Kulia ya Balozi Seif aliyevaa shati ya Kijani ni Mwenyekiti wa Jumuiyua ya Wazazi Taifa Dr. Edmond Bernard Mdolwa.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Taifa Dr. Edmond Bernard Mdolwa akimuelezea Balozi Seif Mikakati ya Jumuiya hiyo katika kujikwamua kiuchumi na kujiendesha.
Picha na – OMPR – ZNZ.
Picha na – OMPR – ZNZ.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Chama cha Mapinduzi kinaamini kwamba nguvu na uhai wake utaendelea kupatikana kupitia Jumuiya zake zilizopewa jukumu la kusimamia kazi za Chama hicho katika utekelezaji wa Ilani na Sera zake.
Alisema Jumuiya za Chama ni muhimili wa chama chenyewe akiitaja ile ya Wazazi ambayo ndio kongwe zaidi inayotegemewa na Chama cha Mapinduzi katika kusaidia nguvu za Chama hicho.Balozi Seif Ali Iddi alitoa kauli hiyo wakati akizungumza na Uongozi Mpya wa Jumuiya ya Wazazi Taifa ukiongozwa na Mwenyekiti wake Dr. Edimond Bernard Mdolwa hapo katika Ukumbi wa Juu wa Jengo la Baraza la Wawakilishi Chukwani nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.
Alisema jitihada za Chama cha Mapinduzi katika kujenga nguvu zake husimamiwa na Jumuiya zake hasa katika harakati za Kampeni za uchaguzi zinazotokea Nchini sambamba na kuelezea mikakati ya mipango yake inayopaswa kuungwa mkono ya Wananchi walio wengi.
Balozi Seif ambae pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM alisema Wazazi ni jumuiya ya Watu wote wanaostahiki kuisaidia na kuipa msukumo katika kuendesha miradi yake ili iweze kujitegemea badala ya kusubiri kupata ruzuku kutoka Uongozi wa juu wa Chama hicho.
Aliutaka Uongozi wa Jumuiya ya Wazazi ujitahidi kubuni Miradi itakayoweza kusaidia kuiendesha Jumuiya hiyo pamoja na Chama chenyewe huku ikizingatia pia kuzifuatilia Skuli inazoziendesha kama bado zina nguvu za kusaidia kuwapatia Elimu Watoto hapa Nchini.
Balozi Seif aliuhakikishia Uongozi huo wa Jumuiya ya Wazazi Taifa kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kutoa msukumo kwa Taasisi hiyo ya Chama katika kutekeleza majukumu yake hasa lile la Usimamizi na Utekelezaji wa Sera na Ilani ya Uchaguzi ya Mwaka 2015/2020.
Mapema Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Taifa Dr. Edmond Bernard Mdolwa alisema Malengo ya Taasisi hiyo ya Chama cha Mapinduzi ambayo iliwahi kulega lega katika kipindi cha Miaka Mitano iliyopita na kufikia hatua ya kutaka kufutwa inakusudia kupitia katika njia ya kujitegemea ndani ya kipindi cha Miaka Miwili ijayo.
Dr. Mdolwa alimueleza Balozi Seif kwamba juhudi zilizochukuliwa na Uongozi wake kutokana na changamoto zilizoikumba Jumuiya hiyo zimeanza kutoa mwanga wa matumaini kiasi kwamba baadhi ya matatizo yaliyopo kwa sasa yanaendelea kupungua.
Alisema wakati watendaji na Viongozi wa Jumuiya hiyo wakijizatiti kutekeleza majukumu yao katika muelekeo wa kujitegemea aliuomba Uongozu wa Juu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuhakikisha kwamba inaiunga mkono katika muelekeo huo.
Dr. Mdolwa alisema ipo baadhi ya Miradi na vitega Uchumi vya Jumuiya ya Wazazi Visiwani Zanzibar ambavyo vinahitaji kupata nguvu za ziada katika uendeshaji wake hasa ile inayoendeshwa kwa Ubia.
Mwenyekiti huyo wa Jumuiya ya Wazazi Taifa alifahamisha kwamba Miradi ya Vitega Uchumi vya Taasisi hiyo vilivyopo Zanzibar Mapato yake yanaweza kuendesha Jumuiya pamoja na Mishahara ya Watendaji wake endapo itasimamiwa na kuendeshwa katika misingi inayostahiki Kibiashara.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
20/2/2018.
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni