Mohammed Dewji akizungumza na
wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambao wanafadhiliwa na
Taasisi ya Mo Dewji katika hafla ya kutangaza washindi wa mpango wa
ufadhili kwa wanafunzi wa elimu ya juu (Mo Scholars).
Taasisi ya Mo Dewji, Mohammed Dewji
akikabidhi zawadi kwa baadhi ya wanafunzi wa elimu ya juu waliopata
ufadhili kutoka katika taasisi hiyo kwa mwaka wa masomo 2017/2018
kupitia mpango wa Mo Scholars.
Baadhi ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambao wanafadhiliwa na
Taasisi ya Mo Dewji wakisikiliza kwa makini katika hafla ya kutangaza washindi wa mpango wa
ufadhili kwa wanafunzi wa elimu ya juu (Mo Scholars).
Taasisi ya Mo Dewji imetangaza
orodha ya wanafunzi 22 wa elimu ya juu waliopata ufadhili kutoka
katika taasisi hiyo kwa mwaka wa masomo 2017/2018 kupitia mpango wake
wa Mo Scholars.
Wanafunzi hao ni Neema Charles,
Winfrida Mrope, Henritha Rwegasira, Monica Ubushimbali, Suzana
Mkindi, Hamisa Selemani, Beatrice Shupa, Phoebe Mwankemwa, Amon
Abraham, Venance Makambe na Amos Ntandu.
Wengine ni Benjamin Mkondya, Ally
Mashaka, Amuniri Sebarua, Iddi Mbilinyi, Samwel Ponda, Eram Temu,
Busumilo Tumaini, Cosmadeus Mayunga, Amos Kashinje, Kelvin Ernest na
Barnaba Barnaba ambao wote ni wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam (UDSM).
Akizungumza kuhusu ufadhili huo,
Mwanzilishi wa Taasisi ya Mo Dewji, Mohammed Dewji aliwapongeza
washindi kwa kufanikiwa kupata ufadhili huo, lakini akiwataka
kujituma ili waweze kufikia malengo waliyojiwekea katika maisha yao.
“Mmepata ufadhili huu muutumie
vizuri, wapo wengi ambao walituma maombi lakini nyie mmefanikiwa
kupata ufadhili. Msome kwa bidii na baadae mpate kazi nzuri ambazo
zitawasaidia kupata kipato na kusaidia ukuaji wa uchumi wa nchi,”
alisema Dewji.
Dewji alisema aliamua kuanza kutoa
ufadhili kwa wanafunzi wa elimu ya juu ili kuunga mkono juhudi za
Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe
Magufuli ya kuhakikisha kila mtoto anapata elimu.
Aliongeza kuwa, dhamira yake ni
kuona Watanzania wengi wananufaika na mpango huo na amejipanga
kuhakikisha kuwa idadi ya wanufaika wa mpango wa ufadhili unaotolewa
na taasisi yake unaongezeka kila mwaka.
“Kasi yetu bado ni ndogo sana
kulinganisha na ninavyotaka. Wakati tunaanza kutoa ufadhili tuliamua
kuanza na wanafunzi 10 lakini mimi nataka tuwape ufadhili Watanzania
wengi ikiwezekana tufike hata 100. Kwangu ni jambo jema sana kusaidia
Watanzania wenzangu kwa sababu nimezaliwa hapa na nitazikwa hapa sina
pengine pa kwenda,” alisema Dewji.
Nae mmoja wa wanafunzi ambaye kabla
ya kupata ufadhili aliweka tangazo kwenye mtandao wa kijamii kwamba
anauza figo yake, Amos Ntandu aliishukuru Taasisi ya Mo Dewji kwa
ufadhili ambao imewapatia kwani baadhi yao waliokuwa wamepoteza
matumaini ya kuendelea na masomo, lakini pia kuomba uongozi wa
taasisi kuendelea kutoa ufadhili kwa Watanzania ili wapate elimu.
“Mimi nilikuwa tayari kuweka
maisha yangu hatarini kwa kutangaza kuuza figo langu, lakini ufadhili
huu mliotupatia umebadili maisha yetu. Idadi ya wanafunzi wanaokosa
mkopo ni kubwa hivyo nawaomba muwe na moyo wa kuendelea kuwasaidia
ili na wao wafikie ndoto zao,” alisema Ntandu.
Pamoja na kutangaza washindi hao,
pia taasisi hiyo ilitoa zawadi ya kompyuta mpakato (laptop) kwa
wanafunzi wa mwaka wa masomo 2016/2017 ambao inawafadhili waliofanya
vizuri katika masomo yao kwa mwaka wa kwanza chuoni.
Kwa sasa idadi ya wanafunzi ambao
wanapata ufadhili kutoka Taasisi ya Mo Dewji imefikia 30, ambapo kati
yao wanafunzi 7 ni wa mwaka wa masomo 2016/2017 na wanafunzi 22 mwaka
wa masomo 2017/2018.
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni