Na Dotto Mwaibale
BENKI ya NMB imetoa msaada wa vifaa vya michezo vyenye thamani ya sh. milioni 10 kwa timu ya Singida United kwa ajili ya maandalizi ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara itakayoendelea kuanzia mwezi Agosti mwaka huu.
Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo makao makuu ya benki hiyo jijini Dar es Salaam leo, Ofisa Mkuu wa Wateja Wakubwa na Serikali, Richard Makungwa alisema msaada huo umelenga kusaidia timu hiyo kwa ajili ya kujiandaa kwa ligi hiyo.
“Tumetoa msaada huu kwa timu ya Singida United kwa kwa ajili ya maandalizi ya ligi hiyo na hii ni kawaida yetu kusaidia timu mbalimbali pale tunapopata nafasi” alisema Makungwa.
Makungwa alisema licha ya benki hiyo kufanya shughuli za kibenki pia imejikita kuinua michezo nchini kwa kutoa msaada wa vifaa vya michezo.
Alitaja vifaa walivyotoa msaada kwa timu hiyo ni viatu vya mpira wa miguu, jezi na mipira vyote vikiwa na thamani ya sh.milioni 10.
Katibu wa timu hiyo Abdurahman Sima alisema vifaa hivyo walivyopata vitatumika kwa lengo lililokusudiwa na si vinginevyo.
“Tunaishukuru benki ya NMB kwa msaada huu tunaomba wadau wengine kuiga mfano wa benki hii ” alisema Sima.
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni