Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema muelekeo wa kuanzishwa kwa Miradi ya Uwekezaji katika maeneo huru ya Kiuchumi unaoshirikisha Wawekezaji kutoka China una lengo la kuimarisha Uhusiano uliopo wa Kihistoria kati ya Zanzibar na China.
Alisema ipo miradi mingi ya Kiuchumi na Maendeleo ambayo tayari imeshaanzishwa kupitia msukumo wa Serikali ya China jambo ambalo linathibitisha uhusiano huo wa muda mrefu ulioasisiwa mara tu baada ya Mapinduzi ya Zanziubar ya Mwaka 1964.
Balozi Seif alitoa kauli hiyo wakati wa mazungumzo yake na Ujumbe wa Wawekezaji kutoka Jamuhuri ya Watu wa China katika Jimbo la Jangsu uliongozwa na Bwana Ge Zhi Yong.
Alisema ujio wa Ujumbe huo wa Wawekezaji kutoka Jimbo la Jangsu ni kigezo kinachotoa shauku kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupata kuungwa mkono azma yake ya kuimarisha Sekta za Uchumi.
Balozi Seif aliuelezea Ujumbe huo kwamba Serikali zote mbili Nchini Tanzania hivi sasa zimejielekeza katika Kuona Tanzania inaingia katika Uchumi wa Viwanda miaka michache ijayo ili kutoa fursa zaidi za ajira kwa Vijana walio wengi.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliupongeza Uongozi wa Jimbo la Jangsu kwa uamuzi wake wa kuendelea kuiunga Mkono Zanzibar katika miradi mbali mbali ya Kiuchumi na Maendeleo ambayo huleta faraja na kupunguza ukali wa maisha kwa Wananchi walio wengi Nchini.
Balozi Seif aliushauri Ujumbe huo utakaporejea China uwe balozi wa kuitangaza Zanzibar kwa Wawekezaji wa Taifa hilo Kubwa Barani Asia kwa vile tayari imeshafungua milango ya uwekezaji hasa katika Sekta ya Utalii.
Mapema Kiongozi wa Ujumbe huo wa Wawekezaji kutoka Jimbo la Jangsu Nchini Jamuhuri ya Watu wa China Bwana Ge Zhi Yong alisema Wawekezaji wa Sekta ya Uhandisi na Viwanda wa Jimbo hiyo wameonyesha nia ya kutaka kuwekeza miradi yao Nchini Tanzania.
Bwana Ge Zhi Yong alisema wakati wanajiandaa na maandalizi ya ujenzi wa Kiwanda cha Saruji Mkoani Tanga taratibu zinaandaliwa katika kulitumia soko la Zanzibar katika uuzaji wa biadhaa hiyo hapo baadae.
Alisema fursa za uwekezaji Nchini Tanzania zimetoa fursa kwa Wawekezaji wa Jimbo lake kuleta wataalamu wa mfumo wa maji Taka katika kuifanya Miji ya Tanzania inakuwa katika mazingira bora kimtazamo.
Bwana Ge Zhi Yong alimueleza Balozi Seif kwamba miradi hiyo inatarajiwa kwenda sambamba na muelekeo wa uanzishwaji wa biashara za ndani pamoja na vifaa vya ujenzi.
Akitoa Taarifa ya ujio wa Viongozi hao kutoka Jimnbo la Jangsu Nchini China Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Mh. Ayoub Mohamed Mahmoud alisema Uumbe huo umekuja Nchini Tanzania chini ya wenyeaji wake Mkoa wa Dar es salaam.
Mh. Ayoub alisema mahusiano mazuri ya ujirani mwema uliopo kati ya Mkoa wa Dar es salaam na Mjini Magharibi yamepelekea Ujumbe huo kufanya ziara maalum Mkoa Mjini Magharibi kwa lengo la kuendeleza Ushirikiano uliopo.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni
(
Atom
)
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni