viongozi wenzagu wa kisiasa na walioko katika wizara na taasisi zote za Serikali, mikoani, wilayani, kwenye idara za Serikali na Halmashauri wazingatie utawala wa sheria wakati wa kushughulikia masuala mbalimbali yanayohusu wajibu na haki za wafanyakazi,” alisema huku akishangiliwa.

Risala yao iligusa maeneo mengine kama vile watumishi wa umma kutopandishwa vyeo kwa wakati muafaka; walitaka kujua bodi za mishahara za kisekta zitaanza kazi lini; kukosekana kanuni za uandikishwaji wa vyama vya wafanyakazi na waajiri; marekebisho ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii na ucheleweshwaji wa malipo ya pensheni; haja ya kuoanisha Sheria ya Utumishi wa Umma ya mwaka 2002 na Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini ya mwaka 2004.

Akijibu baadhi ya hoja hizo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi Ajira na Vijana) Bibi Jenista Mhagama alisema dhana ya utatu baina ya wafanyakazi, waajiri na Serikali ndiyo nguzo kuu ya kukuza uchumi wa Tanzania.

Akifafanua kuhusu fao la kujitoa, Waziri Mhagama alisema baada ya uongozi wa TUCTA kukamilika, itabidi wakutane na kukaa pamoja kuainisha sera inataka nini na hali ya uchumi ya sasa ikoje huku wakiangalia dhana nzima ya hifadhi ya jamii nayo inataka nini.

“Kuna haja ya kuangalia sera inataka nini, tunapaswa tuangalie mabadiliko ya kiuchumi katika nchi yetu na kutazama dhana nzima ya hifadhi ya jamii kwenye maisha yetu ya uzeeni. Tukikaa pamoja, yaani, mwajiri, mfanyakazi na Serikali, tutapata njia ya kisheria ya kuweza kulifunga jambo hili ili lisiendelee kuwa kero kwa wafanyakazi wetu,” alisema.

Akijibu hoja kuhusu suala la watumishi kutopandishwa vyeo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora), Bibi Angella Kairuki alisema kwa kipindi cha miaka mitano jumla ya watumishi 343,689 walipandishwa vyeo ikiwa ni kuanzia mwaka 2011 hadi 2016. Hata hivyo, alisema wanakabiliwa na changamoto ya watumishi wengine kutokidhi vigezo.

“Kuna baadhi ya watumishi hawakidhi vigezo vya maendeleo na masharti vya muundo wa masharti ya utumishi wa umma. Tumetoa maelekezo kuwa wale waliokosa vigezo na wamekaa muda mrefu bila kupandishwa vyeo, wapewe mafunzo na bajeti zitengwe ili waweze kutimiza vigezo vya muundo wa utumishi wa umma,” alisema.

Katika hatua nyingine, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi nchini Kenya (COTU), Bw. Francis Atwoli alisema anaikubalia kasi ya Rais Magufuli katika kupambana na rushwa na kuwataka Watanzania wamuunge mkono badala ya kulalamikia kasi kwani wao wanatamani mwakani aende kugombea kwao katika uchaguzi mkuu ujao.

“Ninawasihi wanaTUCTA suala la rushwa msilipe nafasi. Mpambane nayo kwa sababu kule kwetu imeota mizizi. Muungeni mkono Rais Magufuli, badala ya kulalamika kuwa kasi yake ni kubwa mno. Mnasema eti ana spidi sana, mkiona taabu mtuazime japo kwa mwaka mmoja ili aje atunyooshee mambo kule kwetu,” alisema huku akishangiliwa.

Aliwataka wahimize uhusiano uliopo baina ya vyama vya wafanyakazi, waajiri na Serikali iliyopo madarakani na kuwataka wadumishe umoja miongoni mwa viongozi na wanachama mara baada ya kumalizika kwa uchaguzi.

“Msiruhusu mgawanyiko wa makundi baada ya uchaguzi sababu hauwasadii wafanyakazi ambao ni wanachama wenu. Mmeona madhara ya kuendeleza makundi kule nchini kwetu, msiruhusu hayo yatokee hapa,” alionya.

TUCTA inatarajiwa kufanya uchaguzi wake kesho (Alhamisi, Novemba 24, 2016) na kuchagua uongozi mwingine utakaongoza kwa kipindi cha miaka mitano. Uchaguzi wa mwisho ulifanyika 2011.

IMETOLEWA NA:

OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980,DODOMA.

Hakuna maoni :

Chapisha Maoni