.

.

.

.

.

.

.

.
KARIBUNI TUHABARIKE, TUELIMISHANE, TUPEANE HABARI ZA KUKUFANYA UTABASAMU KIDOGO NA MATUKIO YALIYOFANYIWA UCHUNGUZI WA KINA TOKA KILA PEMBE CONTACTS: +255 787 377 722 Email: drweyunga@gmail.com PIA UNAWEZA KUNI FOLLOW KUPITIA INSTAGRAM YANGU @drweyunga | TANGAZA NASI ILI UWAFIKIE WATU WENGI ZAIDI.

Jumamosi, 20 Januari 2018

BALOZI SEIF AONGOZA KISOMO CHA HITMA, DUA YA PAMOJA KUWAREHEMU WANAJESHI 10 WA TANZANIA WALIOUAWA DRC

Waumini na Wananchi kutoka maeneo mbali mbali wakisoma Hitma na Dua ya kuwarehemu Askari wa WJTZ waliouawa Nchini Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Congo wakiwa katika Ulinzi wa Amani chini ya Umoja wa Mataifa hapo katika Msikiti wa Noor Muhammad Kwamchina.
  Baadhi ya Viongozi waliohudhuria Hitma ya kuwaombea Dua Wanajeshi wa Tanzania waliouawa Mnamo Tarehe 7/12/2017 Nchini Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Congo. Wa kwanza kutoka Kushoto ni Naibu Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Hassan, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Dr. Hussein Mwinyi, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi na Mwenyekiti wa Kamati ya Amani ya Kitaifa Sheikh Salim Mohammed Al – Kadiri.
Balozi Seif akitoa nasaha kwenye kilele cha cha Hitma ya Kuwaombe Dua Wanajeshi wa Tanzania waliouawa Nchini DRC hapo katika Msikiti wa Noor Muhammad.
Balozi Seif akizungumza na vyombo vya Habari mara baada ya kuhudhuria Hitna na Dua ya kuwarehemu Askari wa JWTZ waliouawa Nchini DRC wakati wakilinda amani. Picha na – OMPR – ZNZ.

Waumini wa Dini ya Kiislamu, Wananchi, Askari wa Vikosi vya Ulinzni na Usalama Nchini pamoja na Ndugu na wana Familia leo wameungana katika Kisomo cha Hitma, Dua ya pamoja na Arubaini kwa ajili ya kuwarehemu Wanajeshi 10 wa Tanzania waliouawa wakati wakilinda Amani Nchini Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Congo {DRC}. 

Jeshi la Wananchi wa Tanzania {JWTZ} limepoteza Vijana wake hao mashujaa na walinzi wa Taifa waliouawa wakati wakitekeleza jukumu lao walilokabidhiwa na Umoja wa Mataifa la kusimamia ulinzi wa Amani Nchi ya DRC baada ya kuvamiwa ghafla na Waasi wa Nchi hiyo.

Kisomo cha Hitma na Dua hiyo ya pamoja kimefanyika katika Msikiti wa Ijumaa wa Noor Muhammad uliopo Mtaa wa Kwamchina Mombasa na kushirikisha pia Viongozi wa Serikali zote Mbili Wanasiasa wakiongozwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi.

Tukio hilo la kusikitisha la kuuawa kwa Askari wa JWTZ lililogusa nyoyo za Watanzania wote pamoja na Walimwengu wapenda Amani limeacha msiba, simanzi, huzuni pamoja na majonzi makubwa hasa kwa Wana familia wa Vijana hao.

Akitoa nasaha mara baada ya Kisomo hicho Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Saeif Ali Iddi alisema upo umuhimu mkubwa kwa Jamii kuendelea kuwa na moyo wa subra wakati wanapopatwa na mitihani ili wazidi kuishi kwa Imani, Ushirikiano na upendo zaidi.

Balozi Seif alisema Muumba wa Dunia na vilivyomo ndani yake ambae ni Mwenyezi Muungu tayari ameshawabashiria mema na ya kheir wale wote waja wake walioamini na kupatwa na misiba na wakaamua kurejea kwake.

