Michael Wambura ( mwenye suti ) wakati alipofika makao makuu ya Simba mtaa wa msimbazi kuchukua fomu za kugombea Urais wa timu hiyo.
Kamati ya uchaguzi ya klabu ya soka ya Simba ya jijini Dar es Salaam imemuengua mgombea wa nafasi ya Urais wa timu hiyo katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika June 29' 2014 Michael Wambura.
Mwenyekiti wa kamati ya uchaguzi ya Simba, Damas Ndumbaro amesema kamati yake imefikia uamuzi huo baada ya kuridhika kuwa, Wambura alikiuka katiba ya Simba kwa kuipeleka timu hiyo mahakamani, na pia kusimamishwa uanachama May 05' 2010.
Hata hivyo taarifa zinasema mgombea huyo ambaye amekuwa akikumbwa na misuko suko kila anapojitokeza kuwania nafasi za uongozi wa mpira, atakata rufaa ili kuona haki inapatikana ya yeye kuwania nafasi hiyo ya Urais wa Simba.
Kuondolewa kwa jina la Wambura, kuna maanisha kuwa wagombea wa nafasi hiyo waliosalia ni Evance Aveva na John Tupa.
Kuondolewa kwa jina la Wambura kumepokelewa kwa hisia tofauti na wadau wa soka nchini, wengi wakisema mgombea huyo amekuwa akionekana tishio kwa wagombea wenzake hali inayopelekea kukutana na vizingiti vingi ikiwa ni pamoja na jina lake kuenguliwa.
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni