WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali imeweka mikakati ya kutosha itakayowezesha pamba yote inayolimwa nchini kununuliwa na tayari imeshaanza mchakato wa kutafuta masoko ya ndani na nje ya nchi.
Ametoa kauli hiyo leo (Alhamisi, Februari 8, 2018) Bungeni mjini Dodoma wakati akijibu swali la mbunge wa Sumve, Bw. Richard Ndassa wakati wa kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu.
Bw. Ndassa alitaka kujua Serikali imejipangaje kuwasaidia wananchi walioitikia wito wa kulima pamba iwapo wanunuzi watashindwa kununua pamba yote.
Mbunge huyo ameongeza kuwa mwaka jana, Waziri Mkuu aliwaita viongozi wa mikoa inayolima pamba na kuwapa maelekezo ya kwenda kufufua zao hilo ambapo wakulima waliitikia wito na mwaka huu wanatarajia kupata mavuno mengi.
Waziri Mkuu amesema ni kweli kuwa mwishoni mwa mwaka jana, Serikali iliwaita viongozi hao ambao ni Wakuu wa Mikoa, Wakurugenzi na Wakuu wa Wilaya ambao walipewa maelekezo ya kwenda kuhamasisha kilimo cha zao hilo na kuwasaidia wakulima kuanzia ngazi ya awali.
Waziri Mkuu amesema Serikali inashiriki kikamilifu katika usimamizi wa zao la pamba kuanzia hatua za maandalizi ya shamba kwa kulima kitaalam, upatikanaji wa pembejeo hadi masoko.
“Mimi mwenyewe mwezi huu nitakuwa na ziara ya kikazi mkoani Mwanza, kwa hiyo kati ya tarehe 15-17, nimeitisha mkutano wa wafanyabiashara wote wa pamba nchini iwe ni wanaosokota nyuzi, kuchambua pamba au kukamua pamba, ili mradi wanajihusisha na pamba,” amesema.
Ili kupata uhakika wa masoko nje ya nchi, Waziri Mkuu amesema Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na Kampuni ya Soko la Bidhaa Tanzania (TMX) inawasiliana na mataifa mbalimbali ili kuhakikisha pamba yote iliyolimwa nchini inanunuliwa.
“Serikali imeweka mkakati wa kuimarisha mazao makuu ya biashara ambayo uzalishaji wake umeanza kupungua likiwemo na zao la pamba. Mengine ni korosho, kahawa, chai na tumbaku, yote kwa pamoja yanachangia kukuza uchumi,” amesema.
Amesema awali wakulima wa mazao makuu matano ya biashara nchini likiwemo na zao la pamba walipunguza uzalishaji baada ya kukosa usimamizi hali iliyoilazimu Serikali ichukue uamuzi wa kuyafufua kwa kuwa historia inaonyesha kwamba mazao hayo yanachangia katika ukuaji wa uchumi wa Taifa.
Akijibu swali kuhusu ukosefu wa dawa za kuulia wadudu ambalo Bw. Ndassa alilalamikia, Waziri Mkuu amesema Serikali imeendelea kuagiza dawa hizo kwa kuwa ni sehemu ya mahitaji ya kilimo cha zao la pamba.
“Wiki iliyopita niliona kwenye habari Mkurugenzi wa Bodi ya Pamba akipokea chupa zaidi za milioni moja na akasema kuwa kuna dawa nyingine chupa zaidi ya milioni mbili zinakuja.”
“Ni jukumu la Bodi hiyo kuhakikisha kuwa dawa za zao la pamba, ziwe za maji au za kupulizia zinapatikana nchini na zinapelekwa kwa wakulima,” alisisitiza.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980,
41193 - DODOMA.
ALHAMISI, FEBRUARI 8, 2018.
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni