WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema
safari ya Watanzania kuachana na nguo za mitumba imewadia kutokana na
uwepo wa viwanda vya kutengeneza nguo nchini.
Pia amesema uwepo wa viwanda hivyo
utasaidia wakulima wa pamba kupata soko la uhakika hivyo amewataka
walime pamba ya kutosha ili viwanda vipate malighafi.
Waziri Mkuu alitoa kauli hiyo jana
(Jumamosi, Julai 15, 2017) wakati alipotembelea kiwanda cha nyuzi cha
Namera kilichoko Gongo la Mboto na kiwanda cha nguo cha Nida
kilichopo Ubungo Dar Es Salaam.
Alisema viwanda vya kutengeneza nguo
nchini ni ushahidi tosha kwamba nchi iko njiani kuondokana na
matumizi ya nguo za mitumba kwa kuwa nguo nyingi zitakuwa
zinatengenezwa nchini, hivyo kupatikana kwa bei nafuu.
Alisema kwa sasa wanunuzi wa pamba
hawana sababu ya kwenda kuuza nje ya nchi na badala yake wauze katika
viwanda vya ndani ili vizalishe nguo za kutosha zitakazouzwa nchini
kwa gharama nafuu.
“Pamba yote inaweza kuchakatwa
nchini, hivyo hakuna haja ya kuiuza nje ya nchi. Natoa wito kwa
wakulima wetu wa pamba walime mazao ya kutosha kwa sababu soko la
uhakika ipo na hii ndio safari ya mwisho ya mitumba.”
Awali Waziri Mkuu alitembelea
kiwanda cha saruji cha Lake kinachozalisha saruji ya nyati ambapo
aliwapongeza wawekezaji wote nchini kwa kuunga mkono jitihada za Rais
Dkt. John Magufuli za kuifanya Tanzania kuwa ya uchumi wa viwanda.
Katika kiwanda hicho ambacho
kinazalisha tani 700,000 kwa mwaka kimeajiri watu 2000 na kinalipa
kodi ya sh. bilioni 81.312 kwa mwaka, Waziri Mkuu aliwataka
watumishi wake wawe waaminifu, wafanye kazi kwa weledi na wawe
waadilifu.
Pia Waziti Mkuu alitoa wito kwa
wamiliki wa viwanda vyote nchini kuhakikisha wanatoa kipaumbele cha
ajira kwa wananchi waishio katika maeneo ya karibu na viwanda
sambamba na kulipa kodi kwa wakati na kwa viwango sahihi.
(mwisho).
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAPILI, JULAI 16, 2017
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni