Makamu Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi nchini (TPSF), Bw. Salum Shamte, akizungumza wakati wa mkutano wa tatu kati ya Sekta Binafsi na Sekta ya Umma uliojadili namna ya kuboresha masuala ya biashara na uwekezaji nchini, mjini Dodoma.
Baadhi ya Wawekezaji na wageni
kutoka Taasisi za Kimataifa walioshiriki Mkutano wa tatu wa
majadiliano kati ya wadau wa Sekta Binafsi na Sekta ya Umma
uliofanyika mjini Dodoma.
Baadhi ya Wafanyabiashara na
Wawekezaji walioshiriki Mkutano wa tatu wa majadiliano kati ya wadau
wa Sekta Binafsi na Sekta ya Umma uliofanyika mjini Dodoma.
Baadhi ya Manaibu Mawaziri, Makatibu
Wakuu na Manaibu Makatibu Wakuu na Maafisa wengine kutoka Wizara
mbalimbali wakifuatilia mkutano kati ya Sekta Binafsi na Sekta ya
Umma, Mjini Dodoma.
Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt.
Philip Isdor Mpango (Mb) akifungua mkutano wa tatu kati ya Sekta
Binafsi na Serikali uliofanyika mjini Dodoma.
Na Benny Mwaipaja, WFM, Dodoma
Sekta Binafsi nchini imekiri kuwa
uhusiano kati yake na Serikali umezidi kuimarika kutokana na
kuboreshwa kwa mazingira ya uwekezaji na ufanyajibiashara hapa nchini
kuliko ilivyokuwa hapo awali na kwamba hatua hiyo itachochea ukuaji
wa uchumi wa nchi.
Kauli hiyo imetolewa mjini Dodoma na
Makamu Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi nchini (TPSF), Bw.
Salum Shamte, wakati wa mkutano wa tatu kati ya Sekta Binafsi na
Sekta ya Umma uliojadili namna ya kukuza ushiriki wa Sekta Binafsi
katika kukuza uchumi wa viwanda nchini.
"Sekta binafsi imenituma kuleta
pongezi kwa Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kwa kutekeleza kwa
vitendo utambuzi wa kwamba Sekta Binafsi ni mbia muhimu wa maendeleo
ya Taifa letu" alisema Bw. Shamte.
Aliyataja baadhi ya mafanikio yanayo
onekana bayana kuwa ni pamoja na kuinusuru Bandari ya Dar es Salaam
kwa mabadiliko ya sheria ya fedha ya mwaka 2017 hasa kuondoa VAT
kwenye biashara ya mizigo ya kimataifa na kuondokana na umoja wa
forodha ambao ulipunguza kwa kiasi kikubwa kiwango cha biashara kati
ya Tanzania na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Bw. Shamte alisema kuwa majadiliano
hayo kati ya Serikali na Sekta Binafsi kumeikoa sekta ya utalii hasa
kwa kuondokana na kodi ya ongezeko la thamani (VAT) kwenye leseni
mbalimbali hatua ambayo imerejesha msisimko wa sekta hiyo.
"Serikali imepunguza pia
mlolongo wa kodi kwa wakulima, japokuwa - kazi haijakamilika lakini
mwanzo ni mzuri" aliongeza Bw. Shamte
Alieleza kuwa jitihada mpya na nzuri
za kutatua changamoto za kodi kwa kampuni zinazojihusisha na biashara
kati ya Tanzania Bara na Visiwani, na kuanza kufanya malipo kwa
wakandarasi na watoa huduma wa ndani hatua ambayo wanaamini itakuza
matumizi ya ndani na mzunguko wa fedha.
Makamu mwenyekiti huyo wa TPSF
alisema kuwa Serikali ya Awamu ya Tano ni sikivu na kwamba kwa mara
ya kwanza, wanatarajia kushuhudia Bajeti Kuu ya Serikali ya mwaka
2018/2019 ikiwa bora zaidi kwa kubeba mapendekezo yao mengi
yatakayosaidia kukuza sekta hiyo na pia kuboresha masuala ya kodi na
mapato ya Serikali.
Wakizungumza kwenye mkutano huo,
Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango, na Waziri wa Viwanda,
Biashara na Uwekezaji Bw. Charles Mwijage, wamesema kuwa Serikali
inathamini mchango wa Sekta Binafsi katika maendeleo ya uchumi wa
viwanda na kwamba itaendelea kutatua changamoto mbalimbali
zinazoikabili Sekta hiyo ikiwemo masuala ya kodi.
"Sekta Binafsi ndiyo mhimili wa
uchumi kwa hiyo ni muhimu tuhakikishe upande wa Serikali tunafanya
wajibu wetu kuiweesha Sekta hiyo iwe imara zaidi na iweze kukua kwa
sababu tutapata ajira, bidhaa bora na huduma mbalimbali hatimaye
kukuza uchumi wetu wa viwanda" alisisitiza Dkt. Mpango
Waziri wa Viwanda, Biashara na
Uwekezaji naye aliongeza kuwa Sekta Binafsi ndiyo itakayojenga
viwanda wakati Serikali itakuwa mwezeshaji ndio maana wameamua kukaa
pamoja kujadili changamoto zinazozikabili pande zote mbili na kwamba
baadae watajielekeza kujadili na kila Sekta ili kuharakisha maendeleo
ya kiuchumi.
Wametoa wito kwa Sekta binafsi
nchini kujenga uaminifu na kufuata sheria na kanuni za
ufanyajibiashara na uwekezaji nchini ikiwemo kulipa kodi stahiki.
Akizungumza katika mkutano huo wa
tatu uliojumuisha wadau mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi,
Mkurugenzi wa Shirika la Maendeleo la Marekani (USAID) hapa nchini,
Bw. Andy Karas, ameimwagia sifa Tanzania kwa kukuza uchumi wake kwa
wastani wa asilimia 7 na kushauri kuwa uchumi huo sasa uelekezwe
kutatua changamoto za wananchi hususan kukuza sekta ya kilimo inayoa
ajiri idadi kubwa ya watanzania.
Mwisho
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni