.

.

.

.

.

.

.

.
KARIBUNI TUHABARIKE, TUELIMISHANE, TUPEANE HABARI ZA KUKUFANYA UTABASAMU KIDOGO NA MATUKIO YALIYOFANYIWA UCHUNGUZI WA KINA TOKA KILA PEMBE CONTACTS: +255 787 377 722 Email: drweyunga@gmail.com PIA UNAWEZA KUNI FOLLOW KUPITIA INSTAGRAM YANGU @drweyunga | TANGAZA NASI ILI UWAFIKIE WATU WENGI ZAIDI.

Jumanne, 1 Novemba 2016

NI MUHIMU WA ICC NA AFRIKA KUZUNGUMZA - TANZANIA

Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa,Balozi Tuvako Manongi akizungumza wakati Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipopokea na kujadili Ripoti ya Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai ( ICC) hapo jumatatu. Katika kuchangia Ripoti hiyo, Tanzania imesisitiza haja na umuhimu kwa ICC kukaa na kuzungumza na Nchi za Afrika ili kutafuta suluhu ya misuguano baina ya pande hizo mbili.

                                                                               Na Mwandishi Maalum, New York

Jamhuri ya Muugano wa Tanzania imeishauri Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai ( ICC) kukaa meza moja na nchi wanachama wa Mkataba wa Roma hususani zile za Afrika ili kutafuta suluhu ya changamoto na tofauti zilizopo kati ya mahakama hiyo na wanachama wake.
 

Tanzania imetoa wito huo siku ya jumatatu kupitia Mwakilishi wake wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Balozi Tuvako Manongi, wakati Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, lilipopokea na kujadili Taarifa ya Utendaji ya Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai.

Taarifa ICC imewasilishwa na Rais wa mahakama hiyo Jaji Slivia Fernandez de Gumendi katika kupindi ambacho Jumuiya ya Kimataifa imekumbwa na taharuki baada ya wanachama wawili wa Mkataba wa Roma, Afrika ya Kusini na Burundi kuwasilisha rasmi katika Umoja wa Mataifa kusudio la kujiondoa huku Gambia nayo ikitangaza kutaka kujitoa ingawa bado haijawasilisha rasmi nia yake hiyo.

Mwakilishi huyo wa Tanzania katika mchango wake amesema, uwepo au kuanzishwa kwa ICC kulitokana kwa kiasi kikubwa na uungwaji mkono kutoka Afrika.

Akasema uungwaji mkono huo ulitokana hasa baada ya nchi hizo za Afrika kukatishwa tamaa na kuvunjika moyo baada ya kutokea kwa mauaji ya kimbari nchini Rwanda.

“Baada ya kukatishwa tamaa na kuvunjwa moyo, Mahakama hii, ilikuja kuwa chombo cha kutenda haki dhidi ya watu waliojihusisha na vitendo vya kikatili vikiwamo vya ukatili dhidi ya binadamu, uhalifu kivita na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu. Madhira yasiyoelezeka yaliyotokea Barani Afrika yakaifanya mahakama hii kuwa chombo cha matumaini dhidi ya wale ambao hawakuweza kuguswa au walikuwa juu ya sheria”. Akasema Balozi Manongi

Na kuongeza. “ Kama nchi mwanachama wa Mkataba wa Roma wa Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai na Mwanachama wa Umoja wa Afrika. Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatambua kwamba, uhusiano kati ya mahakama na Afrika ni ule wa misuguano, na ni uhusiano ambao umeleta hofu ya Afrika kujitoa”.



Balozi Tuvako Manongi akaeleza zaidi kwamba, hofu hiyo ya kujitoa kwa Afrika katika mahakama hiyo, haipaswi kuwepo kutokana na mambo kadhaa ambayo Afrika imejipanga kuyatekeleza kwa manufaa ya bara hilo na watu wake.
 

Baadhi ya mipango hiyo ni utekelezaji wa ajenda ya Maendeleo ya Umoja wa Afrika maarufu kama agenda 2063 ambayo pamoja na mambo mengine inachagiza katika utawala bora, demokrasia, usawa wa jinsia, kuheshimu haki za binadamu, haki na utawala wa sheria..

“Viongozi wa wakuu wa nchi na serikali wa Afrika wameutangaza mwaka 2016 kuwa mwaka wa haki za binadamu huku mkazo ukielekezwa katika haki za wanawake. Na katika kutambua kuwa Amani na Haki ni vitu ambavyo haviwezi kutenganishwa, kwa sababu hizo, tunachotakiwa kuhimiza leo sana sana ni majadiliano”.Akasisitiza Balozi.

Tanzania pia ikaeleza kwamba ni vema Mahakama hiyo katika utekelezaji wa majukumu yake ikajenga mazingira ya kuaminiana kati yake na wanawachama wake.

Tanzania pia kupitia Mwakilishi wake, imezitaka nchi hususani zile za mataifa yaliyoendelea kuacha kuzihubiria nchi zinazondelea kama vile zenyewe ni adilifu sana. Na kusisitiza kwamba, kinachotakiwa wakati huu si kunyosheana vidole au kulaumiana bali kufanya kazi kwa pamoja ili kuifanya mahakama hiyo iendelee kutekeleza majukumu yake kwa uwazi , haki na kuaminiwa.

Akasisitiza pia kuwa hata kama matatizo yaliyopo baina ya ICC na Africa yatapatiwa ufumbuzi. Bado kuna haja na umuhimu kwa nchi za Afrika kuziimarisha na kuzijengea uwezo Taasisi zake na vyombo vinavosimamia utoaji wa haki na utawala wa sheria ili viweze kushughulikia makosa ya jinai yakiwamo ya ukatili dhidi ya binadamu na uhalifu wa kivita badala ya kusubiri au kutegemea mahakama za kimataifa kama ICC.

Akabinisha kuwa nchi zinatakiwa kuwajibika kikamilifu siyo kwa kuhofia kuingiliwa mambo yao ya ndani na ICC bali kwa sababu zinaowajibu wa kwanza wa kuwalinda raia wao.

“Kwa Afrika matukio kama yale ya Jamhuri ya Afrika ya Kati, Cote d’ Ivore, Rwanda na Sierra-Leone ni kielelezo cha hatari ambayo tunatakiwa kujikinga nayo.

Vile vile Tanzania imelitaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, kutopeleka ICC rufaa zenye malengo wa kisiasa kwani kwa kufanya hivyo kunachangia kuharibu sifa ya ICC na kuifanya isiaminiwe na kuonekana inatumiwa na wakubwa kutimiza malengo yao.

Pamoja na kulitaka Baraza la Usalama kutoingiza siasa katika rufaa zake, Tanzania pia imewashangaa baadhi ya wajumbe wa Baraza hilo na ambao si wanachama wa Mkataba wa Roma kuwa mstari wa mbele katika kupeleka rufaa kwenye Mahakama hiyo dhidi ya mataifa mengine.

Wazungumzaji wote zaidi ya 50 walioomba kuchangia Taarifa hiyo ya ICC pamoja na kuzungumzia utendaji kazi na changamoto zinazoikabili Mahakama hiyo, walijielekeza zaidi katika kuelezea masikitiko yao juu ya uamuzi wa Afrika ya Kusini na Burundi kujitoa.

Wasemaji hao kama ilivyokuwa kwa Tanzania walisisitiza sana umuhimu wapande zinazopingana kukaa mezani na kuzungumza huku baadhi yao wakizitaka Afrika ya Kusini na Burundi kufikiria upya uamuzi huo.

Hakuna maoni :

Chapisha Maoni