Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Kulia akiwa pamoja na Ujumbe wa Viongozi wa Kamati ya maandalizi ya Mashindano ya Kitaifa Tanzania ya Watu wenye Ulemavu uliofika Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar kumtaarifu uwepo wa mashindano hayo Mwezi Disemba 2017 Visiwani Zanzibar.
Kushoto ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh,. Mohamed Aboud Mohamed.
Msaidizi Mwenyekiti wa Kamati ya maandalizi ya Mashindano ya Kitaifa Tanzania ya Watu wenye Ulemavu Maalim Mohamed Mwinyi Ramadhan aliyenyanyua Mikono, akitoa Taarifa ya uwepo wa mashindano ya michezo ya Watu wenye ulemavu Zanzibar.
Wa kwanza Kulia ni Balozi Seif akichukua dondoo za maelezo na Msaidizi Mwenyekiti huyo wa Kamati ya maandalizi ya Mashindano ya Kitaifa Tanzania ya Watu wenye Ulemavu Maalim Mohamed Mwinyi Ramadhan.
Kulia ya Maalim Mohamed ni Katibu wa Kamati hiyo Mustafa Nahoda, Bibi Salha Moh’d Ali na Haidar Hasham Madeweya Wajumbe wa Kamati hiyo.
Picha na - OMPR – ZNZ.
Zanzibar imebahatika kuteuliwa Kitaifa kuwa Mwenyeji wa Mashindano ya Michezo ya Watu wenye Ulemavu wa Akili Kitaifa Tanzania inayotarajiwa kufanyika Mwishoni mwa Wiki ya kwanza ya Mwezi ujao wa Desemba Mwaka huu wa 2017.
Mashindano hayo yatafanyika kwa lengo la kufanya mchujo wa kuwapata Wanamichezo bora wa kuiwakilisha Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kwenye michezo ya Dunia ya Olimpiki ya Watu wenye ulemavu inayotarajiwa kufanyika Mwaka 2019 huko Abu dhabi.
Msaidizi Mwenyekiti wa Kamati ya maandalizi ya Mashindano ya Kitaifa ya Watu wenye Ulemavu Maalim Mohamed Mwinyi Ramadhan alieleza hayo wakati Wajumbe wa Kamati hiyo walipokutana na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar kumtaarifu uwepo wa mashindano hayo.
Maalim Mohamed alisema vugu vugu la maandalizi ya mashindano ya Michezo hiyo iliyoasisiwa mwanzoni mwa Miaka ya 80 limeanza rasmi tokea mwanzoni mwa Mwaka huu, huku Zanzibar ikiwa katika harakati za kupokea Wanamichezo 525 kutoka Tanzania Bara kati ya wanamichezo wote 700 watakaoshiriki mashindano hayo ya Kitaifa.
Alisema Zanzibar kwa vile imekuwa na uzoefu mkubwa wa kuibua wanamichezo bora imelenga kutoa wachezaji wengi zaidi watakaojumuika kuunda Timu ya Taifa ya Tanzania itakayoshiriki Mashindao hayo ya Abu dhabi.
Msaidizi Mwenyekiti huyo wa Kamati ya maandalizi ya Mashindano ya Kitaifa ya Watu wenye Ulemavu alimueleza Balozi Seif aliyeambatana na Baadhi ya Mawaziri wanaohusika na sekta za Michezo, Elimu na Watu wenye mahitaji Maalum katika Kikao hicho kwamba jukumu la Zanzibar katika michezo hiyo ni kushughulikia masuala ya usafiri pamoja na Malazi.
Hata hivyo Maalim Mohamed alisema bado Kamati yake inaendelea kukumbwa na changamoto kubwa ya upatikanaji wa fedha zitakazokidhi mahitaji ya gharama za Maandalizi hayo pamoja na Kambi ya Vijana walioteuliwa kujiandaa na mashindano hayo.
Wakitoa Mawazo yao Baadhi ya Mawaziri walioshiriki Kikao hicho waliishauri Kamati ya Maandalizi hayo kuzingatia tarehe halisi ya ufunguzi wa Mashindano hayo ambayo inaingiliana na sherehe za Uhuru wa Tanzania Bara zinazofikia kilele chake Tarehe Tisa Disemba.
Mawaziri hao walisema Viongozi wengi wa Kitaifa wakiwemo wale wanaotarajiwa kuteuliwa kuwa Wageni rasmi katika Mashindano hayo wanatarajiwa kushiriki Maadhimisho hayo kitendo ambacho kama Kamati hiyo haikuzingatia mabadiliko ya Tarehe, ushiriki wa Viongozi hao utakosekana.
Hata hivyo Mawaziri hao walisema kufanyika kwa Mashindano ya Michezo ya Watu Wenye Ulemavu Visiwani Zanzibar ni muhimu kutokana na vugu vugu lake linalotoa taswira ya uwepo wageni wengi ambao kwa upande mwengine husaidia kuimarika kwa Sekta ya Utalii.
Akitoa nasaha zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alivipongeza Vyama vinavyosimamia michezo mbali mbali hasa kile cha Watu wenye ulemavu kwa juhudi vinavyochukuwa katika kusaidia uimarishaji wa Sekta ya Michezo Nchini.
Balozi Seif alisema juhudi hizo kwa kiasi Fulani zimeonyesha mwanga wa kuunga mkono jitihada za Serikali kupitia Wizara inayosimamia Michezo za kurejesha vugu vugu la Michezo Visiwani Zanzibar katika azma yake ya kuirejeshea hadhi yake ya Kimataifa iliyofifia kwa miaka mingi iliyopita.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
15/11/2017.
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni
(
Atom
)
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni