Mkurugenzi wa Mipango Wizara ya
Fedha na Mipango Bw. Richard Mkumbo (aliyesimama) akisalimiana na
Viongozi waandamizi wa Wizara hiyo kabla ya kuanza kwa mkutano wa 13
wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara ya Fedha na Mipango mjini
Morogoro.
Wajumbe wa Mkutano wa 13 wa Baraza
la Wafanyakazi wa Wizara ya Fedha na Mipango wakiimba wimbo wa
mshikamano daima, mjini Morogoro.
Viongozi waliokaa meza kuu,
wakiongozwa na Mwenyekiti wa Mkutano wa 13 wa Baraza la Wafanyakazi
wa Wizara ya Fedha na Mipango, wakiimba wimbo wa mshikamano daima,
mjini Morogoro.
Wajumbe wa Mkutano wa Baraza la
wafanyakazi wa Wizara ya Fedha na Mipango wakisikiliza kwa makini
maelezo ya mafanikio ya Mkutano wa Baraza hilo kwa mwaka 2015/2016
ambayo ni pamoja na kuboreshwa kwa mazingira ya kazi, Mkutano
uliofanyika Mjini Morogoro.
Katibu wa Baraza la Wafanyakazi la
Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Cyprian Kuyava, akizungumza wakati wa
Mkutano wa 13 wa Baraza hilo, Mjini Morogoro.
Mwenyekiti wa Mkutano wa 13 wa
Baraza la Wafanyakazi wa Wizara ya Fedha na Mipango ambaye pia ni
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Bi. Dorothy Mwanyika, akitoa hotuba
ya ufunguzi wa mkutano huo kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango,
Mhe. Dkt. Philip Mpango (Mb), Mjini Morogoro.
Mkurugenzi wa Idara ya Huduma za
Sheria wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bi. Susana Mkapa, akitoa nen0
la shukrani baada ya hotuba iliyotolewa na Naibu Katibu Mkuu wa
Wizara hiyo Bi. Dorothy Mwanyika, akifungua mkutano wa Baraza hilo
kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango wa Wizara hiyo, Mhe. Dkt.
Philip Mpango (Mb), Mjini Morogoro.
Meza Kuu (Walioketi Mbele)
wakiongozwa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Bi.
Dorothy Mwanyika, wakiwa katika picha ya pamoja na Wakuu wa idara na
vitengo wa Wizara hiyo, mjini Morogoro.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano
Serikalini-WFM)
Na Benny Mwaipaja, WFM-Morogoro
Watumishi wa Wizara ya Fedha na
Mipango nchini wametakiwa kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali
za kuiletea nchi Maendeleo ya haraka kupitia falsafa ya uchumi wa
viwanda utakao iwezesha nchi kuwa ya uchumi wa kati ifikapo mwaka
2025 kwa kusimamia ukusanyaji wa mapato ya Serikali na kusimamia
matumizi yake ipasavyo.
Rai hiyo imetolewa na Waziri wa
Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, katika Hotuba iliyosomwa kwa
niaba yake na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Bi. Dorothy Mwanyika,
wakati akifungua mkutano wa 13 wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara
hiyo unaofanyika mjini Morogoro kwa siku mbili.
Bi. Mwanyika amesema kuwa Mabaraza
ya wafanyakazi sehemu za kazi, yana malengo ya kuongeza tija,
ufanisi na ushirikishwaji wa wafanyakazi katika uongozi wa pamoja
mahali pa kazi kama agizo la Rais Na. 1 la mwaka 1970 likisomwa
pamoja na miongozo mingine linavyo elekeza.
Aidha amewataka wajumbe wa Baraza
hilo kukumbuka maelekezo ya viongozi wakuu wa nchi wakiongozwa na
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe
Magufuli, kuhusu kusimamia ukusanyaji wa mapato na nidhamu ya
matumizi ya Fedha za Umma, ili kujenga uchumi wa Viwanda na kufikia
maendeleo stahiki.
“Tuunge mkono juhudi za Serikali
kwa kutafsri maelekezo ya viongozi kwa vitendo ili kuthibitisha msemo
usemao Wizara ya Fedha na Mipango ndiyo moyo wa Serikali”
alisisitiza Bi. Mwanyika.
Pia Bi. Mwanyika amewashukuru
viongozi wa Wizara hiyo kwa kufanikisha mpango wa Serikali wa kuhamia
Dodoma ambapo katika awamu ya kwanza wafanyakazi 184 wameripoti
mkoani humo licha ya kuwepo kwa changamoto mbalimbali ikiwemo ukosefu
wa makazi. Hata hivyo amewataka watumishi hao kushirikiana katika
kutatua changamoto hizo kwa pamoja.
Kwa upande wake Katibu wa Baraza la
Wafanyakazi wa Wizara hiyo Bw. Cyprian Kuyava, amebainisha mafanikio
yaliyopatikana kutokana na maazimio mbalimbali ya Mkutano uliopita
wa mwaka 2015/2016 kuwa ni pamoja na kuboresha huduma kwa watumishi,
kuboresha mazingira ya kazi na kuongezeka kwa mshikamano miongoni mwa
wafanyakazi licha ya ufinyu wa Bajeti.
Naye Mkurugenzi wa huduma za Sheria
wa Wizara ya Fedha na Mipango Bi Susana Mkapa amesema Watumishi wa
Wizara hiyo wako tayari kuunga mkono juhudi za Serikali za ukusanyaji
wa mapato, kubana matumizi na hatua ya Serikali kuhamia Dodoma.
Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa
Wizara ya Fedha unafanyika kwa siku mbili kuanzia Machi 27 hadi 28,
2017, huku ajenda kuu ikiwa kufanya mapitio ya utekelezaji wa Bajeti
ya Mwaka 2016/2017 na kujadili makadirio ya bajeti ya mwaka
2017/2018.
Mwisho




Hakuna maoni :
Chapisha Maoni