Alisema Mkusanyiko wa Waumini na Wananchi katika kisomo hicho ulioweka pamoja waumini waliotoka Miji tofauti na Itikadi mbali mbali za Kisiasa pamoja na madhehebu ya Dini ni dalili tosha ya kuonyesha mshikamano wa Jamii aliouamrisha Mwenyezi Muungu.

Balozi Seif alieleza kwamba mahudhurio hayo ni kielelezo cha jinsi Taifa na Wananchi wake walivyoguswa na tukio hilo la msiba wa kuondokewa na wapenzi wao ambalo imani inaonyesha wazi kwamba halitosahaulika milele katika mioyo yao.

Makamu wa Pili wa Raiswa Zanzibar aliishukuru Kamati ya Amani ya Kitaifa Zanzibar kwa jinsi inavyobuni mambo kadhaa yenye maslahi kwa Taifa likiwemo hilo la mkusanyiko huo wa ubunifu wa kuandaa dua hiyo ambalo ni jambo na kupongezwa.

Balozi Seif alielezea matarajio yake kwamba Kamati ya Amani ya Kitaifa Zanzibar itaendelea na jitihada zake za kuwaweka pamoja Waumini wa Dini mbali mbali na kuahidi kwamba Serikali Kuu itahakikisha kwamba inaunga mkono na kuisaidia Kamati hiyo katika kutekeleza jukumu lake.

Aliwaomba Viongozi na Watendaji wa Kamati hiyo waendelee kuongeza jitihada katika mapambano yao dhidi ya vitendo vya mapenzi ya Jinsia Moja, Ubakaji, Udhalilishaji wa Wananwake na Watoto pamoja na mambo mbali mbali yasiyo na maslahi kwa Taifa hili.

Akitoa salamu Mwakilishi wa Familia za Wafiwa wa Wanajeshi hao wa JWTZ Bwana Haji Hassan kwa niaba ya Familia hizo aliwashukuru Watanzania wote walioshirikiana na wafiwa hao katika msiba huo mkubwa.

Bwana Haji Hassan alisema msiba wa Wanajeshi hao 10 uliotokea Mnamo Tarehe 7 Disemba Mwaka 2017 Nchini Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo {DRC} ulikuwa wa Taifa zima jambo ambalo lilileta faraja kwa wana familia hao.

Kwa upande wake Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. Hussein Mwinyi alisema kitendo cha Wananchi wa Zanzibar kupitia Kamati ya Amani ya Taifa cha kusoma Hitma kwa ajili ya kuwarehemu Mashujaa waliopoteza rohozao Nchini DRC kimepokelewa kwa heshima yote na Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.

Dr. Hussein alisema Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa imewajibika na kutekeleza wajibu wake wote wa kuhakikisha Mashujaa hao wameletwa salama Nchini Tanzania baada ya kuuawa wakati wakitetea haki na heshima ya Wanaadamu wenzao wanaoendelea kudhalilika kutokana na vituko vya Waasi Nchini DRC.

Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kwa niaba ya Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania aliendelea kuwapa pole Wafiwa wote kutokana na msiba huo mzito uliogusa kila nyoyo ya Raia wa Taifa hili.

Akimkaribisha Mgeni rasmi kuwaaidhi Waumini walioshiriki Kisomo hicho Mwenyekiti wa Kamati ya Amani ya Kitaifa Sheikh Salim Mohammed Al – Kadir alisema Kamati hiyo imeguswa na Msiba huo uliopelekea Uongozi wa Kamati hiyo kuandaa dua hiyo ili kuonyesha mapenzi kwa Wapiganaji hao.

Sheikh Salim kwa niaba ya Uongozi wa Kamati yake wameishukuru Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa pamoja na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa ushirikiano uloipa Kamati hiyo kuweza kutekeleza majukumu yake iliyopangiwa na Umma.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
20/1/2018.

Hakuna maoni :

Chapisha Maoni