Serikali ya Tanzania imeshukuru msaada mkubwa unaotolewa na Mashirika ya Umoja wa Mataifa katika kuhakikisha kwamba taifa linakuwa na mfumo imara wa utoaji haki kwa kuzingatia demokrasia na uwajibikaji.
Serikali imesema kumekuwepo na mabadiliko makubwa katika mfumo ya utoaji haki nchini kutokana na misaada iliyotolewa na nchi hizo kupitia Mashirika ya Umoja wa Mataifa ambao unasaidia mpango huo wa UNDAP.
Hayo yameelezwa wakati ujumbe mzito wa kutoka nchi za Nordic ulipotembelea Wizara ya Mambo ya Katiba na Sheria. Nchi hizo za Nordic pamoja kutoa mchango wake mkubwa katika bajeti za serikali ya Tanzania pia hutoa mchango mkubwa kwa mashirika ya Umoja wa Mataifa yanayofanya shughuli zake nchini.
Mataifa hayo ni ya Sweden, Norway, Denmark, Finland na Iceland ambayo kwa pamoja yanaitwa mataifa ya Nordic ni wadau muhimu wa Umoja wa Mataifa na pia kwa serikali ya Tanzania.
Ujumbe kutoka nchi hizo upo nchini kwa ajili ya kuimarisha mahusiano kati yao na Mashrika ya Umoja wa Mataifa yanayofanyakazi kama taasisi moja na nchi hizo (Delivering as one) kwa lengo la kuimarisha na kusukuma mbele malengo ya maendeleo endelevu (SDGs).
Katika ziara hiyo iliyoanzia Novemba 14 wajumbe hao waliweza kuangalia utekelezaji mbalimbali wa miradi ya Umoja wa Mataifa na hasa hatua za mwanzo za miradi ya UNDAP ll.
Ujumbe huo wenye watu 13 kutoka Wizara za Mambo ya Nje za mataifa hayo wanatarajia kuzuru pia Kigoma na Dodoma wakimaliza Dar es Salaam.
Wakiwa Dar es Salaam, jana na leo watakutana na wawakilishi wa taasisi mbalimbali zisizo za kiserikali na AZAKI na pia wanatarajia kutembelea ofisi za Bunge.Taarifa iliyotolewa katika mkutano huo imesema ingawa msaada wa Umoja wa Mataifa umekuwa siku zote ukililenga eneo maalumu linaloshughulikiwa na mashirika tofauti ya Umoja wa Mataifa, imekuwa nguvu kupima athari zake katika maeneo mbalimbali yaliyokusudiwa.
Hata hivyo imeelezwa kuwa kupitia programu mbalimbali na miradi katika demokrasia na uwajibikaji kuwezesha utawala bora, kumefanya kuwepo na nafuu fulani.
Serikali ya Tanzania ilielezea matumaini yake kwamba UNDAP ll, Mashirika ya Umoja wa Mataifa yakifanya kazi kama taasisi moja yatasaidia wizara katika kufanikisha kwa namna sahihi mfumo wa haki kwa wananchi.
Programu hizo ni pamoja na UNDAP 1 iliyosaidia wizara kutengeneza na kutekeleza mpango wa haki za binadamu (MHRAP 2013-2017). Mpango huo ulibainisha maeneo mbalimbali yaliyotakiwa kufanyiwa kazi na wadau mbalimbali.
UNDAP I ilisaidia wizara kupitia Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa serikali kujenga uwezo kwa wafanyakazi wake katika masuala ya majadiliano katika mikataba na namna ya kuiandika hasa katika sekta ya uziduaji.
Wanasheria kadha wa serikali na majaji walinufaika na elimu hiyo.
Aidha chini ya UNDAP I, Umoja wa Mataifa ulitoa msaada wa kiufundi kwa wizara kwa lengo la kuwezesha kufanya utafiti kuhusu hali ya mfumo wa haki wa mtoto nchini Tanzania na kuweza mkakati endelevu wa haki za mtoto kuanzia wmaka 2013-2017.
Wizara pia inasaidiwa kufuatilia mkakati huo kupitia majukwaa ya haki za watoto yanayofanyika kila mwaka.
Wizara ya Mambo ya Katiba na Sheria kwa mujibu wa sera ndiyo iliyokabidhiwa majukumu ya kutengeneza kanuni na viwango, kuratibu na kufuatilia utii usio na shuruti katika mfumo wa sheria na hivyo kupata matokeo yaliyokusudiwa ya sheria husika.
Wizara hii inajishughulisha na masuala ya Katiba, utawala na utoaji wa haki; uandishi wa sheria; uendeshaji wa mashtaka; Mikataba na sheria za kimataifa: msaada wa kisheria na haki za binadamu;usajili uboreshaji wa sheria, kabidhi wasihi, udhamini na mufilisi na kadhalika
Mamlaka ya Wizara katika mambo mengi ni mtambuka na hivyo kuifanya kuwa na ugumu fulani katika utendaji wake.
Aidha akifafanua zaidi amesema kutokana na misaada ya mashirika ya Umoja wa Mataifa, Watanzania wameweza kuwa na mfumo bora zaidi wa haki kwa watoto wanaoingia matatani na sheria.
Aidha watoto zaidi ya 1,500 wamepatiwa msaada wa kisheria katika mji wa Mbeya na Dar es Salaam na yote hayo yamewezeshwa na UNDAP l.
Wizara pia iliangalia matatizo ya ukatili wa kijinsia na watoto katika Dar es Salaam, Dodoma na Kilimanjaro na matokeo yake kusambazwa kwa wadau mbalimbali kwa kuyafanyia kazi.
Aidha kwa kusaidiwa na Umoja wa Mataifa ambayo iliratibu mkutano wa kwanza wa wadau kuzungumzia sheria ya ndoa ya mwaka 1971 katika hali ya kuongeza haki zaidi ka wanawake na watoto.
Pia alisema katika UNDAPll mashirika hayo ya Umoja wa Mataifa yanasaidia pia kuangalia mfumo wa haki wa sasa hasa kwa makundi yenye uhitaji yaliyosahaulika na kukuza ulinzi na usalama kwa mama na mtoto.
Ujumbe huo pamoja na kuwa mzito pia utafanya safari ya kuangalia miradi ya Bunge iliyopewa chapuo na fedha za Umoja wa Mataifa pia watatembelea eneo la dawati la Jinsia Chang’ombe na kutembelea taasisi ya PASADA.
Maeneo mengine ni ghala la Chakula Kizota, miradi ya TASAF na pia kiwanda cha kusindika mafuta kilichopo Dodoma.
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni