.

.

.

.

.

.
KARIBUNI TUHABARIKE, TUELIMISHANE, TUPEANE HABARI ZA KUKUFANYA UTABASAMU KIDOGO NA MATUKIO YALIYOFANYIWA UCHUNGUZI WA KINA TOKA KILA PEMBE CONTACTS: +255 787 377 722 Email: drweyunga@gmail.com PIA UNAWEZA KUNI FOLLOW KUPITIA INSTAGRAM YANGU @drweyunga | TANGAZA NASI ILI UWAFIKIE WATU WENGI ZAIDI.

Alhamisi, 10 Agosti 2017

WAFUGAJI LONGIDO WAANZA KUNUFAIKA NA UJENZI WA SOKO LA KISASA LA MIFUGO

LONG1
Katibu Tawala wa Wilaya ya Longido mkoani Arusha, Bw. Toba Nguvila (kushoto), akimweleza jambo Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Afrika-AfDB, Kanda ya Afrika Mashariki, Dkt. Nyamajeje Weggoro (katikati) kabla ya kutembelea Soko la Kisasa Mifugo linalojengwa katika kijiji cha Worendeke, kata ya Kimokouwa, wilayani Longido, mkoani Arusha, linalojengwa kutokana na mkopo wenye masharti nafuu wa sh. Milioni 650 kutoka Benki hiyo. Kulia ni Afisa anayeshughulikia Dawati la Beni ya Maendeleo ya Afrika-AfDB kutoka Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Said Nyenge.
LONG2
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Afrika-AfDB, kanda ya Afrika Mashariki, Dkt. Nyamajeje Weggoro akisikiliza maelezo ya mradi wa ujenzi wa Soko la Kisasa la Mifugo katika kijiji cha Worendeke, kata ya Kimokouwa, wilayani Longido mkoani Arusha, unaogharimu shilingi milioni 650, ikiwa ni mkopo wenye masharti nafuu kutoka Benki hiyo.
LONG3
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Afrika-AfDB, Kanda ya Afrika Mashariki, Dkt. Nyamajeje Weggoro, akisisitiza jambo baada ya kusikiliza maelezo ya mradi huo wa Soko la Kisasa la Mifugo linalojengwa katika kijiji cha Worendeke, kata ya Kimokouwa wilayani Longido mkoani Arusha.
LONG4
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Afrika-AfDB, kanda ya Afrika Mashariki, Dkt. Nyamajeje Weggoro (wapili kulia) akimweleza jambo Katibu Tawala wa wilaya ya Longido mkoani Arusha, Bw. Toba Nguvila, wakati Mkurugenzi huyo alipotembelea na kukagua ujenzi wa Soko la Kisasa la Mifugo, linalojengwa kwa gharama ya shilingi milioni 650 kupitia mkopo nafuu wa Benki hiyo kwa Serikali ya Tanzania.
LONG5
Baadhi ya wafugaji wa kijiji cha Worendeke, kata ya Kimokouwa, wilayani Longido mkoani Arusha, wanaonufaika na uwepo wa soko hilo ambapo wameanza kuuza mifugo yao kwa faida kubwa badala ya kupeleka mifugo yao nchi jirani ya Kenya ambako walikuwa wakipata adha kubwa na faida ndogo kutokana na gharama kubwa walizokuwa wakitumia kufikisha mifugo yao nchini humo.

(Picha zote na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-Wizara ya Fedha na Mipango)

Benny Mwaipaja, WFM, LONGIDO-ARUSHA

WAFUGAJI wilayani Longido Mkoani Arusha wameanza kunufaika na ujenzi wa soko la kisasa la mifugo linalojengwa na Serikali katika kijiji cha Worendeke kata ya Kimokouwa, kupitia mkopo wa fedha kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika-AfDB

Baadhi ya wafugaji wamesema kuwa Soko hilo linalojengwa kwa gharama ya shilingi milioni 650, limewaondolea adha kubwa waliyokuwa wakiipata walipokuwa wakiuza mifugo yao nchini Kenya kutokana na gharama kubwa ya kusafirisha mifugo kwenda huko pamoja na kulipa kodi na ushuru mbalimbali.

Wamesema kuwa kujengwa kwa somo hilo ni mkombozi mkubwa kwao na kwamba hali hiyo itasisimua uchumi wao kwa kuwa wafanyabiashara wa ndani na kutoka Kenya wamekuwa wakiwafuata kwenye soko hilo kununua mifugo yao hatua inayowafanya wapate faida kubwa.

Katibu Tawala wa Wilaya ya Longido, Bw. Toba Nguvila, amesema kuwa soko hilo ambalo ujenzi wa miundombinu yake umekamilika kwa asilimia 85 limeanza kuiingiza Serikali mapato yake ambapo kwa wastani Halmashauri ya wilaya inakusanya wastani wa shilingi milioni 1 kwa siku.

“Asilimia 95 ya wakazi wa wilaya yetu ni wafugaji wa kimaasai ambao kwa kipindi kirefu wameteseka kusafirisha mifugo yao kwenda Kenya na kutopata faida kutokana na gharama kubwa ya kusafirisha, kupitisha mifugo kwenye maeneo ya watu hivyo kulazimika kulipa ushuru, halikadhalika kulipia tozo mbalimbali wakati wakisubiri kuuza mifugo yao” alieleza Bw. Nguvila

Alisema kuwa kuanzishwa kwa soko hilo litakalokuwa na miundombinu muhimu kama vile mizani ya kupimia uzito wa mifugo yao kabla ya kuiuza, si tu kwamba limesababisha wafugaji kupata faida kwa kuuza mifugo yao kwa bei nzuri ya soko, bali pia limeleta neema kwa wafanyabiashara wengine wadogo wakiwemo mamalishe.

“Akina mama wanafanyabiashara zao za kuuza chai na chakula huku kundi kubwa la vijana waliokuwa wakiuza bidhaa zao za kutembeza mikononi katika mpaka wa Kenya na Tanzania-Namanga, ambao wamejiajiri kwa shughuli za kushusha na kupakia mifugo kwenye malori” aliongeza Bw. Nguvila

Alisema kuwa katika kuhakikisha kuwa mifugo inaongezewa thamani, mchakato wa kuanzisha kiwanda kikubwa cha kuchakata nyama kitakachokuwa na uwezo wa kuchakata mifugo 3,000 kwa siku kinatarajiwa kujengwa katika eneo la karibu na soko hilo kwa ajili ya kuuza nyama ndani na nje ya nchi

“Taratibu za kuanzishwa kwa kiwanda hicho zimekamilika na wakati wowote ujenzi wake utaanza hatua ambayo tunaamini watu wetu watanufaika zaidi na biashara ya mifugo kuliko ilivyokuwa hapo awali ikiwa ni juhudi za Serikali ya aAwamu ya Tano ya kuwahudumia wananchi wa hali ya chini ili kuboresha maisha yao” alisisitiza katibu Tawala huyo

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Afrika anayesimamia nchi 7 za Kanda ya Afrika Mashariki, Dkt. Nyamajeje Weggoro, amesema Benki yake imefurahishwa na maendeleo ya ujenzi wa soko hilo litakalochochea uchumi wa wananchi.

Ameahidi kuwa Benki yake inafadhili ujenzi wa masoko mengi ya namna hiyo hapa nchini na nchini nyingine za Kiafrika ili nchi hizo ziweze kukuza uchumi wake na maisha ya watu wake kwa ujumla.

“Benki iko tayari kuendelea kusaidia eneo hili la ujenzi wa masoko ili kuchochea kasi ya maendeleo ya kiuchumi hivyo naushukuru uongozi wa mkoa wa Arusha na Wilaya ya Longido kwa kazi nzuri wanayoifanya kusimamia ujenzi wa soko hili na kwamba ujenzi wake utakamilika kwa wakati kama ilivyopangwa”Alisisitiza Dkt. Weggoro.

Benki ya Maendeleo ya Afrika-AfDB inafadhili ujenzi wa masoko kadhaa Tanzania Bara na Visiwani kupitia mkopo wenye masharti nafuu wenye thamani ya Dola za kimarekani milioni 56 na unatekelezwa kupitia mpango wa kuendeleza miundombinu ya masoko, kuongeza thamani ya mazao na uboreshaji wa huduma za kifedha vjijini.

Hakuna maoni :

Chapisha Maoni