.

.

.

.

.

.

.

.
KARIBUNI TUHABARIKE, TUELIMISHANE, TUPEANE HABARI ZA KUKUFANYA UTABASAMU KIDOGO NA MATUKIO YALIYOFANYIWA UCHUNGUZI WA KINA TOKA KILA PEMBE CONTACTS: +255 787 377 722 Email: drweyunga@gmail.com PIA UNAWEZA KUNI FOLLOW KUPITIA INSTAGRAM YANGU @drweyunga | TANGAZA NASI ILI UWAFIKIE WATU WENGI ZAIDI.

Ijumaa, 10 Novemba 2017

CCM Z'BAR YAKERWA NA VITENDO VYA UDHALILISHAJI WA KIJINSIA

Katibu wa Kamati Maalum ya NEC, Idara ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar Bi. Waride Bakari Jabu. Na Is-haka Omar, Zanzibar.

KATIBU wa Kamati Maalum ya NEC, Idara ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar,Waride Bakari Jabu ameishauri serikali kuunda jopo la wataalamu kutoka taasisi za umma na binafsi watakaofanya Utafiti wa kina na kutoa mapendekezo ya kitaalamu yatakayosaidia kuthibiti vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia kwa wanawake na watoto nchini.

Ushauri huo ameutoa Ofisini kwake Kisiwandui Unguja, wakati akizungumzia tukio la Baba anaetuhumiwa kuwabaka watoto wa kike watatu wa kambo huko Kiungoni Wilaya ya Wete Kisiwani Pemba.

Alisema tukio hilo ni la kinyama ambalo taasisi za kisheria zinatakiwa kutenda haki kwa kutoa hukumu stahiki itakayokuwa fundisho kwa watu wengine wenye tabia kama hizo.

Alisema serikali inatakiwa kuongeza mikakati na mbinu za kutapamba na vitendo hivyo kwa kufanya tafiti za kitaalamu na kuzisimamia taasisi za umma zinazohusika na usimamizi wa sheria za nchini zikiwemo Mahakama,Polisi na Ofisi ya DPP kufanya kazi kwa pamoja ili watu wanaotekeleza vitendo hivyo wachukuliwe hatua za kisheria kwa wakati.

Bi. Waride alisema CCM Zanzibar inalaani vikali vitendo hivyo vinavyowaathiri kisaikolojia wanawake na watoto vinavyotekelezwa na baadhi ya watu wasiokuwa na utu wala maadili mema ya kijamii.

“ Kila mtu kwa nafasi yake ni tupambane na kupinga vitendo vya udhalilishaji kwa kijinsia kwa ni haviathiri wale wanaofanyiwa pekee yao bali madhara yake yanamgusa kila mtu kuanzia ngazi ya familia hadi taifa kwa ujumla.

CCM kikiwa ni chama cha kisiasa kinachotekeleza kwa vitendo falsafa ya ukuaji wa Demokrasia katika misingi ya kuthamini Haki za binadamu na Utawala bora kwa watu wote tutaendelea kupinga udhalilishaji wa aina yeyote kwa binadamu”,. Alisema Bi. Waride na kuongeza kuwa Sera za chama cha Mapinduzi zinajali haki na maslahi ya makundi yote ya kijamii.

Alisema licha ya Serikali na wanaharakati mbali mbali kuthibiti udhalilishaji bado wamekuwa wakirejeshwa nyuma na tabia za baadhi ya wananchi kushindwa kutoa ushahidi mahakamani kwa kuwa na “muhali” yaani kuona aibu ya kutoa ushahidi wa kuwaiginza hatiani watu wanaowafahamu.

Pia aliongeza kuwa endapo jamii itavunja ukimya kwa kuacha tabia ya muhali na rushwa kwa baadhi ya watendaji wa vyombo vya kisheria matukio hayo yatamalizika kabisa , ikizingatiwa kuwa uzoefu unaonyesha kesi nyingi za ubakaji zinawahusisha ndugu na jamaa wa karibu na kifamilia moja.

Alitoa wito kwa wanasiasa, viongozi wa dini na wanaharakati kutokata tamaa dhidi ya vitendo vya udhalilishaji na badala yake watumie vizuri nafasi na ushawishi waliokuwa nao katika jamii kuleta mabadiliko ya kweli yatakayoendeleza heshima na ustaarabu wa Zanzibar Kitaifa na Kimataifa.
“ Zanzibar ni moja ya nchi yenye sifa nyingi nzuri za ustaarabu, hekima, busara na upole wa wananchi wake uliodumu karne na karne, kamwe tusikubali nchi yetu ichafuliwe na watu wachache bali tupambane nao kuenzi heshima tulioachiwa na waasisi wa Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964”, alisisitiza Bi.Waride.

Katibu huyo Bi.Waride aliitaka Mamlaka ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kusimamia vizuri matumizi ya mitandao ya kijamii kwani ni moja ya nyenzo ambayo ikitumiwa vibaya inachangia kuharibu utamaduni na maadili sambamba na kuchochea udhalilishaji wa kijinsia.

Hakuna maoni :

Chapisha Maoni