.

.

.

.

.

.

.

.
KARIBUNI TUHABARIKE, TUELIMISHANE, TUPEANE HABARI ZA KUKUFANYA UTABASAMU KIDOGO NA MATUKIO YALIYOFANYIWA UCHUNGUZI WA KINA TOKA KILA PEMBE CONTACTS: +255 787 377 722 Email: drweyunga@gmail.com PIA UNAWEZA KUNI FOLLOW KUPITIA INSTAGRAM YANGU @drweyunga | TANGAZA NASI ILI UWAFIKIE WATU WENGI ZAIDI.

Alhamisi, 22 Januari 2015

PANDE MBILI ZINAZOKINZANA SUDAN KUSINI ZATIA SAINI MAKUBALIANO MJINI ARUSHA

Mazungumzo ya kutafuta amani nchini Sudani Kusini, hatimaye jana yamemalizika, baada ya pande zote mbili zinazokinzana kukubali kusaini makubaliano zaidi ya 40 waliojiwekea jijini Arusha.

Baadhi ya makubaliano hayo ni pamoja na kufanyia marekebisho katiba ya chama, kupunguza madaraka ya raisi, kuongeza idadi ya wajumbe katika kamati kuu ya chama, kukubali kuwajibika wote kwa yote yaliotokea na kuwaomba msamaha wananchi wa Sudani Kusini kwa kuwasababishia
machafuko na vita.

Mengine ni pamoja na haki ya kila mwanachama kugombea uongozi, kuleta mabadiliko ya kidemokrasia katika chama, utawala bora na uwazi katika chama na kutumia makubaliano ya Arusha kuharakisha mazungumzo ya Adis Ababa.

Akisoma makubaliano hayo mara baada ya kusaini pande hizo zinazokinzana, Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Abdulraham Kinana, amewaomba kutimiza kwa dhati maazimio waliojiwekea na kuyatekeleza kwa faida ya nchi yao.

Naye Rais wa Tanzania Jakaya Kikwete, ameungana na wenzake kadhaa katika kushuhudia tukio la kihistoria la utilianaji sahihi ya makubaliano ya amani na kusitisha mapigano katika nchi mpya ya Sudan Kusini.

Amesema ni vema wahusika wa mapigano hayo wakatimiza maazimio waliojiweka kwa utekelezaji na kuwapongeza kwa uamuzi wa kukubali kusaini makubaliano hayo na kuwataka wayatimize ili kurahisisha utendaji wao wa kazi.

Kikwete amesema kila kiongozi kabla ya kufanya kitu ni lazima atafakari mara mbili jambo lolote analotaka kufanya, kuwa lina faida kwa wananchi wa nchi hiyo au la.

Naye Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta, amewapongeza sana kwa kukubali kusaini makubaliano hayo na kuwakaribisha kwake pale watakapohitaji msaada wowote kwa ajili ya kuharakisha maendeleo ya nchi hiyo.

Rais wa Uganda Yoweri Museveni, naye ameungana na wenzake kuwapongeza kwa kufikia hatua hiyo na kusema nchi hiyo ndugu wa karibu na Uganda na hivyo imekuwa furaha kuona sasa wanakwenda kutulia bila mapigano.


Baada ya hatuba hizo za wosia kwa wapinzani hao ndani ya chama kimoja, Rais Salva Kiir Mayardit na Mpinzani wake, Riek Machar ambaye ndiye aliyekuwa makamu wa Rais kabla ya mtafaruku, walionekana wenye furaha muda wote na kupongezana kwa kupeana mikono mara kwa mara, huku
wakishangiliwa na wapambe wao waliofurika ndani ya ukumbi wa Ngurudoto, Jijini Arusha.

Wakinzani hao wote kwa pamoja wameahidi kutimiza kwa vitendo makubaliano hayo na kupeana ushirikiano katika mambo yote na kuwashukuru wote waliohusika kusuluhisha ugomvi huo hadi kufikia hatua hiyo.

Viongozi wengine walioshuhudia makubaliano ya amani kwa Sudani Kusini ni pamoja na Makamu wa Rais, Mohammed Gharib Bilal, Makamu wa Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa na mjane wa kiongozi wa kwanza wa chama cha SPLM John Garang, ambaye ndiye aliyeongoza harakati za
kupigania uhuru, kuelekea kujitenga kwa nchi hiyo, kutoka kwa iliyokuwa Jamhuri ya Sudan.

Katika vita hivyo zaidi ya watu 20,000 wamepoteza maisha katika mapigano yaliyozuka Sudani Kusini mara baada ya nchi hiyo kujitenga na iliyokuwa Jamhuri ya Sudan mwaka 2011 na wananchi zaidi ya milioni moja hawana makazi ya kuishi sababu ya vita hivyo.

Mazungumzo ya awali ya vikundi vinavyozozana katika chama cha SPLM cha Sudan Kusini, yaliongozwa na ujumbe mzito wa ngazi ya Juu wa Chama cha Mapinduzi ( CCM), ili kutafuta suluhu ya mgogoro ndani ya chama cha hicho kinachotawala nchini Sudani Kusini.

Ujumbe huo uliongozwa na Makamu Mwenyekiti Mstaafu wa CCM Balozi John Samwel Malecela, Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara Philip Mangula na Katibu Mkuu wa Chama hicho Abdulraham Kinana.

Kwa upande wa SPLM, mazungumzo hayo yaliongozwa na Taban Deng Gai,Daniel
Awet Akot, na Deng Alor Kuol.

Miongoni mwa makundi hayo ni kutoka chama cha SPLM, Kundi kutoka kwa wafungwa wa kisiasa, pamoja na kundi lililojitenga kutoka chama cha SPLM.

Chama hicho kiligawanyika makundi matatu na kusababisha jeshi kwa upande wake, kumeguka katika makundi hayo na kusababisha wananchi nao kugawanyika katika makundi hayo matatu .

Mazungumzo hayo pia yalihudhuriwa na wawakilishi kutoka EU, AU,Norway Egypt,Umoja wa Mataifa na Ethiopia.

Mwisho

Hakuna maoni :

Chapisha Maoni