.

.

.

.

.

.

.

.
KARIBUNI TUHABARIKE, TUELIMISHANE, TUPEANE HABARI ZA KUKUFANYA UTABASAMU KIDOGO NA MATUKIO YALIYOFANYIWA UCHUNGUZI WA KINA TOKA KILA PEMBE CONTACTS: +255 787 377 722 Email: drweyunga@gmail.com PIA UNAWEZA KUNI FOLLOW KUPITIA INSTAGRAM YANGU @drweyunga | TANGAZA NASI ILI UWAFIKIE WATU WENGI ZAIDI.

Jumatano, 22 Februari 2017

TUNZENI DARAJA LA BONGA - WAZIRI MKUU

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka wakazi wa mji wa Babati na kata za jirani walitunze daraja la Bonga kwa kulinda miundombinu iliyowekwa.

Ametoa wito huo leo asubuhi (Jumatano, Februari 22, 2017) wakati
akizungumza na wakazi wa kata ya Bonga waliofika kushuhudia uwekaji wa jiwe la msingi wa ujenzi wa daraja hilo, wilayani Babati, mkoani Manyara.

Waziri Mkuu amesema amekagua daraja hilo na kuridhishwa na viwango vya
ujenzi wake lakini akamtaka mkandarasi aendeleze viwango hivyo hadi daraja
likamilike ili daraja hilo liwe la kudumu. “Tukija kuzindua, iwe ni kitu
kimedumu kutokana na ubora wake,” amesema.

Amesema kukosekana kwa daraja hilo kulikuwa kunawatenga wakazi wa kata
mbili za vijijini na mjini ambao walikuwa wakishindwa kuwasiliana lakini
Serikali imesikia kilio cha wabunge wa mkoa huo na ndiyo maana inafanya
jitihada za kuboresha miundombinu ya barabara na madaraja ili kurahisisha
mawasiliano baina ya wananchi wake.

“Nitoe wito kwa wananchi kuwaomba mlitunze daraja hili. Daraja hili
limejengwa kwa nondo. Katika baadhi ya maeneo, kuna mtu yuko radhi kuchomoa nondo kipande cha mita tatu tu lakini aharibu daraja lililotumia mamilioni ya fedha kulijenga,” amesema.

“Pia wako wanaotafuta mabomba, wanakuja na misumeno, wanakata mabomba yaliyounganisha nguzo na kuzuia watembea kwa miguu wasianguke ili wakatumie wakati wangeweza kupata kipande hicho kwa sh. 5,000. Ninawasihi tulitunze daraja letu,” alisisitiza.

Naye Diwani wa kata ya Bonga, Bw. Hitii Qambalai alimshukuru Waziri Mkuu
kwa kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa daraja hilo kwani wananchi walikuwa
wanashindwa kusafirisha mazao yao lakini pia akatumia fursa hiyo kuiomba
Serikali ikamilishe kutuma fedha zilizobakia ili ujenzi wa daraja ukamilike
mapema.

Mapema akisoma taarifa ya ujenzi wa daraja hilo, Mkurugenzi wa Mji ya
Babati, Bw. Fortunatus Fuime alisema ujenzi wa daraja hilo utahusisha
ujenzi wa barabara yenye urefu wa km. 2.3 na vyote vitagharimu sh. milioni
550.4.

“Ujenzi huo ambao ulianza Agosti 10, 2016, unatarajiwa kukamilika Aprili
10, 2017. Kukamilika kwa ujenzi wa daraja hili kutasaidia kuiunganisha
Halmashauri ya Babati, mji wa Babati na wilaya ya Hanang.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMATANO, FEBRUARI 22, 2017.

Hakuna maoni :

Chapisha Maoni