.

.

.

.

.

.

.

.
KARIBUNI TUHABARIKE, TUELIMISHANE, TUPEANE HABARI ZA KUKUFANYA UTABASAMU KIDOGO NA MATUKIO YALIYOFANYIWA UCHUNGUZI WA KINA TOKA KILA PEMBE CONTACTS: +255 787 377 722 Email: drweyunga@gmail.com PIA UNAWEZA KUNI FOLLOW KUPITIA INSTAGRAM YANGU @drweyunga | TANGAZA NASI ILI UWAFIKIE WATU WENGI ZAIDI.

Jumamosi, 11 Februari 2017

BALOZI IDDI AHIMIZA MABALOZI KUSIMAMIA UHUSIANO WA KIDIPLOMASIA KATI YA TANZANIA NA MATAIFA RAFIKI

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizungumza na kuwaaga Mabalozi Sita wa Tanzania walioteuliwa hivi karibuni kuwakilisha Taifa Nchini Mbali mbali Duniani Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.
Balozi wa Tanzania Nchini Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo {DRC} Balozi Paul Mella kwa niaba ya wenzake akimuahidi Balozi Seif kwenda kutekeleza majukumu yao kwa bidii za kizalendo.
Balozi Seif akiwa katika picha ya pamoja na Mabalozi wa Tanzania nchi za Nje mara baada ya kuzungumza nao na kuwaaga rasmi kwenda kutekjeleza jukumu lao la Kidiplomasia, kushoto ya Balozi Seif ni Balozi wa Tanzania Nchini Uswiss Dr. James Nsekela na kulia yake ni Balozi wa Tnaznia Nchini Uturuki Balozi Elizabeth Kiondo. (Picha zote na OMPR – ZNZ).

Press Release:-

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema suala la kusimamia uhusiano wa Kidiplomasia uliopo kati ya Tanzania na Mataifa Rafiki Duniani ndio kazi ya msingi kwa Mabalozi wote katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku.

Alisema Kazi ya Ubalozi inahitaji uadilifu na ueledi mkubwa unaohitaji kuzingatia zaidi heshima na Matakwa ya Taifa yatakayopelekea kuimarika kwa huhusiano uliotukuka wa pande zote husika.

Balozi Seif Ali Iddi alitoa angalizo hilo wakati akiwaaga Mabalozi Sita walioteuliwa hivi karibuni na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. John Pombe Magufuli kuiwakilisha Tanzania katika Mataifa mbali mbali Duniani.

Alisema Serikali ya Awamu zilizopita nyuma iliwahi kulazimika kuwajeresha nyumbani na wengine kuwafukuza kazi baaadhi ya Mabalozi wa Tanzania baada ya kushindwa kuuheshimu Utumishi wao wa Kidiplomasia.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alielezea matarajio yake ya mafanikio kwa kazi kubwa iliyofanywa na Rais wa Jamuhuri ya MKuungano wa Tanzania Dr. John Pombe Magufuli wa kufanya upembuzi wa kina uliyoibuwa Watumishi hao wa Kidiplomasia watakaokuwa kioo chema cha Tanzania katika Mataifa waliyopangiwa kufanya kazi.


Akigusia suala la Maendeleo ya Uchumi Zanzibar Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi aliwataka Balozi hao wanaoiwakilisha Tanzania katika Mataifa mbali mbali Duniani kuvitangaza Visiwa vya Zanzibar ambavyo kwa kiasi kikubwa vitaendelea kuzitegemea Ofisi za Mabalozi hao.

Balozi Seif alisema Zanzibar hivi sasa inategemea kupata zaidi mapato yake kupitia sekta ya Utalii inayopata msukumo kutoka kwa Taasisi na Makampuni mengi ya nje hasa Taifa ya Italy.

Alimuomba Balozi wa Tanzania Nchini Ufaransa Balozi Samuel Shelukindo kuandaa mazingira ya kukutana na Uongozi wa Shirika la Kimataifa la Sayansi, Elimu na Utamaduni { UNESCO } lenye Makao Makuu yake Nchini humo kujadili na Wataalamu wake kuangalia mazingira ya kuyahami Majengo ya Mji Mkongwe wa Zanzibar ambao kwa kipindi kirefu uko chini ya hifadhi ya Urithi wa Dunia.

Balozi Seif alisema majengo mengi ndani ya Mji Mkongwe hivi sasa hayako katika mazingira mazuri jambo ambalo Unesco ina wajibu wa kusaidia sambamba na kutoa ushauri badala ya kuwa wakali katika kuelekeza pekee.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwaeleza Mabalozi hao wa Tanzania Nchi mbali mbali Duniani kwamba maeneo mengi ya Kihistoria yaliyopo katika Visiwa vya Zanzibar ukiwemo Mji Mkongwe ni chem Chem ya kuimarika kwa mapato yake kupitia sekta ya Utalii.

Balozi Seif Ali Iddi alimuagiza Balozi wa Tanzania Nchini Uturuki Balozi Elizabeth Kiondo kufuatilia mahusiano na Mikataba iliyopo ya muda mrefu kati Uturuki na Tanzania na Zanzibar kwa Ujumla.

Alisema ipo mikataba mingi iliyokwishatiwa saini kati ya Uturuki na Zanzibar katika sekta mbali mbali ikiwemo ile kubwa ya Utalii ambayo inastahiki kufuatiliwa muelekeo na utekelezaji wake.

Naye kwa niaba ya Mabalozi hao wa Tanzania Nchi mbali mbali Ulimwenguni, Balozi wa Paul Mella anayekwenda nchini Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Congo { DRC } alimuahidi Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba watazingatia jukumu walilopewa na Taifa katika kutekeleza wajibu wao.

Balozi Paul alisema Watanzania wana haki ya kujenga matumaini makubwa kutoka kwa Kikosi hicho mahiri kinachoelekea katika eneo lake la uwajibikaji kuisimamia na kuitangaza Diplomasia ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

11/2/2017.

Hakuna maoni :

Chapisha Maoni