Alisema licha ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuajiri walimu wengi wa masomo ya Sayansi katika azma yake ya kukabiliana na tatizo hilo lakini bado upungufu huo unaendelea kuziathiri skuli nyingi Unguja na Pemba.
Balozi Seif Ali Iddi alitoa angalizo hilo baada ya kuzindua rasmi jengo jipya la madarasa Mawili ya Skuli ya Maandalizi ya Kiombamvua lililojengwa na Uongozi wa Hoteli ya Sea Cliff kutekeleza ahadi uliyotoa wa kusaidia huduma za Kijamii na maendeleo ya Wananchi wa Vijiji vinavyoizunguuka Hoteli hiyo.
Alisema baadhi ya wakati Serikali hulazimika kuagiza walimu wa fani ya sayansi kutoka nje ya Nchi jambo ambalo husababisha kutumia gharama kubwa ya fedha ambayo inaweza kupunguzwa iwapo wanafunzi wenyewe wataamua kupenda masomo ya sayansi.
Balozi Seif ambae pia ni mwakilishi wa Jimbo la Mahonda aliwahimiza wanafunzi wote wa Jimbo hilo kuongeza juhudi za masomo wakati Uongozi wao unajitahidi kujenga mazingira mazuri yatakayowaondolea changamoto zinazowakabili katika masomo yao.
Alisema Uongozi wa jimbo la Mahonda una malengo katika kuona wanafunzi wote wa skuli zilizomo ndani ya jimbo hilo wanaendelea kupata elimu yao hadi upeo wa uwezo wao kimasomo.
Balozi Seif alifahamisha kwamba juhudi kubwa zimeanza kuchukuliwa na Uongozi huo katika kuzijengea miundombinu pamoja na vifaa vya Maabara na Maktaba baadhi ya skuli za sekondari za Jimbo hilo ili kuwa na uwezo na maarifa wanafunzi hao ya kufanya vizuri kwenye mitihani yao ya Taifa.
Alikemea tabia ya baadhi ya wanafunzi kupenda kuzurura ovyo wakati wa masomo maskulini na kuagiza kutaka kuachwa mara moja kitendo hicho kisicholeta tija katika hatma yao ya baadae.
Balozi Seif aliushukuru Uongozi wa Hoteli ya Sea Cliff kwa uungwana wake wa kutekeleza ahadi uliyotoa wakati wa vikao vyake na Uongozi wa Kamati ya Bandari ya Kiombamvua katika njia ya kuleta maridhiano ya pande hizo mbili.
Balozi Seif alisema hali haikuwa shwari kati ya Wananchi wa Vijiji vinavyoizunguuka Hoteli ya Sea Cliff na Uongozi wa Hoteli hiyo iliyotaka kulitumia eneo la pembezoni mwa Bahari ya Kiombamvua kwa ajili ya kujenga uwanja wa mchezo wa Golf licha ya kufuatwa kwa taratibu zilizohusika.
Alisema mzozo huo ulikuwa ulichochewa na baadhi ya wanasiasa na kupelekea Kamati ya Bazara la Wawakilishi Zanzibar kuingilia kati na hatimae kuagizwa kufuatwa kwa muongozo uliokubalika na pande hizo mbili.
Mapema akikabidhi funguo za Jengo la Skuli hiyo ya Kiombamvua kwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ambaye na yeye kumkabidhi Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mh. Riziki Pembe Juma, Mwakilishi wa Hoteli ya Sea Cliff Nd. Yasser De Costa alisema Uongozi huo utaendelea kusaidia kuduma za Kijamii kadri hali itakavyoruhusu.
Nd. De Costa aliwashukuru Wananchi wa Vijiji vinavyoizunguuka Hoteli hiyo kwa ushirikiano wao wa kina uliopelekea kuchanyua kwa maendeleo yanaoanza kuonekana ndani ya Vijiji hivyo likiwemo suala zito la kuimarika kwa huduma za Elimu.
Mwakilishi huyo wa Sea Cliff aliwasihi wanafunzi wa Vijiji hivyo kuacha mzaha na badala yake akili na maarifa yao wakayaelekeze katika kusaka Elimu itakayowajengea nuru njema katika mustakaba wa maisha yao ya baadaye.
Akitoa salamu za Uongozi wa Hoteli ya Sea Cliff katika hafla hiyo, Meneja Mkuu wa Hoteli hiyo Bwana Jean Claude alieleza kwamba matunda ya jengo hilo Jipya la Skuli ya Maandalizi ya Kiombamvua lazima yaonekane.
Bwana Claude alisema elimu ndio kila kitu ikiwa ni msingi imara wa maendeleo wakati na mahali popote pale Duniani.
Akipokea funguo za Jengo hilo jipya la Skuli ya maandalizi ya Kiombamvua Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mh. Riziri Pembe Juma aliwahakikishia Wananchi wa Kiombamvua kwamba kazi iliyobaki ya kumalizia uwekaji wa vikalio na huduma za Walimu ndani ya jengo hilo ni ni jukumu la Wizara hiyo.
Akiushukuru Uongozi wa Hoteli ya Sea Cliff kwa misaada yake ya kuunga mkono sekta ya Elimu Zanzibar Mh. Riziki alisema jitihada zitafanywa mara moja katika kuona majengo hayo yanaanza kazi mara moja ili kuwaondoshea usumbufu watoto wa maeneo hayo.
Alishauri ipo haja ya kuchukuliwa kwa hatua za mapema kati ya Wananchi wa Kiombamvua na Wizara ya Elimu katika kufikiria wazo la kuanza ujenzi wa majengo ya Skuli ya Msingi ili watoto wanaomaliza mafunzo yao ya maandalizi Skulini hapo waendelee kwa hatua ya elimu ya msingi.
Ujenzi wa Jengo jipya la Skuli ya Maandalizi ya Kiombamvua lenye madarasa Mawili, Vyoo, Ofisi ya Walimu pamoja na Tangi la kuhifadhia Maji lililojengwa na Hoteli ya Sea Cliff limegharimu jumla ya shilingi za Kitanzania Milioni 70,000,000/-.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
23/2/2017.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kulia akifarajika pamoja na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mh. Riziki Pembe Juma na Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini “B” Nd. Issa Juma mara baada ya kulizindua rasmi jengo jipya la Madarasa Mawili la Skuli ya Maandalizi ya Kiombamvua lililojengwa na Hoteli ya Sea Cliff.
Balozi Seif akimkabidhi Ufunguo wa Jengo la Skuli ya Maandalizi ya Kiombamvua Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mh. Riziki Pembe Juma katika hafla rasmi ya uzinduzi wa Skuli hiyo.
Baadhi ya wanafunzi wa Skuli ya Msingi ya Kiombamvua wakifuatilia sherehe za uzinduzi wa jengo jipya la skuli ya Maandalizi ya Kiombamvua uliofanywa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif. Baadhi ya Wazazi, Walezi, Walimu na Wananchi wa Kijiji cha Kiombamvua walioshiriki uzinduzi wa jengo jipya la skuli ya maandalizi ya Kiombamvua uliofanywa na Balozi Seif.
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni