Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi na salamu za pole kwa vifo vya wanafunzi Mkoani Arusha.
Salamu hizo za pole zimetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kwa niaba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Ali Mohamed Shein na Wananchi wote wa Zanzibarn kufuatia msiba huo mzito kwa Taifa.
Balozi Seif Ali Iddi alisema Wananchi wa Zanzibar wamepokea kwa huzuni, masikitiko na mshtuko mkubwa taarifa ya ajali hiyo iliyotokea katika Kijiji cha Rhotia, Wilaya ya Karatu Mkoani Arusha na kusababisha vifo hivyo pamoja na Majeruhi kadhaa.
Alisema huo ni msiba mkubwa siyo tu kwa Wazazi, Ndugu na Jamaa wa Watoto hao bali pia ni kwa Taifa zima, kwani Watoto hao walikuwa nguvu kazi kubwa iliyotumainiwa kuja kulitumikia Taifa laWatanzania baada ya kumaliza Masomo yao.
Balozi Seif alimuomba Mwenyezi Mungu awape wazazi na familia za Watoto hao moyo wa subira na uvumilivu katika kipindi hichi kigumu cha msiba na Wananchi wote Nchini Tanzania wako pamoja katika msiba huo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar pia alimuomba Mwenyezi Muungu mola wa viumbe wote azilaze roho za marehemu wote mahali pema pepono amin na wale majeruhi awaponyeshe haraka ili warudi kuendelea na maisha yao ya kila siku.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

Hakuna maoni :
Chapisha Maoni