.

.

.

.

.

.

.

.
KARIBUNI TUHABARIKE, TUELIMISHANE, TUPEANE HABARI ZA KUKUFANYA UTABASAMU KIDOGO NA MATUKIO YALIYOFANYIWA UCHUNGUZI WA KINA TOKA KILA PEMBE CONTACTS: +255 787 377 722 Email: drweyunga@gmail.com PIA UNAWEZA KUNI FOLLOW KUPITIA INSTAGRAM YANGU @drweyunga | TANGAZA NASI ILI UWAFIKIE WATU WENGI ZAIDI.

Jumapili, 25 Februari 2018

WAKAZI 8,100 WA VIJIJI VYA WANDELA NA DANG'AIDA HAWANA UHAKIKA WA UPATIKANAJI WA MAJI SAFI NA SALAMA

Na,Jumbe Ismailly HANANG 

WAKAZI 8,100 wa Kijiji cha Wandela,kata ya Getanuwasi na Kijiji cha Dang’aida,Kata ya Bassotu,wilayani Hanang,Mkoani Manyara hawana huduma ya maji safi na salama,na hivyo wapo hatarini kupatwa na magonjwa ya kuambukiza kutokana na kunywa maji machafu na wanayochangia na mifugo.

Kati ya wakazi hao,wakazi wa Kijiji cha Wandela ni 4,500 na wakazi wa Kijiji cha Dang’aida ni 3,600 wanaohangaika kutafuta maji na hivyo kulazimika kuyafuata umbali wa kilomita saba kwenda na kurudi hadi katika Kijiji cha Getanuwasi.

Akitoa taarifa hiyo kwa Mbunge wa jimbo la Hanang,Dk.Mary Nangu aliyepo katika ziara ya kutembelea na kukagua shughuli za maendeleo jimboni hapa,Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Wandela,Minaeli Mwanya alisema wananchi wa Kijiji hicho wanakabiliwa na tatizo la upatikanaji wa maji safi na salama tangu mwaka 1993.

“Nilihamia mwaka jana katika Kijiji cha Wandela One,lakini kwa wananchi wa Kijiji cha Wandela wana matatizo ya maji ambapo watu 4,500 wanasumbuka kutafuta maji safi na salama tangu mwaka 1993 hadi leo”alisisitiza Minaeli.

Aidha afisa mtendaji huyo alisisitiza kwamba licha ya jitihada za kupeleka maombi kwenye mamlaka zinazohusika na utafutaji pamoja na utoaji wa huduma hiyo na kupewa matumaini ya kupatikana kwa huduma hiyo,lakini kwa zaidi ya miaka ishirini sasa wananchi hao wamekuwa wakinywa maji huku wakichangia na wanyama.

Naye Kaimu Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Dang’aida,Emanueli James Mosha alisema wananchi 3,600 wa Kijiji hicho hawana uhakika na upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama kutokana na maji wanayokunywa kuwa machafu na wanachangia na wanyama pia.

Akijibu hoja za wananchi hao,Mbunge wa jimbo la Hanang,Dk.Mary Nagu alisema hivi sasa kipaumbele chake ni kujenga miundombinu ya barabara za kuunganisha kijiji kimoja kwenda kingine hadi vijiji vyote 96 vitakapokamilika.

Hata hivyo Mbunge huyo aliwahakikishia wananchi hao kwamba wilaya ya Hanang ni moja kati ya wilaya nchini zenye matatizo ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama na kwamba ili kuondokana na kero hiyo atahakikisha kila kata na vijiji vyote vinapata maji safi na salama.

Kwa upande wao baadhi ya wananchi Kijiji cha Dang’aida,Mwanahamisi Salimu alisema tangu alipohamia katika Kijiji hicho mwaka 1995 alikuta ukame huo wa maji na hivyo kulazimika kufuata maji hayo katika Kijiji cha Hiribadaw.

Alisema baadhi yao walio na wanyama kazi kama vile punda waliweza kuwatumia lakini kwa wasiokuwa nao walilazimika kutoka saa saba usiku na kutembea umbali wa zaidi ya kilomita saba hadi Kijiji hicho kufuta maji.

“Tumekuwa tukitoka saa saba usiku nawaamsha watoto wangu twende kuchota maji na kwa kuwa ni wanafunzi huwaruhusu kurudi nyumbani saa 12 alfajiri ili nao waweze kuwahi kwenda shuleni.”alifafanua mama huyo.

Kwa mujibu wa mwananchi huyo wanafuata maji katika Kijiji cha Kitwanuwasi na kuyanunua kwa bei ya shilingi 1,000/= kwa dramu moja na shilingi mia moja kwa dumu moja.

Hakuna maoni :

Chapisha Maoni