
Mwakilishi wa Jimbo la Mahonda Balozi Seif Ali Iddi kulia akisisitiza umuhimu wa kukamilishwa Jengo Jipya la Skuli ya Msingi ya Matetema Wilaya ya Kaskazini “B” ili kuondoa msongamano wa wanafunzi kwenye Skuli hiyo. Kulia ya Balozi Seif ni Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mh. Riziki Pembe Juma na Msaidizi Mwalimu Mkuu wa Skuli ya Msingi ya Matetema Mwalimu Ali.




Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Mh. Riziki Pembe Juma akitoa msimamo wa Wizara wa hatua zitakazochukuwa katika kukabiliana na matatizo yanayoikumba Skuli ya Msingi Matetema. Picha na – OMPR – ZNZ.
Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar imeombwa kuchukuwa hatua za dharura katika kulitafutia ufumbuzi wa haraka tatizo la ukosefu wa utulivu wa Masomo kwa Wanafunzi wa Skuli ya Msingi ya Matetema iliyomo ndani ya Jimbo la Mahonda Wilaya ya Kaskazini “B” ambao unaweza kuathiri hatma yao ya kupata haki yao ya Kielimu.
Kauli hiyo imetolewa na Wazee, Wazazi na Viongozi wa Kijiji cha Matetema mbele ya Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mh. Riziki Pemba Juma katika Kikao cha dharura kilichoitishwa na Mwakilishi wa Jimbo la Mahonda Balozi Seif Ali Iddi kujadili kadhia hiyo ya muda mrefu kijijini hapo.
Wazee na Wazazi hao wakizungumza kwa uchungu na hasira mbele ya Viongozi hao walisema mazingira ya kielimu ya Wanafunzi wa Skuli ya Msingi hivi sasa yanatisha na kusikitisha hasa wanapoonekana wanafunzi wake wakizurura muda mrefu wakati wa vipindi vya masomo.
Mjumbe wa Kamati ya Skuli ya Matetema Nd. Iddi Himid Iddi akionyesha hasira zisizomithilika kutokana na kadhia hiyo alisema uwamuzi wa Wananchi wa Kijiji cha Matetema kujenga skuli hiyo ulikuwa na lengo la kuwaondoshea usumbufu Watoto wao kufuata Elimu masafa ya marefu katika Kijiji cha Kitope.
Ndugu Himid alisema ushirikiano uliopo baina ya Wazee, Wazazi na Uongozi wa Skuli hiyo umefifia kiasi kwamba husababisha kuzaliwa kwa vitendo vya ajabu vinavyowapa muda mrefu Wanafunzi wa Skuli hiyo kuzurura Mitaani wakati wa masomo.
Alisema mazingira ya Skuli hiyo kwa wakati huu yanatoa fursa kwa Wanafunzi wake kukosa vipindi vya masomo, upotevu wa maadili, heshima na nidhamu mambo ambayo yanatoa muelekeo mbaya wa hatma ya baadae ya Wanafunzi hao.
Naye Mzee ambae pia ni Mzazi wa Kijiji cha Matetema Mzee Ame Sheha alisema tatizo la kuhamishwa kwa baadhi ya Walimu waliokuwa wakifundisha Skulini hapo limechangia kuzorotesha maendeleo ya Kielimu ya Skuli ya Msingi ya Matetema.
Mzee Ame alisema tatizo hilo limekwenda sambamba na idadi kubwa ya Walimu Wanawake wanaoshindwa uwezo wa kuwadhibiti Wanafunzi wao hasa wale wa Kiume wenye umri mkubwa kidogo.
Aliishauri Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar kufanya uchunguzi wa kina uliopelekea uhamishwaji wa Walimu wa mwanzo waliokuwa wakifundisha Skuli hiyo ambao hadi sasa pengo lao bado halijazibwa na kuathiri harakati za ufundishaji Skulini hapo.
Akitoa ufafanuzi wa changamoto za Wazazi na Wazee hao wa Kijiji cha Matetema, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mh. Riziki Pemba Juma aliwaahidi Wazazi hao kwamba Wizara ya Elimu itawajibika na kuhakikisha kwamba inayachukulia hatua zinazostahiki matatizo hayo ndani ya kipindi kifupi kijacho.
Mh. Riziki alisema changamoto zilizowasilishwa na Wazazi na Wazee hao zinahitaji utafiti wa kina ili Wizara itakapofikia hatua za kuzichukuwa hatua yasijeibuka malalamiko mengine mapya.
Hata hivyo Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali alieleza kwamba Wazee na Wazazi wataendelea kulazimika kuwahamasisha Watoto wao kupenda kuhudhuria masomo yao ili kuwajengea hatma njema ya maisha yao ya baadae.
Waziri Riziki alisema suala la Ufaulu wa Wanafunzi licha ya juhudi kubwa zinazochukuliwa na Wizara ya Elimu pamoja na Walimu katika kuwashajiisha wanafunzi wao kusoma lakini bado litaendelea kubakia mikononi mwa Wazazi wenyewe.
Aliwahimiza Wazazi na Wazee kutoona tabu kupita maskulini kuangalia maendeleo ya Watoto wao na pale wanapogundua mwenendo mbaya wa Walimu kutofundisha wazee hao watalazimika kutoa Taarifa kwa Afisa wa Elimu wa Wilaya yao ili hatua za nidhamu zichukuliwe dhidi ya muhusika huyo.
Mheshimia Riziki Pemba Juma alisema inasikitisha kuona Skuli nyingi hapa nchini hazikufanya vizuri kwenye mitihani yao ya mwaka uliopita wakati Viongozi kwenye maeneo yao wanajitahidi mawajenga mazingira mazuri ya Miundombinu ya Kielimu ya Watoto wao.
Mapema akikiongoza Kikao hicho cha dharura cha Wazee wa Matetema Mwakilishi wa Jimbo la Mahonda ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema matokeo ya mitihani ya wanafunzi wengi yanadhihirisha usimamizi mdogo uliopo unaochukuliwa kwa wanafunzi Maskulini.
Balozi Seif alizishauri Kamati za Maskuli Nchini kuiga mfano wa Kamati kama hizo za miaka ya nyuma zilizojipangia utaratibu wa kuwaita walimu wa skuli zao kuwauliza matatizo yanayosababisha ufaulu mdogo wa Wanafunzi wanaowasimamia.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliendelea kusisitiza kwamba viongozi wakuu pamoja na wale wa Mikoa, Wilana na Majimbo bado wako tayari kutoa aina yoyote ya nguvu katika kuona maendeleo ya Elimu ya Wanafunzi wa Visiwa vya Zanzibar yanastawi na kukua kila mwaka.

Hakuna maoni :
Chapisha Maoni