Waziri Mahiga (wa tatu kutoka kulia) akiwa katika picha ya pamoja na Mjumbe Maalum, Balozi Adt (wa nne kushoto) pamoja na Maafisa Waandamizi kutoka Wizarani pamoja na Ubalozi wa Ujerumani nchini.
Waziri
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt.
Augustine Mahiga amesema kuwa Tanzania na Ujerumani zitaendelea
kuimarisha ushirikiano katika masuala mbalimbali ikiwemo yale yanayohusu
kudumisha amani na usalama duniani pamoja na kuheshimu misingi ya haki
za binadamu kupitia Jumuiya za Kikanda na Kimataifa.
Mhe. Waziri Mahiga ameyesema
hayo alipokutana kwa mazungumzo na Balozi Harro Adt, Mjumbe Maalum wa
Kansela wa Ujerumani, Mhe. Angela Merkel kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania, Mhe. John Pombe Magufuli alipofika Wizarani kwa ajili ya
kuwasilisha ujumbe huo.
Katika
mazungumzo yao, Mhe. Waziri Mahiga alisema kuwa, Ujerumani na Tanzania
zina mahusiano ya kihistoria tangu enzi za ukoloni hadi sasa. Katika masuala
ambayo Tanzania inanufaika na ushirikiano huo ni pamoja na ujenzi wa
miundombinu, maboresho katika sekta ya elimu na mchango katika uhifadhi
wa wanayamapori.
“Uhusiano wa Tanzania na Ujerumani ni wa kihistoria tangu ukoloni. Hata hivyo Ujerumani wamejaribu
kutafsiri ushirikiano wetu katika misingi bora sasa kuliko ile ya
kikoloni. Ujerumani imekuwa ikiisaidia Tanzania moja kwa moja katika
sekta mbalimbali kama elimu, wanyamapori na miundombinu na misaada
mingine imekuwa ikipitia Umoja wa Ulaya” alisema Waziri Mahiga.
Akizungumzia
ziara ya Balozi Adt nchini, Mhe. Waziri Mahiga alisema Mjumbe huyo
Maalum wa Kansela wa Ujerumani ameleta ombi kwa Mhe. Rais na kwa
Watanzania la kuiunga mkono Ujerumani kwenye nafasi ya Mjumbe asiye wa Kudumu kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wakati
wa uchaguzi utakaofanyika mwaka 2018.
Aliongeza kusema kuwa, Ujerumani
imedhamiria kugombea nafasi hiyo ikiwa na dhamira ya kuunga mkono
mageuzi ndani ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ikiwemo kuziunga
mkono nchi za Afrika kwenye harakati za kupatiwa nafasi mbili za kudumu
kwenye Baraza hilo.
Aidha,
Mhe. Waziri Mahiga alifafanua kwamba, katika kufikia malengo hayo
Ujerumani imejiwekea misingi mikuu minne ambayo ni:- Kusaidia jitihada
za amani na usalama duniani; Kusimamia Haki ndani ya Baraza la Usalama
la Umoja wa Mataifa; Kuhamasisha mageuzi ya Teknolojia na Kuhimiza
ushirikiano na Ubia wa Kimataifa.
Mhe.
Mahiga alieleza kuwa kwa kuzingatia misingi hiyo, amemueleza Balozi Adt
azma ya Tanzania kuiomba Ujerumani iisadie Afrika kujenga Jengo la
Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu ambapo Tanzania ndio
Makao yake Makuu huko Mjini Arusha.
Mhe. Mahiga pia alimhakikishia Balozi Adt kuwa ameupokea ujumbe wa Kansela wa Ujerumani na atauwasilisha kwa Mhe. Rais.
Kwa
upande wake Balozi Adt, Mjumbe Maalum kutoka Ujerumani alisema kuwa
amefurahishwa na mapokezi aliyoyapata baada ya kuwasili nchini. Pia ana
imani kuwa Tanzania ambao ni rafiki wa kihistoria wa Ujerumani itawaunga
mkono kwenye nafasi hiyo ili kuwawezesha kutekeleza malengo
waliyojiwekea ikiwemo kuhakikisha Afrika inapata nafasi mbili za kudumu
kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
-Mwisho-
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dar es Salaam, 12 Machi, 2017
|
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni