Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Mart
Nooij ametangaza kikosi cha wachezaji 24 kwa ajili ya mechi ya
kalenda ya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) dhidi ya
Swaziland itakayochezwa Novemba 16 mwaka huu jijini Mbabane.
Akizungumza Dar es Salaam, leo
(Novemba 5 mwaka huu), Nooij alisema kikosi hicho kitaingia kambini
Novemba 10 mwaka huu saa 6 mchana kwenye hoteli ya Accomondia, na
siku hiyo hiyo jioni kitafanya mazoezi kwenye Uwanja wa Gymkhana.
Novemba 11 mwaka huu, Taifa Stars
inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager itaondoka kwenda Afrika
Kusini ambapo itaweka kambi ya siku mbili kabla ya kuondoka Novemba
13 mwaka huu kwenda Swaziland.
Wachezaji walioitwa kwenye kikosi
hicho ni makipa Aishi Manula (Azam) na Deogratias Munishi (Yanga).
Mabeki ni Abubakar Mtiro (Kagera Sugar), Aggrey Morris (Azam),
Emmanuel Simwanda (African Lyon), Hassan Isihaka (Simba), Kelvin
Yondani (Yanga), Nadir Haroub (Yanga), Osacr Joshua (Yanga), Said
Moradi (Azam), Salim Mbonde (Mtibwa Sugar) na Shomari Kapombe (Azam).
Viungo ni Amri Kiemba (Simba),
Erasto Nyoni (Azam), Haruna Chanongo (Simba), Himid Mao (Azam),
Mwinyi Kazimoto (Al Markhiya, Qatar), Said Ndemla (Simba) na Salum
Abubakar (Azam).
Washambuliaji ni Juma Luizio (ZESCO,
Zambia), Mbwana Samata (TP Mazembe, DR Congo), Mrisho Ngasa (Yanga),
Simon Msuva (Yanga) na Thomas Ulimwengu (TP Mazembe, DR Congo).
WADAU KUBUNI JEZI MPYA YA TIMU ZA
TAIFA
Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF) linakaribisha wabunifu, kubuni mwonekano wa jezi mpya
za timu ya Taifa kwa mechi za nyumbani na ugenini. Ubunifu ni lazima
uzingatie rangi za bendera ya Taifa.
Mshindi wa jezi ya nyumbani atapata
sh. 1,000,000 (milioni moja), na mshindi wa jezi ya ugenini atapata
pia sh. 1,000,000 (milioni moja).
Ubunifu utumwe kwenye anwani ya
barua pepe: info@tff.or.tz au uwasilishwe kwa CD au flash zikiwa
katika mfumo wa PDF katika ofisi za TFF zilizopo ghorofa ya tatu
katika Jengo la PPF Tower, Mtaa wa Ohio na Garden Avenue. Mwisho wa
kupokea designs ni Novemba 15, 2014.
Kwa maelezo zaidi unaweza
kuwasiliana nasi kwa simu namba; 0713 210242 au 0714 634838.
MPANDA UTD, UJENZI RUKWA KUANZA SDL
Michuano ya Ligi Daraja la Pili
(SDL) inayoshirikisha timu 24 katika makundi manne ya timu sita sita
kwa mtindo wa nyumbani na ugenini inaanza kutimua vumbi Novemba 22
mwaka huu ambapo Mpanda United itakuwa mwenyeji wa Ujenzi Rukwa.
Mechi hiyo ya kundi A itachezwa
kwenye Uwanja wa Mandela mjini Sumbawanga. Siku hiyo hiyo katika
kundi hilo kutakuwa na mechi kati ya Mvuvumwa FC na CDA (Lake
Tanganyika, Kigoma), na Milambo dhidi ya Singida United kwenye Uwanja
wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora.
Kundi B mechi za ufunguzi ni kati ya
Pamba na JKT Rwamkoma kwenye Uwanja wa CCM Kirumba huku Bulyanhulu FC
ikiwa mwenyeji wa AFC kwenye Uwanja wa Bulyanhulu mkoani Shinyanga.
Abajalo FC ya Dar es Salaam
itaikaribisha Kariakoo FC ya Lindi kwenye mechi ya kundi C
itakayochezwa Uwanja wa Karume. Nazo Kiluvya United na Transit Camp
zitaoneshana kazi kwenye Uwanja wa Mabatini uliopo Mlandizi mkoani
Pwani.
Kundi D mechi tatu za ufunguzi ni
kati ya Town Small Boys na Volcano FC (Uwanja wa Majimaji, Songea),
Njombe Mji na Mkamba Rangers (Uwanja wa Sabasaba, Njombe), na Wenda
FC dhidi ya Magereza Iringa kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.
IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA
MIGUU TANZANIA (TFF)
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni