.

.

.

.

.

.

.

.
KARIBUNI TUHABARIKE, TUELIMISHANE, TUPEANE HABARI ZA KUKUFANYA UTABASAMU KIDOGO NA MATUKIO YALIYOFANYIWA UCHUNGUZI WA KINA TOKA KILA PEMBE CONTACTS: +255 787 377 722 Email: drweyunga@gmail.com PIA UNAWEZA KUNI FOLLOW KUPITIA INSTAGRAM YANGU @drweyunga | TANGAZA NASI ILI UWAFIKIE WATU WENGI ZAIDI.

Jumatano, 8 Novemba 2017

SMZ YASAINI MKATABA NA KAMPUNI YA UJENZI YA CHINA KUJENGA BARABARA NNE ZA UNGUJA

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar leo imetiliana saini Mkataba wa Ujenzi wa Barabara Nne za Bububu- Mahonda- Mkokotoni, Pale Kiongele, Matemwe – Muyuni na Fujoni – Kombeni zinazotarajiwa kuwa na urefu wa Kilomita 52.

Mkataba huo uliofanyika katika Ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kaskazini “A” uliopo Mkokotoni ulishuhudiwa na Viongozi mbali mbali wa Serikali na Kisiasa wakiongozwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi.

Upande wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Saini ilitiwa na Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji Nd. Mustafa Aboud Jumbe wakati ule wa Kampuni ya Kimataifa ya Uhandisi wa Ujenzi ya China { CCECC } inayojenga Bara bara hizo ulitiwa na Mkurugenzi wa Kampuni hiyo Nchini Tanzania Bwana Jiang Yi Giao.

Ujenzi wa Mradi huo wa Bara bara ambao ni utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya Mwaka 2015 -2020 unagharamiwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Mkopo nafuu wa fedha wa Shilingi Bilioni 58 kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika { ADB }.

Akizungumza mara baada ya utiaji saini Mkataba huo wa Ujenzi wa Bara bara Nne za Unguja Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar isingependa kuona inaingia katika migogoro na Wajenzi wa Miradi tofauti.

Balozi Seif alisema zipo Kampuni zilizowahi kutiliana saini Mikataba ya Ujenzi wa Miundombinu ya Bara bara na hatimae Kampuni hizo zikaingia mitini na kushindwa kukamilisha Mikataba ya Miradi waliyoikubali.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwataka Wananchi watakaohusika na maeneo yatakayopita Miradi hiyo ya Bara bara wasaidie kuharakisha Miradi hiyo ili imalizike kwa wakati uliopangwa.

Alisema changamoto za ulipaji wa fidia za Majengo pamoja na vipando vya Wananchi kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya Mradi huo isiwe vikwazo vya kuviza mpango wa Maendeleo uliokusudiwa kufanywa na Taifa.

Mapema Kaimu Mkuu wa Mkoa Kaskazini Unguja ambae pia ni Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Mh. Ayoub Mohamed Mahmoud alisema Mradi huo wa Bara bara utahudumia watu wote bila ya ubaguzi au itikadi za Kisiasa.

Hivyo Mh. Ayoub alionya kwamba Mtu au kikundi chochote kitakachojaribu kuzuia kuendelea kwa miradi hiyo Serikali haitosita kumchukuliua hatua zinazofaa za kinidhamu.

Alisema ni vyema kwa Wananchi wawe tayari kuipokea miradi hiyo sambamba na kushirikiana na Serikali pamoja na Wajenzi wa Mradi huo ili kuhakikisha inafanikiwa na kuleta tija kwa Jamii yote Nchini.

Naye Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji Zanzibar Balozi Ali Karume alisema kuimarika kwa Miundombinu ya Bara bara Nchini ni chachu ya Maendeleo kwa Taifa.

Balozi Karume alisema usumbufu wa usafiri kwa Wananchi wanaoishi katika maeneo utakayopita Mradi huo unatarajiwa kuwa Historia baada ya kukamilika kwa ujenzi wa Bara bara hizo.

Waziri wa Ujenzi, Miundombinu na Usafirishaji aliwaomba Wajenzi wa Mradi huo kutoka Kampuni ya Kimataifa ya Uhandisi wa Ujenzi ya China { CCECC } kuhakikisha kwamba mradi huo unakamilika kwa wakati uliomo kwenye Mkataba wa Ujenzi.

Akitoa salamu za Kampuni ya Kimataifa ya Uhandisi wa Ujenzi ya China { CCECC } Mkurugenzi wa Kampuni hiyo Tawi la Tanzania Bwana Jiang Yi Giao aliihakikishia Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwamba Utaalamu na uzoefu iliyonayo Kampuni hiyo ndio shahada inayothibitsha wazi kwamba kazi za Taasisi hiyo zinafanywa kwa sheria na Taratibu zilizopo.

Bwana Jiang alisema Kampuni ya CCECC iliyoasisiwa mnamo mwaka 1979 tayari ina uzoefu mkubwa uliopelekea kuwa miongoni mwa Makampuni ya Kimataifa ya Uhandisi wa Ujenzi 100 yaliyopo Duniani.

Alisema Kapuni hiyo ya ujenzi imeshakuwa maarufu Duniani likiwemo Bara la Afrika ambapo Miradi mbali mbali imeshajenga ikiwemo Reli ya Tanzania na Zambia, Bara bara na Madaraja ya kisasa katika Miji mingi Barani Afrika yakiwemo Majengo makubwa ya huduma za Jamii pamoja na Kijiji cha Kisasa Nchini Rwanda.

Bwana Jiang alifafanua kwamba CCECC pia imekuwa mstari wa mbele katika kusaidia miradi ya Kijamii kwa Wananchi wa Mataifa yanayofunga Mikataba ya Ujenzi wa Miradi tofauti ya Maendeleo na Kampuni hiyo.

Bara bara ya Bububu –Mahonda – Mkokotoni itajengwa na kupanuliwa upana wa Mita 8 wakati nyengine Tatu zilizobakia zitajengwa kwa upana wa Mita 6 chini ya usimamizi wa Taasisi ya Gauff kutoka Nchini Ujerumani.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
8/11/2017.
Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji Zanzibar wa kwanza kutoka kushoto Nd. Mustafa Aboud Jumbe na Mkurugenzi wa Kampuni ya Kimataifa ya Uhandisi wa Ujenzi ya China { CCECC } Bwana Jiang Yi Giao wakitia saini Mkatab wa ujenzi wa Bara bara Nne za Unguja hapo Ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kaskazini “A” Mkokotoni.
Nd. Mustafa Aboud Jumbe na Bwana Jiang Yi Giao wakibadilishana hati mara baada ya kutia saini Mktaba huo wa ujenzi wa bara bara za Unguja.
Mkurugenzi wa Kampuni ya Kimataifa ya Uhandisi wa Ujenzi ya China { CCECC } Bwana Jiang Yi Giao akiwasilisha salamu za Kampuni yake kwenye hafla ya kutia saini Mktaba huo wa ujenzi wa bara bara Nne za Unguja.
Balozi Seif akizungumza katika hafla ya kutia saini Mktaba huo wa ujenzi wa bara bara Nne za Unguja iliyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri ya Wilaya ya Kaskazini “A” hapo Mkokotoni.Kulia ya Balozi Seif ni Kaimu Mkuu wa Mkoa Kaskazini Unguja ambae pia ni Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Mh. Ayoub Muhamed Mahmoud na na Mkurugenzi wa Kampuni ya Kimataifa ya Uhandisi wa Ujenzi ya China { CCECC } Bwana Jiang Yi Giao.
Balozi Seif aliyepo kati kati walio kaa akiwa katika picha ya pamoja na Viongozi wa Serikali, Kisiasa na Wahandisi wa Ujenzi wa Bara bara Nne za Unguja kutoka Kampuni ya CCECC ya China mara baada ya utiaji saini Mkataba wa Ujenzi wa Bara bara hizo.
Balozi Seif akiagana na Mkurugenzi wa Kampuni ya Kimataifa ya Uhandisi wa Ujenzi ya China { CCECC } Bwana Jiang Yi Giao mara baada ya hafla ya utiaji saini Mkataba wa Ujenzi wa Bara bara Nne za Unguja.

Wa kwanza kulia ni Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Ushafirishaji Zanzibar Nd. Mustafa Aboud Jumbe, wa kwanza kutoka kushoto ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa Kaskazini Unaguja Nd. Haji Juma Haji na Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Ushafirishaji Zanzibar Balozi Ali Karume.

                                                                                             Picha na – OPMR – ZNZ.

Hakuna maoni :

Chapisha Maoni