JAMHURI
YA MUUNGANO WA TANZANIA
KURUGENZI
YA MAWASILIANO YA RAIS IKULU
Simu:
255-22-2114512, 2116898
E-mail:
press@ikulu.go.tz
Tovuti :
www.ikulu.go.tz
Faksi: 255-22-2113425 |
|
OFISI YA RAIS,
IKULU,
1 BARABARA YA BARACK OBAMA,
11400 DAR ES SALAAM.
Tanzania.
|
TAARIFA
KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli
amemuagiza Waziri na Katibu Mkuu katika Ofisi ya Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kusitisha mara moja utekelezaji wa zoezi
la kuwaondoa wafanyabiashara wadogo maarufu kwa jina la Machinga
katika Jiji la Mwanza mpaka hapo mamlaka husika itakapokamilisha
maandalizi ya maeneo watakapohamishiwa na kwa kuwashirikisha
wamachinga wenyewe.
Rais
Magufuli akiwa na Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan ametoa
agizo hilo leo tarehe 06 Desemba, 2016 Ikulu Jijini Dar es Salaam
huku akionya kuwa kiongozi yeyote ambaye hayupo tayari kutekeleza
agizo hilo aachie ngazi.
"Kumeibuka
tabia ya Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi kuwafukuza
Wamachinga bila utaratibu wowote wa wapi wanawapeleka na wakati
mwingine wanapelekwa maeneo ya mbali ambayo hayafai hata kwa kufanya
biashara, hili jambo sio sawa hata kidogo.
"Sipendi
Wamachinga wafanye biashara kwenye hifadhi ya barabara lakini hakuna
sheria katika nchi hii inayosema mtu wa biashara ndogondogo au
Mmachinga hatakiwi kukaa katikati ya mji, tukianza kwenda kwenye
utaratibu wa namna hiyo maana yake tunaanza kutengeneza madaraja ya
Watanzania, kwamba kuna Watanzania fulani wa daraja fulani wanapaswa
kukaa katikati ya mji na Watanzania wa daraja fulani hawatakiwi kukaa
katikati ya mji, huo sio mwelekeo wetu na wala Ilani ya Uchaguzi ya
Chama Cha Mapinduzi ambayo mimi na wewe (Makamu wa Rais) tulipita
kuinadi, haisemi tutengeneze madaraja ya watu wanaostahili kukaa
mjini na wengine hawastahili kukaa mjini, sasa nimeona hili
nilizungumze na nataka kulirudia kwa mara ya mwisho"
amesema Rais Magufuli.
Dkt.
Magufuli ameelekeza kuwa Wamachinga waliondolewa katika maeneo yao
Jijini Mwanza waachwe waendelee na shughuli zao mpaka hapo
Halmashauri ya Jiji la Mwanza itakapokamilisha maandalizi ya mahali
watakapohamishiwa na kwa kuwashirikisha Wamachinga wenyewe.
"Narudia
na hii ni mara ya mwisho, kawaambieni hata Wamachinga wa Mwanza
warudi kwenye maeneo yao mpaka watakapowatengenezea utaratibu mzuri,
Kigamboni hapa palikuwa na wamachinga eneo fulani wamehama vizuri
kweli, wakatengenezewa miundo mbinu yao katika soko lao na sasa hivi
wanafanya kazi vizuri, na waliwashirikisha viongozi wa Wamachinga,
lakini Mwanza imekuwa ni amri tu na wengine wanatumia hata msemo wa
Hapa Kazi Tu, mimi sikusema msemo wa Hapa Kazi Tu wa namna hiyo,
nadhani mmenielewa"
amesisitiza Rais Magufuli alipokuwa akiwaekeleza Naibu Waziri wa
TAMISEMI Mhe. Suleiman Jafo na Katibu Mkuu TAMISEMI Mhandisi Mussa
Iyombe.
Wakati
huo huo,
Rais Magufuli ameagiza Wizara ya Nishati na Madini kusitisha mara
moja zoezi la kuwaondoa wachimbaji wadogo katika Kijiji cha
Nyaligongo kilichopo katika Kata ya Mwakitolyo Mkoani Shinyanga na
badala yake wachimbaji hao waachwe waendelee na shughuli zao, na
leseni ya mwekezaji anayedai eneo hilo ni lake aondolewe.
"Wale
waliofukuzwa Shinyanga wabaki palepale, kama ni leseni ya huyo
mwekezaji ifutwe, Mhe. Makamu wa Rais fuatilia hili, mweleze Waziri
wa Nishati na Madini, waache kufukuza wananchi hovyohovyo, wale
wanapata riziki yao, wanasomesha watoto wao lakini wanafukuzwa tu.
"Na
hizi ndio ajira zenyewe, tulisema tunatengeneza ajira, wewe mwekezaji
ni mmoja unakwenda kuwafukuza watu 5,000? haiwezekani na wala haingii
akilini"
amesisitiza Rais Magufuli.
Rais
Magufuli amekemea vitendo vya wawekezaji wakubwa kupewa maeneo ambayo
wachimbaji wadogo wanaendesha shughuli zao tena kwa mtindo kwa
kutengeneza nyaraka zinaonesha mwekezaji husika alipewa eneo hilo
kabla ya wachimbaji wadogo na kusisitiza kuwa mchezo huo
hautavumiliwa.
Hata
hivyo Rais Magufuli amesema maagizo yake hayana maana kuwa Wamachinga
na Wachimbaji wadogo waendeshe shughuli zao kwa kuvunja sheria bali
wazingatie sheria na Mamlaka zisiwanyanyase watu wanyonge
Gerson
Msigwa
Mkurugenzi
wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar
es Salaam
06
Desemba, 2016
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni