.

.

.

.

.

.

.

.
KARIBUNI TUHABARIKE, TUELIMISHANE, TUPEANE HABARI ZA KUKUFANYA UTABASAMU KIDOGO NA MATUKIO YALIYOFANYIWA UCHUNGUZI WA KINA TOKA KILA PEMBE CONTACTS: +255 787 377 722 Email: drweyunga@gmail.com PIA UNAWEZA KUNI FOLLOW KUPITIA INSTAGRAM YANGU @drweyunga | TANGAZA NASI ILI UWAFIKIE WATU WENGI ZAIDI.

Jumatano, 3 Mei 2017

SEKTA YA VIWANDA NCHINI NA ULIPAJI KODI YA MAPATO

CHEMBA ya Madini na Nishati (TCME) imetambua na kuguswa na taarifa zisizo sahihi kwamba kampuni zinazojihusisha na uchimbaji mkubwa wa madini zimekuwa zikifanya shughuli zake hapa nchini bila ya kulipa kodi ya mapato. 

Chemba hii ni muwakilishi wa makampuni wanachama waliorasimisha shughuli zao katika sekta ya madini kuanzia kampuni ndogo za utafiti wa madini hadi wachimbaji wakubwa na wa kati wa madini, pamoja na makampuni yanayotoa huduma kwa makampuni yanayofanya utafiti na uchimbaji wa madini.
 

Chemba na wanachama wake wanaunga mkono uwepo wa sekta ya uchimbaji madini inayoratibiwa vema na inaweka msisitizo mkubwa katika kuhakikisha shughuli za wanachama wake zinaendeshwa kwa kufuata sheria na kanuni zilizowekwa na mamlaka za Serikali hapa nchini.
 

Makampuni ya uchimbaji madini hapa nchini yanaratibiwa kwa kiwango cha juu na mamlaka zilizo chini ya Serikali ili kuhakikisha yanafanya shughuli zake kwa kufuata sheria na kanuni za nchi. Makampuni haya yameendelea kuchangia kwa kiasi kikubwa uchumi wa nchi kwa njia mbali ikiwemo utengenezaji wa ajira pamoja na ulipaji wa kodi.
 

Katika ripoti ya utendaji ya mwaka 2015 ya Wakala wa Ukaguzi wa Madini. Tanzania (TMAA) ambao wanafanya kazi chini ya Wizara ya Nishati na Madini, imeripotiwa kwamba makampuni makubwa ya uchimbaji madini hapa nchini, kwa ujumla wake, kati ya mwaka 2009 na 2015 yameweza kulipa zaidi ya Shilingi Bilioni 870 (USD390 Milioni) kama mrabaha, na zaidi ya Shilingi Bilioni 680 (USD305 Milioni) kama kodi ya mapato, hii ni mbali na kodi nyingine zisizo za moja kwa moja ambazo pia zimelipwa.
 

Katika mwaka wa 2015 pekee, migodi mitano mikubwa ya uchimbaji Dhahabu pamoja na mgodi mmoja wa kuchimba Almasi, kwa pamoja iliweza kulipa zaidi ya Shilingi Bilioni 146 (USD65.5 Milioni) kama mrabaha na zaidi ya Shilingi Bilioni 380 (USD170 Milioni) kama kodi nyingine ikiwamo kodi ya mapato. Viwango hivi ni dhahiri vitakuwa vimeongezeka zaidi kwa mwaka 2016.
 

Zimekuwepo pia taarifa kwamba makampuni haya ya uchimbaji mkubwa wa madini yamekuwa yakifaidika kwa kurejeshewa kodi ya ongezeko la thamani (VAT) pasipo uhalali wa kupata marejesho hayo. Taarifa hizi si sahihi. Ukweli ni kwamba makampuni ya uchimbaji mkubwa wa madini yamekuwa na yataendelea kusafirisha nje ya nchi kwa ajili ya kuuza madini yote ambayo wanayazalisha hapa nchini. 

Kwa mujibu wa Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani ya mwaka 2014 (VAT ACT 2014) wafanyabiashara ambao mauzo yao yote hufanyika nje ya nchi hukadiriwa kodi ya ongezeko la thamani kwa kiwango cha sifuri (zero rated) na kwa sababu hiyo basi hustahili kurejeshewa kodi ya VAT ambayo huilipa kupitia manunuzi anayoyafanya hapa nchini.


Marejesho haya yanafanyika kwa uhalali na yanafuata matakwa ya sheria ya VAT. Ni muhimu ikaeleweka kwamba makampuni haya bado yanalipa kodi ya VAT ambayo huwa hairejeshwi iwapo yatafanya manunuzi ya bidhaa ama huduma ambazo kisheria hazistahili marejesho. 


Kwa mfano makampuni haya yameendelea kulipa bila kurejeshewa kodi ya VAT pale yanapofanya manunuzi hapa nchini ya huduma za chakula kwa wafanyakazi wake pamoja na manunuzi ya vipuri vya kwa ajili ya magari madogo ambayo ndiyo yaliyo mengi huko migodini.
 

Ikumbukwe kwamba sheria ya VAT ambayo makampuni ya uchimbaji madini yanafanya kazi chini yake ndiyo hiyo hiyo ambayo inatumika pia kwa makampuni katika sekta nyingine za uzalishaji ambayo mauzo yao yote hufanyika nje ya nchi.
 

Kwa mujibu wa ripoti ya TMAA ya mwaka 2015 sekta rasmi ya uchimbaji madini mkubwa inatoa ajira za moja kwa moja 7,355 na zaidi ya 3,000 kupitia makampuni ya wakandarasi. Kwa mujibu wa tafiti zilizofanyika huko nyuma ajira moja rasmi uhudumia watu wengine 11 wasio na kazi. 

Kwa mantiki hiyo sekta rasmi ya madini inawezesha wastani wa watu 114,000 kuendelea kuishi na kupata huduma za msingi. Kodi zinazolipwa na makampuni ya madini husaidia kufanikisha shughuli mbali mbali za maendeleo ikiwamo ujenzi wa miundombinu muhimu kwa maendeleo ya nchi yetu.



Chemba itaendelea kushirikisha taasisi, mamlaka, vyombo mbali mbali vya habari pamoja na jamii kwa ujumla, katika kuboresha uelewa wa wananchi na mamlaka za nchi kuhusu jinsi gani wanachama wake wanatii sheria za nchi kuhusu kulipa kodi na tozo mbali mbali kwa mujibu wa sheria na kanuni. 


Vile vile tutaendelea kuelimisha jamii kuhusu mchango mkubwa ambao sekta rasmi ya uchimbaji madini hapa nchini imekuwa ikiutoa katika uchumi wa nchi yetu kupitia uwekezaji, ulipaji wa kodi, utengenezaji wa ajira, kuchangia soko la fedha za kigeni, manunuzi ya huduma pamoja na michango ya hiyari (CSR) kwa shughuli mbali mbali za maendeleo ya jamii.
 

Ni jambo la muhimu sana kuhakikisha kwamba wadau wa sekta hii wanaielewa kwa ufasaha jinsi inavyoendeshwa na kisha waiunge mkono ili iendelee kukua na kuchangia zaidi katika pato la taifa.
 

Ni muhimu ifahamike kwamba pamoja na kuwa na mikataba ya kisheria (MDA’s) ambazo zinatoa unafuu wa tozo na kodi mbalimbali kwayo, bado makampuni haya yameridhia kutekeleza matakwa kadhaa yaliyoingizwa na kanuni na sheria ya uchimbaji madini ya mwaka 2010 (Mining Act, 2010) ili hali baadhi ya matakwa hayo yanakwenda kinyume na mikataba (MDA’s) ambayo Serikali iliingia na makampuni haya yalipokuja kuwekeza hapa nchini kwa mara ya kwanza. 

Kwa mfano badala ya makampuni haya kulipa kiwango kisichozidi dola za kimarekani 200,000 kwa mwaka kwa halmashauri kama ushuru wa huduma, makampuni haya yamekubali kulipa ushuru huo kwa kiwango cha 0.3% ya thamani ya mauzo yote ya madini. Makampuni pia yamekubali kulipa mrabaha kwa kiwango cha 4% badala ya 3% iliyo kwenye mikataba ya hapo awali.

Kuhusu Sekta ya Madini Tanzania
 

Historia ya uchimbaji wa madini hapa chini inaanzia enzi za ukoloni wakati wafanyabiashara wazawa na wale wa ki-Arabu walipochimba na kuuza maliasili za nchi hii ikiwemo Dhahabu, Shaba, Fedha, Chuma na Chumvi. Uchimbaji wa kwanza wa kibiashara wa dhahabu ulifanyika katika eneo linalozunguka ziwa Victoria chini ya utawala wa ki-Jerumani kati ya miaka ya 1890. 

Kati ya miaka ya 1920 na 1930 miradi kadhaa ya uchimbaji iliendelezwa na wamiliki kutoka Uingereza pamoja na Afrika ya Kusini. Mojawapo ya miradi hiyo ilikuwa mgodi wa Almasi wa Williamson kule Mwadui.


Kufuatia kupatikana kwa Uhuru wa Tanganyika mwaka 1961, uendeshaji wa sekta ya madini uliwekwa chini ya Serikali na taasisi zake kama vile Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) na Shirika la Uchimbaji Madini la Taifa (STAMICO). Sera mpya na sheria zilizopitishwa mwishoni mwa miaka ya 1990 ziliwavutia wawekezaji wageni ambao walianzisha migodi mikubwa ya uchimbaji wa dhahabu. 


Mgodi wa kwanza wa aina hii ulianza uzalishaji mwezi Novemba 1998. Kwa sasa hivi nchi yetu ina migodi mikubwa mitano ya uchimbaji wa Dhahabu na mgodi mmoja mkubwa wa uchimbaji Almasi. Ipo pia migodi mingine ya Dhahabu na Almasi ya kiwango cha kati pamoja na makampuni kadhaa yanayoendeleza utafiti wa mashapo yenye madini kwa ajili uanzishwaji wa migodi mingine siku zijazo kwa faida ya wadau wote.


Migodi yote mikubwa ya uchimbaji madini iwe ya Dhahabu au madini mengine yoyote ni miradi ambayo huhitaji mitaji mikubwa kuweza kuianzisha na utaalamu wa hali ya juu kuiendesha. Kwa mantiki hiyo miradi hii huchukua muda mrefu kabla muwekezaji hajarudisha gharama zake za uwekezaji na kuanza kutengeneza faida inayostahili kukatwa kodi ya mapato. Hii haimaanishi kwamba migodi hii inapata hasara bali ina maana kwamba kipato kinachozalishwa hakijawa na sifa ya kukatwa kodi.
 

Hali hii ni ya kawaida katika ulimwengu wa uchimbaji mkubwa wa madini na Tanzania haiwezi kuiepuka. Majira ambapo kampuni itatakiwa kuanza kulipa kodi ya mapato yanaweza kutofautiana na makisio yaliyoonyeshwa kwenye upembuzi yakinifu wakati mradi husika unaanza kutokana na sababu mbali mbali ikiwamo kuporomoka kwa bei ya madini husika na kupanda kwa bei ya mali ghafi zinazotumika kwenye uzalishaji.
 

Katika kipindi ambacho mwekezaji huendelea kurejesha mtaji wake mgodi huendelea kuchangia pato la taifa na uchumi wa nchi husika kwa kulipa kodi zisizo za moja kwa moja kama vile ushuru wa forodha, kodi ya zuio, ushuru wa huduma, tozo ya kuendeleza stadi, (SDL) pamoja na PAYE na michango ya hifadhi ya jamii ambayo pamoja na kwamba inatozwa kwa waajiriwa (na sehemu fulani hulipwa na mwajiri - kwa michango ya hifadhi ya jamii) michango hiyo isingekuwepo kama wafanyakazi wasingekuwa wameajiriwa katika mgodi husika.
 

Vile vile ni vema ikaeleweka kwamba hali hii ya kuchelewa kulipa kodi ya mapato hadi pale gharama za uwekezaji wa mwanzo zitakaporudi si pekee kwa kampuni za uchimbaji madini tu bali iko hivyo hata katika sekta nyingine za uzalishaji. Tofauti pekee ni kwamba muda wa kusubiri huwa mrefu zaidi kwa uwekezaji kwenye sekta ya madini kutokana na ukweli kwamba mtaji wake wa mwanzo huwa ni mkubwa mno. 

Chemba itaendelea kushirikiana na kuhamasisha mashauriano na Serikali kuhusu changamoto mbali mbali zinazoikabili sekta hii ili kuhakikisha zinatatuliwa na kuiwezesha Tanzania kunufaika ipasavyo na maliasili zake.

Imetolewa na Mwenyekiti
Tanzania Chamber of Minerals and Energy

Hakuna maoni :

Chapisha Maoni