WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekagua
shamba la uzalishaji wa mbegu bora za mihogo aina ya mkombozi
linalomilikiwa na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kikosi cha Rwamkoma
wilayani Butiama.
Amekagua shamba hilo linalomilikiwa
na Kikosi cha JKT Rwamkoma leo (Jumamosi, Januari 20, 2018)
alipowasili wilayani Butiama akiwa katika ziara ya kikazi mkoani
Mara. Kikosi hicho kimewezeshwa na Halmashauri ya Butihama.
Waziri Mkuu amewakipongeza kikosi
cha JKT Rwamkoma kwa uamuzi huo wa kuzalisha mbegu bora za mihogo
ambazo baadae zitasambazwa kwa wakulima wa zao hilo wilayani hapa.
Pia amewataka wakazi wanaoishi
karibu na shamba la kikosi hicho hilo kulitumia kama shamba darasa
kwa ajili ya kujifunza namna bora ya kulima zao hilo.
Kwa upande wake Mkuu wa Kikosi hicho
Luteni Kanali David Msakulo alisema shamba hilo linaukubwa wa ekari
60, na mbegu zitakazozalishwa zitatosha kupanda ekari 900.
Mkuu huyo wa kikosi hicho aliongeza
kuwa mbegu hizo zinazozalishwa katika shamba hilo zitagawanywa kwa
wakulima katika kata zote 18 za wilaya ya Butihama.
Alisema mbali ya kuzalisha mbegu pia
wanatarajia kuanzisha kiwanda cha kuchakata zao la mihogo ili kuweza
kuliongezea thamani.
Mbali na shamba la mbegu bora za
mihogo pia kikosi hicho kina shamba lingine la pamba lenye ukubwa wa
ekari 57, ambapo wanatarajia kuvuna tani 57 za pamba. Mwakani
wanatarajia kuongeza ukubwa wa shamba na kufikia ekari 300.
Awali, Waziri Mkuu alitembelea
shamba darasa la mkoa wa Mara la zao la pamba lililopo Kisangwa
wilayani Bunda akiwa njiani kuelekea wilayani Butihama, kuendelea na
ziara yake ya kikazi mkoani Mara.
Mkuu wa Mkoa wa Mara, Bw. Adam
Malima alisema shamba darasa hilo ni moja ya jitihada za Mkoa wa Mara
kuelimisha wakulima wa zao hilo mbinu bora za uzalishaji ili kuongeza
tija katika uzalishaji.
(mwisho)
IMETOLEWA NA:
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni