Kikao cha kawaida cha Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), kinatarajiwa kukaa Machi 26, mwaka huu ambako pamoja na ajenda nyingine, itaamua tarehe rasmi ya Uchaguzi Mkuu utakaofanyika baadaye mwaka huu.
Kikao hiki cha kawaida, kwa mujibu wa katiba hufanyika mara nne kwa mwaka na huamua masuala mbalimbali ya uendeshaji na usimamizi wa mpira wa miguu nchini.
Kadhalika Mkutano Mkuu wa uchaguzi kwa mujibu wa Katiba ya TFF, hufanyika kila baada ya miaka minne kwa mwaka.
ROBO FAINALI AZAM SPORTS FEDERATION CUP
Mechi mbili za kwanza hatua ya Robo Fainali ya Kombe la Shirikisho Azam (Azam Sports Sports Federation Cup 2016/2017), zitachezwa Machi 18, mwaka huu kwenye viwanja viwili tofauti.
Mechi hizo ni kati ya Kagera Sugar itakayocheza na Mbao FC ya Mwanza kwenye Uwanja wa Kaitaba, mjini Bukoba mkoani Kagera kadhalika Simba itakayosafiri hadi Arusha kucheza na Madini kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha.
Mechi nyingine zitapangiwa tarehe za baadaye. Mechi hizo ni kati ya Azam FC na Ndanda FC kadhalika Tanzania Prisons ya Mbeya itakayocheza na mshindi kati ya Young Africans ya Dar es Salaam na Kiluvya United ya Pwani.
Bingwa wa michuano hiyo kwa mujibu wa kanuni, atazawadiwa Tsh. 50 milioni.
Pia bingwa wa michuano hiyo, ndiye atakayeiwakilisha nchi kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika ya Total wakati Bingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara ndiye ataiwakilisha nchi kwenye michuano ya Total Ligi ya Mabingwa Afrika.
IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni