.

.

.

.

.

.

.

.
KARIBUNI TUHABARIKE, TUELIMISHANE, TUPEANE HABARI ZA KUKUFANYA UTABASAMU KIDOGO NA MATUKIO YALIYOFANYIWA UCHUNGUZI WA KINA TOKA KILA PEMBE CONTACTS: +255 787 377 722 Email: drweyunga@gmail.com PIA UNAWEZA KUNI FOLLOW KUPITIA INSTAGRAM YANGU @drweyunga | TANGAZA NASI ILI UWAFIKIE WATU WENGI ZAIDI.

Jumatatu, 19 Desemba 2016

SERIKALI YA MAPINDUZI YA ZANZIBAR YATILIANA SAINI MKATABA WA USHIRIKIANO NA KAMPUNI YA ZTE

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kushoto na Rais wa Kampuni ya ZTE ya Mji wa Shengzhen Nchini China Bwana Zhang Rejun kulia wakitia saini Mkataba wa ushirikiano katika uendelezaji wa miradi itakayotumia mfumo wa Teknolojia ya Kisasa ya Mawasiliano hao Makao Makuu wa ZTE Mjini Shengzhen China.
Rais wa Kampuni ya ZTE ya Mji wa Shengzhen Nchini China Bwana Zhang Rejun akitia saini Mkataba huo kwa niaba ya Kampuni yake huku akishuhudiwa pia na Naibu Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji Zanzibar Mh. Mohamed Ahmed Salum na kushoto yake Mwakilishi wa Kampuni hiyo Tanzania Bwana Wayne Zhu.
Balozi Seif akitia saini hiyo akishuhudiwa nyuma yake na Waziri wa Fedha na Mipango Zanzibar Dr. Khalid Salum Moh’d wa kwanza kutoka Kulia na Katibu Mkuu Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi wa Umma na Utawala Bora Bibi Asha Ali Abdulla wa Pili kutoka Kushoto.
Balozi Seif kushoto akibadilishana hati na Rais wa ZTE Bwana Zhang Rejun baada ya kutia saini Mkataba wa Ushirikiano wa uendelezaji wa miradi itakayotumia mfumo wa Teknolojia ya Kisasa ya Mawasiliano.

Mtaalamu wa Ufundi wa Kampuni ya ZTE Bibi Radhika Devi wa kwanza kutoka Kushoto akimkaguza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif na Ujumbe wake katika vitengo mbali mbali ndani ya Makao Makuu ya Kampuni hiyo Mjini Shengzheng.

Kushoto ya Balozi Seif ni Naibu Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji Zanzibar Mh. Mohamed Ahmed Salum na Katibu Mkuu Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi wa Umma na Utawala Bora Bibi Asha Ali Abdulla

Picha na - OMPR –ZNZ.
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Kampuni ya Kimataifa ya Mitandao ya Kisasa ya Mawasiliano ya ZTE ya Mji wa Shengzhen Nchini Jamuhuri ya Watu wa China zimetiliana saini Mkataba wa ushirikiano katika uendelezaji wa miradi itakayotumia mfumo unaokubalika Kimataifa kwa hivi sasa.
Miradi hiyo itakayotumia mfumo waTeknolojia ya Kisasa { TEHAMA } ni pamoja na Mradi wa Mawasiliano Serikalini { E Goverment } huduma za umeme, usafiri, miji mipya, afya pamoja na huduma za Kijamii ikiwemo utaratibu wa udhibiti wa ukusanyaji wa Mapato ya Serikalini.
Saini ya Mkataba huo imetiwa na Rais wa Kampuni ya ZTE Bwana Zhang Rejun wakati upande wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imetiwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ambaye yuko Nchini China kwa ziara rasmi ya Kiserikali ya siku Tano.
Akizungumza na Uongozi wa Kampuni hiyo ya ZTE kwenye Makao Makuu yake Mjini Shengzhen Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Zanzibar inaendelea kuipa fursa zaidi Kampuni ya ZTE katika mtazamo wake wa miradi ya maendeleo inayotarajia kuanzisha hapo baadaye.
Balozi Seif alisema hatua hiyo ya Serikali imekuja kutokana na Uongozi wa juu wa Kampuni ya ZTE kuonyesha juhudi kubwa za kuendelea kuunga mkono harakati za kuimarisha miradi ya Maendeleo zinazotekelezwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliishukuru na kuipongeza Kampuni ya ZTE kwa kasi kubwa ya uwajibikaji wa watendaji wake katika mfumo wa Teknolojia ya kisasa ya mawasiliano unaoonekana kukubalika na Mataifa mengi Duniani zikiwemo pia Nchi za Bara la Afrika.
 
Balozi Seif aliutolea mfano mradi Mkubwa wa mawasiliano Serikalini {E Goverment } ambao ulisimamiwa na Kampuni hiyo kwa upande wa Zanzibar ukikamilika katika awamu ya kwanza.
 
Naye Waziri wa Fedha na Mipango wa Zanzibar Dr. Khalid Salum Moh’d alisema kazi kubwa inayofanywa na Uongozi wa Kampuni ya ZTE katika kusaidia miundombinu ya mawasiliano Zanzibar imeleta faraja kwa Wananchi walio wengi Visiwani Zanzibar.
 
Dr. Khalid alisema wakati Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ikijitahidi kuendelea kudhibiti mapato yake kwa kutumia mfumo wa Kisasa wa Mawasiliano Kampuni ya ZTE bado ina nafasi ya kusaidia Taaluma katika kazi hiyo kwa lengo la kupata ufanisi mkubwa zaidi.
 
Mapema Rais wa Kampuni ya Kimataifa ya Mitandao ya Kisasa ya Mawasiliano ya ZTE ya Mji wa Shengzheng Nchini China Bwana Zhang Rejun aliueleza Ujumbe wa Zanzibar unaoongozwa na Balozi Seif kwamba Kampuni yake hivi sasa tayari imeshatekeleza miradi ipatayo Mitano Visiwani Zanzibar.
 
Bwana Zhang alisema uwamuzi wa Uongozi wa Kampuni yake kuongeza Miradi Zanzibar umekuja kutokana na mazingira bora ya uwekezaji pamoja na rasilmali za asili za maumbile zilizotoa kigezo kikubwa kwa Kampuni hiyo.
 
Kampuni ya Kimataifa ya Mitandao ya Kisasa ya Mawasiliano ya ZTE ya Mji wa Shengzheng Nchini iliyoasisiwa mwaka 1985 tayari imeshawekeza miradi yake katika Mataifa 60 ulimwenguni na kupata tuzo tofauti katika ubora wa utoaji huduma zake katika kiwango kinachokubalika Kimataifa.


Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

Hakuna maoni :

Chapisha Maoni