.

.

.

.

.

.

.

.
KARIBUNI TUHABARIKE, TUELIMISHANE, TUPEANE HABARI ZA KUKUFANYA UTABASAMU KIDOGO NA MATUKIO YALIYOFANYIWA UCHUNGUZI WA KINA TOKA KILA PEMBE CONTACTS: +255 787 377 722 Email: drweyunga@gmail.com PIA UNAWEZA KUNI FOLLOW KUPITIA INSTAGRAM YANGU @drweyunga | TANGAZA NASI ILI UWAFIKIE WATU WENGI ZAIDI.

Jumatano, 19 Julai 2017

BALOZI SEIF AFUNGUA TAMASHA LA 22 LA UTAMADUNI WA MZANZIBAR

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali
Iddi akifurahia vitu vya sanaa za mkono wakati alipotembelea maonyesho
ya Wajasiri Amali kabla ya kuzindua Tamasha la 22 la Utamaduni wa
Mzanzibari
Balozi Seif akihitaji maelezo kutoka kwa Mjasiri
amali wa sanaa ya vitu vya ufinyanzi kwenye maonyesho ya kazi za sanaa
katika uwanja wa Kumbu kumbu ya Mapinduzi Kisonge Michenzani Mjini
Zanzibar.
Mjasiri amali wa utengenezaji wa vitu vya sanaa
ya asili Viatu vya Mitarawanda kutoka Shehia ya Bweleo Bwana Ali
Mwinjuma Kirobo akimpatia maelezo Balozi Seif wakati alipotembelea
banda lao
Wasanii mbali mbali kutoka Wilaya za
Unguja wakionyesha umahiri wao katika udumishaji wa Utamaduni wa
Mzanzibari hapo Kisonge Mnara wa Kumbu kumbu.
Balozi Seif akionyesha umahiri wake katika kucheza
ngoma ya ndege kutoka Skuli ya Msingi Kisiwandui iliyokuwa ikitumbuiza
kwenye hafla ya ufunguzi wa Tamasha la 22 la Utamaduni wa Mzanzibari
hapo Mnara wa kumbu kumbu Michenzani Mjini Zanzibar.

Picha na – OMPR – ZNZ.
 
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amesisitiza
umuhimu wa Jamii Nchini kuendelea kukuza maadili na kujiepusha na
vitendo vya  unyanyasi wa kijinsia dhidi ya Watoto na Wanawake  ili
irejeshea heshima yake Zanzibar.
Alisema Visiwa vya Zanzibar havikuwa ni kituo muhimu cha Biashara
katika mkarne zilizopita bali pia vilikuwa ni kitovu cha Elimu,
heshima, ustaarabu na ukuzaji wa silka, mila na desturi za Utamaduni
wa asili.
Akilifungua Tamasha la 22 la Utamaduni wa Mzanzibari hapo katika
Mnara wa Kumbukumbu ya Mapinduzi Michenzani Mjini Zanzibar Balozi Seif
Ali Iddi aliwaomba wana Jamii kushirikiana na Wizara inayosimamia
Utamaduni katika kuuenzi Utamaduni wa Taifa hasa kuhamasisha jamii
kuepuka tabia zisizofaa zinazowadhalilisha Watoto, Wanawake na Watu
wenye mahitaji Maalum.
Balozi Seif alisema suala la kukuza utamaduni si jambo geni na ni
vyema wazazi wa karne hii wakaiga mifano ya Wazazi wa zamani
waliotumia mbinu mbali mbali zikiwemo sherehe za jando na unyago mfumo
uliomtayarisha Kijana wa Kike na wa Kiume  namna ya kukabiliana na
maisha yake ya baadae.
Alisema mfumo huo wa malezi uliozingatia heshima iliyopevuka Wazee
hao pia walijumuisha matumizi ya hadithi, nyimba na hata misemo ya
kiswahili katika kujenga tabia za Vijana zinazokubalika katika Jamii
na Taifa kwa ujumla bila ya kutokea mgongano katika imani za Dini na
Makabila.



Balozi Seif alikumbusha kwamba Jamii iliyopita iliishi  kwa Utamaduni
wa kusaidiana malezi bila ya kulaumiana wala kudombana jambo ambalo
liliashiria kuwepo kwa maadili mema katika jamii yaliyodhibiti
matatizo ya udhalilishaji wa kijinsia ambao kwa sana unaonekana kama
jambo la kawaida.
Alisisitiza Wajibu wa Wazazi katika kushirikiana na Serikali na
Taasisi zinazohamasisha  haki za Watoto na Wanawake kuwafichua waovu
wanaoendeleza vitendo vya  kikatili vya ubakaji badala ya kuwatetea
waovu hao waliokusudia kuliangamiza Taifa la baadae.
Balozi Seif alieleza kwamba ni uhimu kwa Wananchi, Wazazi, Walimu wa
Skuli hata wale wa Vyuo vya Quran kusimamia ipasavyo malezi ya Vijana
kwa pamoja kwa vile wana nafasi kubwa ya kusaidiana na malezi hayo na
utoaji wa miongozo kwa vijana wao.
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na hata ile ya Jamuhuri ya Muungano
wa Tanzania zimeandaa Mikakati kadhaa katika kuhakikisha kwamba wale
wote watakaohusika na vitendo vya udhalilishaji wa Watoto, Wanawaka na
Watu wenye Mahitaji Maalum  wanachukuliwa hatua za kinidhamu na
Kisheria.
 
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alielezea faraja yake kutokana
hatua kubwa zinazochukuliwa na Taasisi Maalum zilizomo ndani ya Wziara
ya Kazi, Uwezeshaji, Vijana, Wazee, Wanawake na Watoto wakishirikiana
na Taasisi za Kiraia zinasimamia kadhia hizo ambazo zinapigwa vita
Kitaifa na Kimataifa.
 
Aliipongeza Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo kwa
maandalizi mazuri ya mwaka huu yaliyojumisha shughuli mbali mbali
zilizojumuisha  Vikundi tofauti vya Wajasiri Amali wa Kazi za Mikono.
Balozi Seif alisema kwmba hiyo inadhihirisha wazi kuwa ndani ya
Utamaduni wa Taifa zimo hazina zitakazosaidia kuongeza Kipato cha
Wananchi  kupitia kazi zao za ujasiri amali.
 
“ Wajasiri Amali wana umemo wao wanaouamini usemao Utamaduni wako
ajira yako ”. Alifafanua Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi
Seif Ali Iddi.
 
Aliishauri Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo kuendelea na
desturi yake ya kushirikiana na Taasisi nyengine zenye kufanya
Matamasha  ya Utamaduni kwa lengo la kwenda sambamba na kasi ya
kuulinda Utamaduni wa Asili.
 
Alisema Matamasha hayo kama lile la Filamu la Kimataifa {ZIFF},
Tamasha la Mwaka Kogwa, Tamasha la Jahazi na Tamasha la Vyakula vya
asili la Makunduchi  yana mchango mkubwa katika kukuza Utamaduni wa
Zanzibar na ni vyema yakadumishwa zaidi.
 
Akitoa Taarifa ya Tamasha hilo Katibu Mkuu Wizara ya Habari Utamaduni,
Utalii na Michezo Nd. Omar Hassan Omar alisema lengo la Tamshala
Utamaduni wa Mzanzibari ni kukuza na kuendeleza sanaa ya Utamaduni,
kuwakusanya pamoja wazalishaji wa sanaa ili kulinda urithi wa
Zanzibar.
 
Hata hivyo Ndugu alisema Utamaduni wa Zanzibar unapita katika  wakati
mgumu wa mmong’onyoko wa maadili kutokana na baadhi ya watu waovu
kuendeleza Kisisi na uvundo wa ubakaji mambo ambayo lazima Jamii
ijikaze katika kukabiliana nayo.
 
Alisema vitendo hivyo mbali ya kulitia aibu Taifa lililokulia katika
maadili ya heshima  lakini pia linarudisha nyuma maendeleo ya wananchi
kutokana na athari kubwa wanayoipata watu wanaoathirika na ubakwaji.
Katibu Mkuu huyo wa Wizara ya Hari, Utamaduni, Utalii na Michezo
waliwahimiza na kuwaomba wananchi Mjini na Vijijini kutumia fursa ya
kuangalia maonyesho mbali mbali ya kazi za wajasiria amali wa fani ya
sanaa ndani ya Wiki nzima ya Tamasha litakaloendelea hadi Tarehe 25
mwezi huu.
 
Akimkaribisha Mgeni Rasmi kulifungua Tamasha hilo Waziri wa Habari,
Utamduni, Utalii na Michezo Mh. Rashid Ali Juma aliisisitiza Jamii
kutilia nguvu Ujumbe wa Mwaka huu wa Tulinde Maadili yetu kupinga
udhalilishaji ili kurejesha hadhi ya Utamaduni Zanzibar.
 
Utamaduni ni moja ya tasnia inayokuwa kwa kasi Duniani ambayo imekuwa
ikikuza Sekta ya Utalii inayotegemewa kuwa muhimili wa Taifa. Hivyo
aliwapongeza Wajasiri amali kwa juhudi wanazochukuwa katika kuimarisha
kazi za sanaa.
 
Alisema ipo haja ya kutenga eneo maalum la kutunza na kuendelea na
kufufua vitu vilivyoanza kupotea ambavyo ni nembo na ishara
inayoitangaza Zanzibar Kiutamaduni na kuipatia sifa Zanzibar
Kimataifa.
 
Mapema Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif aliangalia
maonyesho ya Vikundi vya wajasiri amali kutoka Wilaya mbali mbali za
Unguja na kuridhika na kazi kubwa inayoendelea kufanya na wasanii hao
katika kulinda na kuendeleza sanaa ya Zanzibar.
 
Balozi Seif pia akapokea gwaride la vikundi vya sanaa vilivyojumuisha
ngoma za asili kama ngoma ya ndege, Meni Bati, Boso,Mkurungu, usukaji
wa vifaa vya sanaa, Dhikiri pamoja na Maulidi ya Homu.
Ujumbe wa Mwaka huu wa Tamasha la Utamaduni wa Mzanzibari unaeleza – “
Tulinde Maadili yetu kupinga udhalilishaji ”.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa  Pili wa Rais wa Zanzibar
19/7/2017.


Hakuna maoni :

Chapisha Maoni