Mwenyekiti wa Halmashauri ya Sherehe na Maadhimisho ya Kitaifa ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar wa kwanza Kulia akikiongoza Kikao cha Halmashauri hiyo kilichokutana katika Jengo la Makumbusho ya Kifalme Forodhani Mjini Zanzibar.
Picha na – OMPR – ZNZ.
Jumla ya Miradi 49 ya Kiuchumi, Maendeleo na Ustawi wa Jamii inatarajiwa kuzinduliwa na kuwekewa Mawe ya Msingi ndani ya Kumi la shamra shamra za maadhimisho ya Sherehe za kutimia Miaka 54 ya Mapinduzi ya Zanzibar ya Mwaka 1964.
Miongoni mwa Miradi hiyo 33 inazinduliwa rasmi baada ya kukamilika kwake wakati miradi 16 inatarajiwa kuwekewa Mawe ya msingi ikijumuisha pamoja na ile ya Taasisi za Umma, miradi ya Jamii sambamba na miradi ya Wawekezaji vitega uchumi.
Hayo yalibainika wakati wa Kikao cha Halmashauri ya Sherehe na Maadhimisho ya Kitaifa kilichokutana chini ya Mwenyekiti wake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi na kufanyika katika Jengo la Makumbusho Kifalme liliopo Forodhani Mjini Zanzibar.
Wajumbe wa Kikao hicho cha Halmashauri ya Sherehe na Maadhimisho ya Kitaifa katika majadiliano yao walifikia maamuzi ya kuipunguza Miradi Mitatu iliyoainishwa kuingizwa katika ratiba ya sherehe hizo baada ya kubaini kutofikia kiwango kinachokubalika katika uzinduzi pamoja na kuwekewa Mawe ya Msingi.
Hata hivyo Baadhi ya Wajumbe wa Kikao hicho walipendekeza kubadilishwa kwa nyakati na siku za uzinduzi na uwekaji wa mawe ya msingi kwa kuzingatia ratiba za viongozi Wakuu kuepuka kusafiri zaidi ya mara moja wakati wanaposhiriki katika matukio mbali mbali ndani ya Kumi hilo la Sherehe.
Naye Kaimu Kamanda wa Brigedia Nyuki Kanali Said Khamis Said alisema kutakuwa na mabadiliko kidogo ya Gwaride la Mwaka huu kutokana na Siku ya kilele cha sherehe za maadhimisho ya kutimia Miaka 54 ya Mapinduzi ya Zanzibar kuangukia Ijumaa.
Kanali Said alisema siku hiyo imezingatiwa vyema na Kamati ya Sekriterieti ya Halmashauri ya Sherehe na Maadhimisho ya Kitaifa ili kuwapa fursa Wananchi kumaliza mapema sherehe hizo kwa lengo la kujiandaa na ibada ya Sala ya Ijumaa.
Mapema Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Dr. Idriss Muslim Hijja alisema miradi yote iliyopendekezwa kuingizwa katika maadhimisho ya Sherehe za Mapinduzi ya Zanzibar Mwaka huu imefuatiliwa na kutolewa Taarifa kwa Sekriterieti ya Halmashauri ya Sherehe na Maadhimisho ya Kitaifa.
Dr. Hijja alisema yapo marekebisho yaliyofanywa na Kamati hiyo katika kupembua miradi inayostahiki kuingizwa ndani ya ratiba ya sherehe na kufikia maamuzi ya kuitoa ile miradi iliyoshindwa kufikia kiwango kinachohitajika kuingizwa kwenye mtiririko huo.
Katika uzinduzi na uwekaji wa Mawe ya msingi ya miradi iliyomo ndani ya sherehe hizo Viongozi wa Kitaifa wa Serikali zote mbili wamejumuishwa katika ratiba hizo wakiwemo Marais, Mawaziri pamoja na Viongozi wastaafu wa pande zote mbili.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni