Wafanyabiashara wa Tanzania wamesema wapo tayari kwa kufanya ushirikiano wa kibiashara wa ubia na wafanyabiashara kutoka nje ili kukuza diplomasia ya kiuchumi na mataifa mengine.
Akizungumza katika hafla ya chakula cha mchana na mabalozi wa Tanzania nje ya nchi kilichoandaliwa na Taasisi ya sekta binafsi (TPSF) nchini, Mwenyekiti wa Taasisi hiyo, Dkt. Reginald Mengi amesema wafanyabiashara watanzania si omba omba na wapo tayari kwa kufanya biashara ya ubia na wenzao.
“Napenda kusisitiza kwamba sisi watanzania si omba omba kwa wafanyabishara wa nje, tuna nia, uwezo, ujuzi na tunajiamini kwa kufanya biashara za kimataifa kwa ubia ili kukuza uchumi wa nchini zetu,” amesema Dkt. Mengi.
Amesema kwamba fursa za uwekezaji zipo nchini kwenye sekta za kilimo, mafuta, gesi, usindikaji na mawasiliano ila ni muhimu kuunganisha nguvu za wafanyabiashara ili kuweza kupata matokeo chanya.
Dkt. Mengi alilisisitiza kwamba sekta binafsi nchini ina imani kubwa na Rais Dkt John Pombe Magufuli katika adhma yake ya kukuza sekta ya viwanda ili kutatua tatizo la ajira na kuongeza mapato ya nchini.
“Ni muhimu kuimarisha sekta binafsi ili iweze kutoa mchango mkubwa katika uanzishwaji wa viwanda hapa nchini, kwa vyovyote vile sekta hii binafsi ndio itakayojenga viwanda hapa Tanzania,” aliongeza.
Kwa Upande wa Mabalozi, Dkt. Emmanuel Nchimbi ambaye anakwenda kuiwakilisha nchi huko Brazil, amesema kwamba mabalozi ni kiungo muhimu kati ya wananchi wa mataifa husika katika kukuza mahusiano na ushirikiano wa kimataifa.
“Sisi ni wawakilishi wenu huko kwenye mataifa ya nje na zaidi na kukuza mahusiano au diplomasia ya kiuchumi kwa maslahi ya wananchi wetu,” amesema Dkt. Nchimbi.
Naye Balozi wa Tanzania, Geneva, Dkt. James Msekela amesema kwamba ni muhimu kuanzisha mawasiliano ya mara kwa mara kati ya wafanyabishara na mabalozi ili kusaidia upatikanaji wa taarifa za fursa mbalimbali za uwekezaji au masoko kutoka kwenye bidhaa za nyumbani.
“fursa zipo kwenye kila sekta ni muhimu wafanyabishara wa ndani wakajenga uaminifu na kujiamini ili kuweza kuingia katika ushindani wa kibiashara katika soko la kimataifa,” amesema Dkt. Msekela.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Sekta Binafsi, Geofrey Simbeye amesema wataanzisha mawasiliano ya kudumu na mabalozi wa Tanzania nje ya nchi ili kuweza kubadilishana mawazo na taarifa juu ya fursa za kibiashara katika nchi wanazokwenda kuwakilisha.
Alifafanua kwamba serikali imefungua milango kwa sekta binafsi kufanya kazi kwa bidii ili kuweza kukuza uchumi wa Tanzania na kuondoa tatizo la umaskini.
Kikao hicho kati ya sekta binafsi na mabalozi wa Tanzania wanaokwenda kuwakilisha nchi katika mataifa matano ambapo mabalozi hao ni Dkt Emmanuel Nchimbi-Brazil, Dkt. James Msekela-Geneva, Profesa Elizabeth Kinyondo-Uturuki, Mbelwa Kairuki-China na Balozi George Madafa- Italy
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni