SERIKALI imepeleka sh. bilioni 1.92
katika Halmashauri ya Mji wa Nanyamba wilayani Mtwara kwa ajili ya
ujenzi na uboreshaji wa vituo vya afya.
Hayo yalibainika jana (Jumatano,
Februari 28, 2018) wakati Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alipozungumza
na wakazi wa Halmashauri hiyo, wakati wa ziara yake.
Waziri Mkuu ambaye yuko mkoani
Mtwara kwa ziara ya kikazi alisema fedha hizo zilitolewa na Serikali
ili kuimarisha upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi.
Alisema jumla ya sh. bilioni 1.2
zimetolewa kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya cha kwenye Kata ya
Njengwa, ambapo aliwasisitiza watendaji kutobadilisha matumizi.
Waziri Mkuu alisema ujenzi huo
utahusisha chumba cha upasuaji, maabara, chumba cha kujifungulia,
jengo la mama na mtoto na wodi ya wanawake na wanaume, eneo la
kuchomea taka na chumba cha kuhifhadhia maiti.
“Serikali imeamua kuimarisha sekta
ya afya kwa kujenga na kuboresha vituo vya afya ili kuhakikisha
wananchi wanapata huduma za afya karibu na makazi yao.”
Aidha, Waziri Mkuu aliwataka
wananchi hao kuendelea kuiunga mkono Serikali yao, ambayo imedhamiria
kuwatumikia ili waweze kupata maendeleo.
Pia Waziri Mkuu alisema Serikali
inatarajia kuipitia upya sheria ya elimu pamoja na sheria ya mtoto
ili kuweka masharti ya kumlinda mtoto wa kike hususani kudhibiti
mimba kwa wanafunzi.
Awali, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Bw.
Gelasius Byakanwa alisema Serikali itawachukulia hatua watu wote
watakaobainika kuwapa watoto wa kike dawa za uzazi wa mpango ili
kuwazuia wasipate mimba.
Bw. Byakanwa alisema wanafunzi wa
kike katika Halmashauri ya Mji wa Nanyamba wamebainika kuwa wanatumia
dawa za kuzuia mimba wakiwa shuleni, hivyo kuwaruhusu kushiriki
katika matendo yasiyokuwa ya kimasomo.
Alisema Serikali itafanya msako wa
kuwatafuta wote wanaotumia dawa hizo pamoja na wanaowapa na
watakaobainika hatua kali zitachukuliwa dhidi yao kwa sababu jambo ni
hatari kwa maendeleo ya wanafunzi hao.
Naye, Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya
Rais-TAMISEMI Bw. Josephat Kakunda alisema alisema Serikali imepeleka
sh. bilioni 1.92 katika Halmashauri ya Mji wa Nanyamba ili kuboresha
huduma za afya.
Asema kati yake sh. milioni 700
zilipelekwa katika kituo cha afya cha Nanyamba ambapo sh. milioni 300
zilitumika kwa ajili ya ununuzi wa dawa na sh milioni 400 ukarabati
wa kituo, huku sh. bilioni 1.2 ujenzi wa kituo cha afya cha kata ya
Njengwa.
Haya hivyo, Waziri huyo alisema kuwa
Serikali inampango wa kuifanyia marekebisho sheria ya mtoto kwa
kuondoa kipengele cha dhamana kwa watu watakaotuhumiwa kuwapa mimba
watoto wa shule.
Alisema hatua hiyo inatokana na
baadhi ya watuhumiwa hao wanapopewa dhamana kwenda kuzungumza na
wazazi au walezi wa binti jambo linalochangia katika kuharibu
ushahidi.” Ni bora wakakaa rumande hadi hukumu itakapotolewa na
kama hawatokutwa na hatia watarudi uraiani”.
(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
ALHAMISI, MACHI 01, 2018.
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni