.

.

.

.

.

.

.

.
KARIBUNI TUHABARIKE, TUELIMISHANE, TUPEANE HABARI ZA KUKUFANYA UTABASAMU KIDOGO NA MATUKIO YALIYOFANYIWA UCHUNGUZI WA KINA TOKA KILA PEMBE CONTACTS: +255 787 377 722 Email: drweyunga@gmail.com PIA UNAWEZA KUNI FOLLOW KUPITIA INSTAGRAM YANGU @drweyunga | TANGAZA NASI ILI UWAFIKIE WATU WENGI ZAIDI.

Alhamisi, 1 Machi 2018

CHANGAMTO YA HUDUMA ZA AFYA MBECHA YAPATIWA UFUMBUZI

CHANGAMOTO ya upatikanaji wa huduma za afya iliyokuwa inawakabili wakazi wa kijiji cha Mbecha kata ya Nanganga imekuwa historia baada ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa zahanati.

Amesema wakazi hao walikuwa wakipata shida ya kutembea umbali mrefu kufuata huduma za afya katika vijiji vya jirani mara mtu anapougua ikiwa ni pamoja na dharura mbalimbali zikiwemo za wajawazito.

Waziri Mkuu ambaye ni mbunge wa jimbo la Ruangwa ameweka jiwe hilo la msingi leo (Alhamisi, Machi 01, 2018), alipowasili mkoani Lindi kwa ziara ya kikazi katika jimbo la Ruangwa. Ujenzi wa zahanati hiyo umefadhiliwa na African Relief Organisation.

“Mbecha mtu akiugua tulikuwa tunapata shida ya sehemu ya kupata huduma za matibabu, leo matibabu yatakuwa yanapatikana hapa kijijini. Kwa niaba ya Wanaruangwa nawashukuru sana viongozi wa African Relief Organisation”.

Waziri Mkuu amesema kuwa mkakati wa Rais Dkt. John Magufuli ni kuimarisha sekta ya afya kwa kujenga na kuboresha vituo vya afya ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma za afya karibu na makazi yao.

Awali, Mtendaji wa Kijiji cha Mbecha, Bw. Alfan Ngaeje alisema wazo la ujenzi wa zahanati ya kijiji hicho lilianza 1987, ambapo utekelezaji wake ulikwama kutokana na hali duni ya kiuchumi iliyokuwa ikiwakabili wakazi wake.

Alisema wananchi wengi waliendelea kupata shida ya kupata huduma za afya hasa akinamama wajawazito na watoto waliokuwa wakitembea umbali mrefu kufuata huduma hiyo kwenye zahanati za vijiji vya jirani.

Hivyo alimshukuru Waziri Mkuu kwa niaba ya wakazi wa kijiji hicho kwa kuwatafutia mfadhili aliyewajengea zahanati hiyo ambayo ipo katika hatua za mwisho kukamilika.

Mtendaji huyo alisema huduma zitakazokuwa zinatolewa kwenye zahanati hiyo ni pamoja na matibabu ya wagonjwa wa nje (OPD), kliniki kwa wajawazito na watoto, chanjo na uzazi wa mpango.

Huduma nyingine ni kuzuia maambukizi wa virusi vya ukimwi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto, kujifungua, elimu ya kujikinga na mangonjwa mbalimbali. Jumla ya kaya 594 zenye wakazi 2,485 wanatarajiwa kunufaika na zahanati hiyo.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
ALHAMISI, MACHI 01, 2018.

Hakuna maoni :

Chapisha Maoni