Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa
na Michezo Ndugu Dr. Harrison Mwakyembe, Leo Jumamosi Januari 20,
2018 ameitembelea timu ya Taifa ya Vijana chini ya miaka 16 Serengeti
Boys iliyopo kambini kwenye hostel za Makao Makuu ya Shirikisho la
Mpira wa Miguu Tanzania TFF na kuwaachia ujumbe wa Serikali.
Dr. Mwakyembe akitoa salamu za
Serikali amewaambia Vijana wanaounda timu hiyo kuwa serikali
inawaamini na wanalo jukumu la kuiperusha vyema bendera ya Tanzania.
Amewataka kupambana kwaajili ya
Tanzania na kuhakikisha wanafanya vyema kwenye kila mashindano huku
akiwataka makocha wa kikosi hicho kuwapa mafunzo mazuri kwa ustawi wa
Vijana hao.
Aidha Dr. Mwakyembe amesema anaamini
Vijana hao watakuwa bora chini ya TFF iliyopo madarakani inayoongozwa
na Rais Ndugu Wallace Karia.
"Naamini mtaimarika na kuwa
bora maana hata TFF hii sasa ina ari na morali kubwa".Alisema
Dr. Mwakyembe.
Katika ziara yake hiyo Dr. Mwakyembe
alipata nafasi ya kutazama mchezo wa kirafiki kati ya Serengeti Boys
na Makongo Sekondari iliyomalizika kwa Serengeti Boys kupata ushindi
wa mabao 4-1.
Kabla ya mchezo huo Serengeti Boys
walicheza mchezo mwingine wa kirafiki dhidi ya Kituo cha Bombom
iliyomalizika kwa sare ya kufungana bao 1-1.
IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA
MIGUU TANZANIA TFF
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni