.

.

.

.

.

.

.

.
KARIBUNI TUHABARIKE, TUELIMISHANE, TUPEANE HABARI ZA KUKUFANYA UTABASAMU KIDOGO NA MATUKIO YALIYOFANYIWA UCHUNGUZI WA KINA TOKA KILA PEMBE CONTACTS: +255 787 377 722 Email: drweyunga@gmail.com PIA UNAWEZA KUNI FOLLOW KUPITIA INSTAGRAM YANGU @drweyunga | TANGAZA NASI ILI UWAFIKIE WATU WENGI ZAIDI.

Jumatatu, 24 Julai 2017

WAZIRI MKUU AMSIMAMISHA KAZI DED WA MBOZI KWA MATUMIZI MABAYA YA FEDHA

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemsimamisha kazi Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Mbozi mkoani Songwe, Bw. Eliseyi Mgoyi pamoja na maofisa wengine watatu kwa tuhuma za matumizi mabaya ya fedha za umma.

Pia amemuagiza Kamanda wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoa wa Songwe, Bw. Damian Sutta kuwakamata na kuanza kuwachunguza haraka maofisa hao na kisha ampelekee taarifa ofisini kwake.

Waziri Mkuu amewasimamisha kazi maofisa hao leo (Jumapili, Julai 23, 2017) wakati alipozungumza na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi kwenye ukumbi wa Shule ya Sekondari Vwawa, akiwa katika ziara yake ya kikazi.

Maofisa wengine waliosimamishwa kazi ni pamoja na Mweka Hazina wa Halmashauri hiyo Bw. Simon Noel, Bw. Bahati Chomoka ambaye ni Cashier na Bw. Remmy Haule ambaye ni Ofisa Ugavi.

Waziri Mkuu amesema Maofisa hao wamekiuka sheria za matengenezo ya magari ya Serikali kwa kwenda kutengeneza katika gereji ambazo hazikusajiliwa na wala hazifanyi shughuli hiyo, jambo ambalo halikubaliki.

Amesema Kampuni ya Umbwila ni moja kati ya Kampuni zinazolipwa fedha nyingi za utengenezaji wa magari ya Halmashauri ya wilaya ya Mbozi huku ikiwa haina sifa za kufanya kazi hiyo ya utengenezaji magari.Kampuni zingine ni Julius Diesel, Kasaba na Mtoni Garage.

“Mfano duka la Umbwila ambalo linauza vipuri vya magari lakini Halmashauri inalilipa fedha kwa ajili ya utengenezaji wa magari jambo ambalo si sahihi kwa sababu lile ni duka la vipuri na si gereji. Wanamlipa muuza vipuri kama mtengeneza magari”

Waziri Mkuu ameongeza kuwa “hatuwezi kuendesha Serikali kwa namna ambayo haikubaliki kwani watu tuliowapa dhamana ndio wanaongoza kwa vitendo vya rushwa na ufisadi. Wameifanya Halmashauri hii kama shamba la bibi.”

Kufuatia hali hiyo, Waziri Mkuu amemtaka Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Mheshimiwa Eric Ambakisye kuhakikisha anasimamia vizuri utendaji ndani ya Halmashauri hiyo na kwamba Serikali inataka watu waadilifu na wenye uaminifu na nidhamu.

“Halmashauri inanuka rushwa tunataka iwe safi. Hatuwezi kukubali kuona Halmashauri hii na zingine nchini zikigeuzwa kuwa magenge. Kwa Serikali hii no, hatuhitaji rushwa wala harufu ya ufisadi.”

Waziri Mkuu amesema Serikali haiwezi kuvumilia kuona watumishi waliopewa dhamana wakijinufaisha kwa fedha za umma na kuwaacha wananchi wakiendelea kuteseka kwa kukosa huduma mbalimbali za kijamii zikiwemo za maji, afya na elimu, hivyo itaendelea kuwachukulia hatua.

Pia Waziri Mkuu amewataka Madiwani na Wakuu wa Idara katika Halmashauri zote nchini wabadilike na wahakikisha wanashirikiana na kufanya kazi kwa ushirikiano kwani wakigawanyika watashindwa kutekeleza majukumu yao ya kuwatumikia wananchi.

IMETOLEWA NA: 

OFISI YA WAZIRI MKUU

Hakuna maoni :

Chapisha Maoni