



Wa kwanza kutoka kushoto ni Mkurugenzi wa Idara ya Uratibu wa shughuli za SMZ na SMT Nd. Khalid Bakari Amrani, Mkurugenzi Mtendaji wa Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa Nd. Ali Juma Hamad na Mkurugenzi wa Idara ya Sherehe na maadhimisho ya Kitaifa Bibi Riziki Daniel Yussuf.





Jamii imeaswa kuendelea kushirikiana katika harakati zao za kila siku za kimaisha na Kifamilia ili kukifanya kizazi chao kukua katika maadili na utamaduni unaokubalika kidini na kidunia jambo ambalo litatoa faraja kwa wazazi, walezi pamoja na Viongozi wa Kitaifa.
Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Mihayo Juma Nhunga wakati wa hafla maalum ya kuuaga mwaka 2016 na kuukaribisha mwaka Mpya wa 2017.
Mh. Mihayo alisema hayo kwa niaba ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliyeandaa hafla hiyo Nyumbani kwake Mtaa wa Kama nje kidogo ya Kaskazini Magharibi ya Mji wa Zanzibar akiwashukuru baadhi ya Viongozi na Wafanyakazi wa Ofisi hiyo pamoja na Familia zao walioshiriki katika kuukaribisha mwaka mpya.
Katika kuuaga mwaka 2016 uliobeba matukio mbali mbali yakiwemo mengi ya udhalilishaji wa Kijinsia ya yale yaliyopoteza maisha ya Wananchi wengi kutokana na ajali za bara barani, Naibu Waziri Mihayo alisema suala la kupendana miongoni mwa Jamii ndani ya mwaka mpya wa 2017 linafaa kufanywa kuwa jambo la msingi.
Kupitia hafla hiyo ya chakula cha usiku Mhe. Mihayo Juma Nhunga kwa Niaba ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwatakia kheir ya mwaka Mpya Wananchi wote wa Zanzibar na kuwataka wale waliokoseana ndani ya mwaka uliopita wasameheane.
Alisema Mwaka mpya unahitaji zaidi mambo mapya na ya msingi ili kulifanya Taifa na wananchi wake waelekee kwenye maendeleo yatakayoleta faida na kustawisha maisha yao ya kila siku.
Hafla hiyo ya chakula cha usiku uliyowakutanisha baadhi ya Viongozi na watendaji wa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar na Familia zao iliambatana na muziki laini uliotoa burdani safi kwa washiriki hao walioshindwa kukaa kwenye viti vyao na kuonekana wakianza kuserebuka.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
1/1/2017.
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni