Na Stella Kalinga-Simiyu
Wanariadha wawili wa Kimataifa kutoka katika jimbo la Hanover Nchini Ujerumani wanatarajia kushiriki mashindano ya riadha ya Kilimanjaro Marathon yatakayofanyika Februari 26 mwaka huu, Mkoani Kilimanjaro ikiwa ni moja kati ya ushirikiano baina ya Ujerumani na Tanzania.
Akifungua mafunzo ya siku moja ya makocha na walimu wa michezo mbalimbali kutoka mikoa minne ya kanda ya Ziwa ,Rais wa Shirikisho la Riadha Nchini ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka aliwataja wanariadha hao kuwa ni Christin Kulgemeyer na Stephan Immega ambao watakuwa chachu ya kuwatia moyo wanariadha wengine wa Kitanzania.
Mtaka alibainisha kuwa licha ya kushiriki mashindano hayo,wanariadha hao watapata fursa ya kuona Mlima Kilimanjaro ikiwa ni moja kati ya kuitangaza Tanzania na vivutio vyake.
Aidha katika ufunguzi huo Mtaka aliwataka makocha na viongozi wa michezo mbalimbali kutoka mikoa ya Simiyu,Mwanza,Mara na Shinyanga kuyatumia mafunzo hayo vizuri ili kujenga mtazamo chanya wa kimichezo katika mikoa ya kanda ya Ziwa.
Aliongeza kuwa viongozi hao wanapaswa kutambua kuwa riadha inakuwa ni moja kati ya njia ya kuitangaza nchi kwa Mataifa nyingine ikiwa ni pamoja na kujenga ushirikiano baina ya Mkoa wa Simiyu na jimbo la Hanover Nchini Ujerumani.
“Kupitia wanariadha hawa imekuwa faraja kuona Tanzania riadha inakuwa ni sehemu ya kuitangaza nchi yetu, kwa sababu hawa wanariadha wametoka Ujerumani kuja kushiriki mashindano ya Kilimanjaro Marathoni mwaka huu 2017, ikiwa ni pamoja na kuwa sehemu ya ushirikiano kati ya Mkoa wa Simiyu na Jimbo la Hanover Ujerumani” alisema.
Hata hivyo wanariadha hao wameonyesha kufurahishwa na kuanzishwa kwa ushirikiano wa kimichezo baina ya nchi yao na Mkoa wa Simiyu kwani wanaamini watajifunza mengi kutokana na kubadilishana uzoefu na kuifanya micheczo kuwa na nafasi kubwa Duniani.
Mafunzo ya makocha na walimu wa michezo wa mikoa ya Simiyu, Mwanza,Mara na Shinyanga yanaendeshwa na wataalam wa michezo kutoka Jimbo la Hanover nchini Ujerumani.
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni
(
Atom
)
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni