WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amewanusuru viongozi 19 wa vyama vikuu vya ushirika vya mikoa ya
Shinyanga (SHIRECU) na Mwanza (NCU) kwenda selo na badala yake
amewapa siku 23 wampe maelezo yatakayomridhisha juu ya mahali zilipo
mali za vyama hivyo viwili.
Amefikia uamuzi huo leo (Ijumaa,
Desemba 22, 2017) wakati akifunga kikao cha siku moja cha wadau wa
zao la pamba alichokiitisha mkoani Shinyanga. Viongozi hao
wanatuhumiwa kwa upotevu wa mali zilizokuwa zikimilikiwa na vyama
hivyo vya ushirika.
“Nataka kila mtu akaandae taarifa
kuhusu mali za ushirika zilipo, au zimeenda wapi na kama mlizikopea,
mseme ni wapi, lini na kwa ridhaa ya nani. Nataka maelezo ya kutosha
kuniridhisha mali za ushirika zimeenda wapi,” alisema Waziri Mkuu.
“Hawa nitakaowataja walipaswa
kuchukuliwa na RPC, wakatoe maelezo yao na hatua dhidi yao
zichukuliwe. Sasa nataka nikutane nao Dodoma ifikapo Januari 15, 2018
saa 3:30 asubuhi ofisini kwangu,” alisisitiza.
Kuhusu tuhuma za viongozi wa Chama
Kikuu cha Ushirika Mkoa wa Mwanza (Nyanza Cooperative Union - NCU),
Waziri Mkuu alisema chama hicho kati ya mwaka 2001 na 2017, kilikuwa
jumla ya mali 10 ambazo ziliuzwa kinyemela katika mazingira yenye
utata na kwa bei ndogo ikilinganishwa na thamani halisi ya mali hizo
zilizopo jijini Mwanza.
Aliwataja viongozi waliohusika na
upotevu huo ambao wanatakiwa kutoa maelezo yao kuwa ni Murtazar
Alloo ambaye ni mnunuzi wa maghala matatu mali ya NCU, Bw. Samson
Ng’halida (mnunuzi wa New Era Oil Mills), Bw. Amos Njite Lili
(mnunuzi wa ghala la Igogo), Bi. Antonia Zacharia (mnunuzi wa jengo
la KAUMA), Bw. Timothy Kilumile (mnunuzi wa jengo la KAUMA), Bw.
Robert Kisena (mnunuzi wa pili wa New Era Oil Mills), Bw. Peter
Ng’hingi (aliyekuwa Mjumbe wa Bodi), Bw. Daniel Lugwisha (aliyekuwa
Mhasibu Mkuu - NCU), Bw. George Makungwi (aliyekuwa Afisa Miliki -
NCU) na Bw. Sospeter Ndoli (aliyekuwa Afisa Utumishi -NCU).
Kuhusu mali za Nyanza
zinazoshikiliwa na benki ya CRDB. Waziri Mkuu alisema benki hiyo
inaidai NCU mikopo yenye thamani ya sh. bilioni 2.123 na kwamba benki
hiyo inashikilia mali 16 zenye thamani ya sh. bilioni 18.132. Alitaka
vyombo vya dola vifanye uchunguzi ili kubaini uwiano wa mikopo na
mali zinazoshikiliwa na benki ya CRDB.
Kwa upande wa viongozi wa SHIRECU,
Waziri Mkuu alisema wanatuhumiwa kwa upotevu wa zaidi ya sh. bilioni
11 ambazo wanadaiwa na benki ya TIB yakiwemo madeni ya mishahara ya
watumishi ambayo yanafikia sh. bilioni 1.2.
“SHIRECU kwa sasa haina mali
zozote kwa sababu mali zote zinashikiliwa na TIB kutokana na mikopo,”
alisema.
Aliwataja viongozi wa SHIRECU ambao
wanatakiwa kutoa maelezo yao kuwa ni Bw. Joseph Mihangwa (Meneja
Mkuu), Bw. Sillu Mbogo (Kaimu Mhasibu Mkuu), Bw. Maduhu Nkamakazi
(Kaimu Mkaguzi wa Ndani), Bw. James Kusekwa (Kaimu Meneja Uendeshaji)
na wajumbe wa Bodi ya SHIRECU.
Wajumbe hao wa Bodi ni Bw. Robert
Mayongela (Mwenyekiti), Bi. Mary Mabuga (Makamu Mwenyekiti), Bw. Sigu
Maganda (Mjumbe), Bw. Clement Bujiku (Mjumbe) na Bw. Charles Lujiga.
Waziri Mkuu ambaye aliwasili mkoani
humo leo asubuhi, alikwenda kwanza kukagua kiwanda cha kutengeneza
nyuzi cha JOC na kisha kurejea ukumbini kuendelea na kikao cha wadau
wa pamba ambacho kimeshirikisha wakuu wa mikoa 16, wabunge, ma-RAS,
wakuu wa wilaya, wakulima, wanunuzi wa pamba na wenye viwanda.
Waziri Mkuu ameondoka Shinyanga
kuelekea Ruvuma ambako atakuwa na ziara ya siku moja.
(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
IJUMAA, DESEMBA 22, 2017
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni