Na Asteria Muhozya, Muleba
Imeelezwa kuwa, Serikali imepanga kutumia Nguzo za Zege katika utekelezaji wa Mradi wa Usambazaji Umeme Vijijini Awamu ya Tatu, unaotarajia kuanza kutekelezwa kuanzia mwezi Januari, 2017 chini ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa kushirikiana na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO).
Hayo yamebainishwa kwa nyakati tofauti na Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Medard Kalemani wakati wa ziara yake ya kukagua utekelezaji wa mradi wa REA Awamu ya Pili katika Kata za Ngenge na Ngwanseri, Wilayani Muleba Mkoani Kagera, pamoja na kueleza mipango ya Serikali katika utekelezaji wa mradi husika Awamu ya Tatu.
Dkt. Kalemani amesema kuwa, lengo la kutumia nguzo hizo za zege ni kutokana na uimara wake utakaowezesha upatikanaji umeme wa uhakika na kuepuka kuchomwa na kuongeza kuwa, tayari nguzo hizo zimeanza kutumika katika Mkoa wa Kilimanjaro.
Akizungumzia utekelezaji wa REA Awamu ya Pili, amesema Serikali imetekeleza mradi huo kwa kasi kubwa kutokana na dhamira yake ya kuhakikisha kuwa, ifikapo mwaka 2025 asilimia 75 ya Watanzania wawe wameunganishwa na nishati hiyo ambayo ni kichocheo cha shughuli za kiuchumi.
“ REA awamu ya pili imekamilika kwa kiwango kikubwa. Vipo baadhi ya vijiji havijafikiwa kutokana na dosari ndogo ndogo lakini tutavikamilisha kuwezesha utekelezaji wa Awamu ya Tatu. Hata katika Wilaya hii vipo na tayari nimemwelekeza Mkandarasi kukamilisha kazi hiyo haraka,”amesisitiza Dkt. Kalemani.
Akielezea mipango kwa Awamu ya Tatu, amesema kuwa, Serikali imelenga kuhakikisha kuwa, awamu hiyo inavifikia vijiji vyote ambavyo havikuunganishwa katika Awamu ya Pili, visiwa vyote, Taasisi mbalimbali, Sehemu zinazotoa Huduma za Kijamii zikiwemo za Afya, shule na visima vya maji.
Aidha, alisema kuwa, kukamilika kwa utekelezaji wa Miradi Ujenzi wa njia za Kusafirisha umeme wa Msongo Mkubwa wa kV 400 kutoka Iringa hadi Shinyanga kupitia Dodoma na Singida kutawezesha upatikanaji wa umeme wa uhakika pamoja na kuchochea uchumi wa viwanda hususan katika mikoa ya Kanda ya Ziwa.
Wakati huo huo, Dkt. Kalemani ametumia fursa hiyo kuzitaka Halmashauri zote nchini kushirikiana na TANESCO kuweka utaratibu shirikishi ambao utawawezesha wananchi kupata huduma za kuunganishiwa nishati hiyo kupitia utaratibu wa kuanzisha madawati ya TANESCO katika maeneo yatakayotambuliwa ili kuwawezesha wananchi kupata huduma hiyo kwa urahisi.
“TANESCO na Halmashauri, pangeni namna ya kuwawezesha wananchi kufikiwa kwa urahisi na huduma za kunganishwa nishati ya umeme. Mkubaliane kupanga siku maalum ambayo wananchi watahudumiwa. Serikali inataka kila mwananchi apate umeme, hivyo tuweke utaratibu ambao utarahisisha na kuwezesha azma hiyo kufikiwa kwa haraka,” amesisitiza Dkt. Kalemani.
Pia, Dkt. Kalemani amewataka Wakandarasi wote wakati wa utekelezaji wa miradi ya Awamu ya Tatu kuhakikisha kuwa, wanajitambulisha katika Halmashauri na Mamlaka nyingine ili waweze kutambulika ili kuepusha udanganyifu.
Vilevile, Dkt. Kalemani ameitaka TANESCO kuwaidhinisha Wakandarasi wote watakaofanya kazi ya ‘wiring’ katika nyumba za wananchi katika utekelezaji wa REA Awamu ya Tatu ikiwemo kutoa orodha zao ili kuwapunguzia wananchi kero ikiwemo kuwaepusha na utapeli unaofanywa na baadhi ya wasiowaaminifu.
Akizungumzia Sekta ya Madini, Dkt. Kalemani amewahamasisha wachimbaji wadogo wadogo kujiunga katika vikundi ikiwemo kujisajiri katika Ofisi za Madini zilizopo katika maeneo mbalimbali nchini kwa lengo la kuwawezesha wachimbaji hao kuomba ruzuku kupitia vikundi pindi zinapotolewa na Serikali.
Katika ziara ya kutembelea Kata hizo, Dkt. Kalemani ameambatana na Mkuu wa Wilaya ya Muleba, Mhandisi Richard Ruyango, Wataalam kutoka Wizara ya Nishati na Madini, REA, TANESCO na Wakandarasi wanaotekeleza mradi wa REA Awamu ya Pili Wilayani humo
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni