WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewahakikishia wananchi wa wilaya ya Ileje kwamba Serikali itajenga kwa kiwango cha lami barabara ya Mpemba-Isongole.
Amesema barabara hiyo yenye urefu wa kilomita 58 ni muhimu kwa maendeleo ya Taifa kwani itafungua fursa za kiuchumi na kupunguza kero ya usafiri kwa wananchi.
Aliyasema hayo jana jioni (Jumamosi, Julai 22, 2017) alipozungumza na wananchi wa wilaya ya Ileje kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa Stendi.
Waziri Mkuu alisema barabara hiyo itawawezesha wananchi wa wilaya ya Ileje mkoani Songwe, ambao wana mazao mengi kuyafikia masoko kwa urahisi.
“Ujenzi wa barabara hiyo utaongeza fursa za kiuchumi katika Wilaya ya Ileje, hasa kufungua biashara za mipakani kati ya nchi ya Tanzania na Malawi.”
Alisema Serikali imedhamiria kuwaondolea wananchi changamoto mbalimbali hasa miundombinu ya barabara, hivyo aliwaomba waendelee kuiamini na kushirikiana nayo.
Awali Mkuu wa wilaya hiyo, Bw. Joseph Mkude alisema kiasi cha fedha kinachotolewa kwa matengenezo ya barabara hakitoshi ukilinganisha na ubovu wa barabara zao.
Kufuatia hali hiyo Mkuu huyo wa wilaya aliiomba Serikali kuipa kipaumbele miradi ya ujenzi wa barabara iliyo kwenye ukanda wa mvua nyingi ili zipitike wakati wote.
Pia alisema wilaya hiyo inakabiliwa na tatizo la uharibifu wa barabara unaofanywa na wananchi wasio waadilifu, hivyo kuhitaji matengenezo ya mara kwa mara.
Hata hivyo alisema kwa sasa wanatoa elimu ya utunzaji na ulinzi wa miundombinu ya barabara kwa wananchi ili kupunguza gharama za matengenezo ya kila mara.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni
(
Atom
)
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni